Mamlaka husika nchini Burundi zimekataa kukipatia usajili chama kipya cha upinzani cha Amizero y'Abarundi kilichoanzishwa hivi karibuni na kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Agathon Rwasa.
Rwasa alianzisha chama cha National Freedom Front au FNL-Amizero y'Abarundi yenye maana ya "Matumaini kwa Waruundi" baada ya kupitishwa kwa mabadiliko ya katiba mwezi Mei mwaka huu, mabadiliko ambayo yanakataza muungano wa wagombea binafsi kushiriki kwenye uchaguzi.
Barua kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Burundi imesema kuwa, Chama cha Rwasa kimenyimwa usajili kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ya kushabihiana nara za chama hicho na chama kingine ambacho tayari kimekwishasajiliwa.
Hata hivyo baadhi ya duru hasa za mrengo wa upinzani zinatilia shaka sababu iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Burundi ya kukinyima usajili chama hicho cha upinzani ambacho kinaonekana kuwa na nguvu.
Licha ya mara kadhaa Rwasa kuonekana kutokuwa mpinzani wa kweli kwa chama tawala cha CNDD-FDD, muungano wake wa Amizero y'Abarundi ulipata asilimia 17 ya kura katika uchaguzi wa mwaka 2015 na kushika nasafari ya pili baada ya chama tawala.
Hivi karibuni Agathon Rwasa, mwanasiasa mkongwe na mashuhuri wa upinzani nchini Burundi, alisema itawalazimu wanasiasa wa upinzani kujizatiti katika vyama vyao ili baadaye kujiweka pamoja wakati wa mpambano wa uchaguzi kwa mujibu wa katiba mpya.
Burundi ilitumbukia katika machafuko ya kisiasa mapema mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kugombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu; hatua ambayo ilitajwa kuwa ni kinyume na katiba ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇