Mwakilishi wa Tazania Kudumu UN Tuvaco Manongi akizungumza katika kikao hicho |
Na Mwandishi Maalum, New York
Tanzania imeitaka Jumuiya ya Kimataifa kupunguza matumizi makubwa katika kujilimbikizia silaha zikiwamo za maangamizi na badala yake fedha hizo zielekezwe katika kusaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ( agenda 2030).
Wito huo umetolewa siku ya jumanne na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika pamoja na mambo mengine, usalama wa kimataifa likiwamo suala ya upokonyaji wa silaha ilipokuwa ikijadilia ajenda ya upokonyaji silaha.
“ Kila Septemba 26 ya kila mwaka, tunaadhimisha siku ya kimataifa ya kumaliza kabisa silaha za nyukilia. Lakini wakati Kamati hii ikianza mijadala yake hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa ya kulimaliza tatizo hili” akasema Balozi Manongi na kuongeza, badala yake dunia inashuhudia nchi ambazo zinazomiliki silaha za nyukilia zikiendelea na kasi ya kuziongeza ikiwa ni pamoja na kuwekeza mabilioni ya dola katika kuzifanyia marekebisho na kuziimarisha.
“Kwa Tanzania, upokonyaiji wa silaha na maendeleo ni mambo yanayohusiana. Kiasi cha fedha ambacho kinaelekezwa katika matumizi ya kijeshi yangeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu. Ni kwa sababu hiyo tunaona umuhimu wa kazi za Kamati hii”.Amesisitiza Balozi.
Akizungumzia nafasi ya Umoja wa Mataifa katika kusimamia suala na upokonyaji wa silaha kupitia Taasisi zake, Balozi amesema licha ya ugumu na changamoto katika eneo hilo. Tanzania bado inamatumaini ya Umoja wa Mataifa kama chombo muhimu kinachoweza kudhibiti usambaaji wa silaha za maangamizi zikiwamo silaha ndogo ndogo, za kati na nyepesi.
Pamoja na kuelezea namna Nchi zenye silaha za maangamizi zinavyoendelea kujilibikizia silaha hizo ikiwani ni pamoja na kuziimarisha ili ziwe za kisasa. Balozi pia ametumia fursa hiyo kutahadharisha dhidi ya hasara za kibinadamu zinazoweza kutokea dhidi ya matumzi ya silaha hizo.
Na kwa sababu hiyo, Tanzania imezisihi nchi zinazomiliki silaha za nyukilia kutumiza wajibu wao kisheria ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kuangamiza silaha hizo kwa uwazi na bila kuchelewa na kwa kuzingatia makubaliano ya Mkataba wa Kimataifa wa upokonyaji wa silaha.
Tanzania pia imekumbushia haja na umuhimu wa nchi ambazo hazina silaha za nyukilia kutonyimwa fursa ya kutumia teknolojia ya nyukilia kwa shughuli salama zikiwamo za utafiti na shughuli nyingine za maendeleo na ustawi wa nchi zao.
Kuhusu Ukanda Huru zisizokuwa na silaha za nyukilia, Tanzania ambayo ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Palendaba (Africa Nuclear Free Zone) inaunga mkono uwepo wa Kanda huru ambazo hazina silaha za nyukilia.
Katika hatua nyingine , Tanzania imekaribisha kuanzishwa kwa Benki ya Teknolojia kwa nchi zilizonyuma kimaendeleo ( Technology Bank for Least Developing Countries).
Kuanzishwa kwa bank hiyo kunalenga pamoja na mambo mengine kuzisaidia nchi za LDC’s kuwa na fursa na uwezo wa kutumia teknolojia sahihi kutoka kwa mataifa yaliyoendelea.
Hayo yameelezwa na Bw. Songalieli Shilla, Afisa Mkuu Mambo ya Nje katika Uwakilishi wa kudumu wa Tanzania wakati alipochangia kwa niaba ya Tanzania majadiliano ya Kamati ya Pili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ilipokuwa ikijadili masuala mtambuka yakiwamo ya ukuaji wa uchumi na maendeleo.
Tanzania ikasisitiza kwamba kuanzishwa kwa Banki hiyo kutazisaidia nchi za LDC’s kuingia katika ushindani na mataifa yalioendelea. Na kwamba Tanzania inafarijika pia kwamba Benki hiyo itaendelea kuzisaidia hata zile nchi ambazo zitakuwa zimefunzu kutoka nchi zenye uchumi wa chini na kwenda kwenye uchumi wa kati.
Benki hiyo ambayo chimbuko lake ni mkutano uliofanyika mwaka 2011 nchini Uturuki na ambayo tayari maandalizi ya awali yamekwisha kufanyika inatarajiwa kuzinduliwa mwakani.
Kamati ya Pili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inahusima na masuala ya Uchumi na Fedha, na katika mkutano huo, pamoja na kukaribisha uanzishwaji wa Benki hiyo, pia Tanzania imezungumzia changamoto mbalimbali ambazo zinakweza kukwamisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu hususani kwa nchi zinazoendelea.
Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji wa raslimali fedha kutoka vyanzo vya ndani na kutoka kwa wadau na washirika wa maendeleo.
Baada ya kukamilika kwa Mkutano na Majadiliano ya jumla ya Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa, mkutano uliowakutanisha viongozi wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali duniani. Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, kupitia Kamati Sita zinazounda Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, zimeingia katika ngwe nyingine muhimu ambapo sasa wajumbe wanakutana kupitia Kamati hizo kujadiliana agenda na maazimio mbalimbali kuanzia yale yanayohusu uchumi, fedha na maendeleo, haki za binadamu, ustawi wa jamii, Amani na usalama, umalizwaji wa ukoloni, utawala wa sheria , sheria za kimataifa na bajeti na utawala.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇