LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 7, 2026

WANAFUNZI LUKUKI WA TIA WANUAFAIKA NA MIKOPO YA ELIMU YA JUU

 Na Richard Mwaikenda, Dodoma

WANAFUNZI 19,342 wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu, hatua iliyowawezesha kuendelea na masomo yao na kutimiza ndoto za kitaaluma katika kipindi cha utekelezaji wa mipango ya taasisi hiyo.

‎Wanafunzi hao wamenufaika na mikopo hiyo wakiwa katika kampasi za TIA zilizopo Tanga, Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Mbeya, Kigoma na Mtwara.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Septemba 7, 2026, Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Amos Pallangyo, alisema mikopo hiyo imekuwa sehemu muhimu ya kuwezesha wanafunzi kutoka makundi mbalimbali kupata elimu ya juu.

Prof. Pallangyo alisema TIA imeendelea kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya juu nchini sambamba na kuimarisha uwezo wa taasisi hiyo kuhudumia ongezeko la wanafunzi.

Alisema mwaka 2021/22 TIA ilikuwa na kampasi sita zilizopo Dar es Salaam, Singida, Mbeya, Mtwara, Mwanza na Kigoma, lakini hadi mwaka 2025/26 idadi hiyo imeongezeka na kufikia kampasi nane baada ya kuongezwa kwa kampasi za Tanga na Zanzibar.

“Ukuaji huo wa kimuundo umeenda sambamba na ongezeko kubwa la wanafunzi. Idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 24,494 mwaka 2021/22 hadi 37,397 mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 52.7,” alisema.

Alisema ongezeko hilo limeongeza pia uwezo wa TIA kuhudumia wanafunzi kwa asilimia 35, huku taasisi ikiendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza programu zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira.


PROGRAMU ZAONGEZEKA

Kwa upande wa programu za masomo, Prof. Pallangyo alisema TIA imeongeza idadi ya programu kutoka 49 mwaka 2021/22 hadi kufikia 54 mwaka 2025/26.

Alisema miongoni mwa programu hizo mpya ni Shahada ya Maendeleo ya Biashara na Ujasiriamali pamoja na Shahada ya Uchumi na Fedha, ambazo zimeanzishwa kwa lengo la kuwaandaa vijana wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya uchumi wa sasa.

‎“Programu hizi zinalenga moja kwa moja kukuza vijana wenye ujuzi wa biashara, ujasiriamali, uchumi na fedha, hivyo kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kujiajiri,” alisema.


WAHITIMU 62,680

Prof. Pallangyo alisema mafanikio ya TIA hayapimwi kwa ongezeko la idadi ya wanafunzi na kampasi pekee, bali pia kwa idadi ya wataalamu wanaozalishwa na kuingia katika soko la ajira.

Alisema jumla ya wahitimu 62,680 wamehitimu katika kipindi hicho na kuingia katika soko la ajira, ujasiriamali na kutoa huduma mbalimbali za kitaaluma.

Alisema takwimu hizo zinaonesha mchango wa TIA katika kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi unaohitajika katika utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya Taifa.

“Ukuaji wa TIA haujikiti tu katika idadi ya wanafunzi, bali unaendelea kutengeneza rasilimali watu inayohitajika katika uchumi wa Taifa letu,” alisema.

Alisema katika mwaka wa fedha 2026/27, TIA itaendelea kuimarisha programu za elimu, kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu na kuwekeza katika mazingira bora ya kujifunzia ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya elimu ya uhasibu, biashara, uchumi na maeneo mengine yanayohusiana na taaluma hizo.

Prof. Pallangyo alikuwa akielezea utekelezaji wa TIA katika mwaka wa fedha 2025/26 pamoja na mwelekeo wa taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari–MAELEZO, jijini Dodoma.


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages