LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 24, 2026

MWANRI: OLE WAO WANAOTUMIA RUSHWA KUSAKA UONGOZI CCM

Na William PaulI, Gazeti la Uhuru, Siha
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Aggrey Mwanri, ameahidi Chama kitawashughulikia viongozi wote wanaotaka kupewa nafasi za uongozi kwa kutumia rushwa.

Mwanri alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya CCM, wilayani Siha ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Kilimanjaro.

Alisema mwakani CCM itafanya uchaguzi wake wa ndani, na haipo tayari kuona viongozi wanachaguliwa kwa kutoa rushwa.

“Wananchi wana kero zinazowakabili tumeelekeza viongozi kuanzia wenyeviti, madiwani na wabunge, nendeni kwa wananchi mkasikilize hizo kero na kuzitafutia majawabu,” alisema Mwanri.

Alisema wananchi wana matarajio na matumaini na Chama, japokuwa matatizo mengine yapo ndani ya halmashauri, huku akiwataka wakurugenzi kushirikiana na madiwani kutatua kero hizo.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema yapo makundi ambayo yamezalishwa ndani ya Chama kutokana na uchaguzi mkuu mwaka 2025 na hayajavunjwa hadi hivi sasa, ingawa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, alipofika mkoani Kilimanjaro alitoa siku 60 tatizo hilo liwe limekwisha.

Alisema pamoja na kusisitiza hivyo, Wasira alionya wahusika watakaokaidi watachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za Chama.

MAAGIZO KWA RC
Mwanri alitumia mkutano huo kumwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, kusaidia kurudisha umoja na mshikamono katika Jimbo la Siha na kuahidi kuwasamehe waliomkosea.

Aliwaomba wananchi wa Wilaya ya Siha kurudisha umoja, akiahidi katika uongozi wake hatolipiza kisasi.

"Kama kuna mtu yeyote ana wasiwasi na mimi nitalipiza kisasi, imani yangu hainiruhusu kulipa kisasi na kama kuna yeyote alinikosea, leo (jana) natangaza msamaha," alisema.

Aliwataka wananchi wanapoona watu wanawagawanya kwa udini na ukabila kuwagombeza na kuwazomea kwa kuwa ni jambo baya kwa jamii.

Alisema vitu ambavyo vilichangia kuwaunganisha wananchi na kuwaletea maendeleo vinapaswa kuendelea kuungwa mkono.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema suala la umilikishwaji ardhi kwa wananchi wa Siha wafanye shughuli za maendeleo ni tatizo, ambapo atakwenda kuziandikia barua mamlaka husika kuona uwezo wa kumilikisha ardhi hiyo kwa wananchi.

MWENYEKITI WA CCM K’NJARO
Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro, Patrick Boisafi, alisema uteuzi wa Aggrey kuwa Naibu Katibu Mkuu haukuwa kwa bahati mbaya, bali umetokana na utendaji kazi wake.

Boisafi alisema baada ya kuteuliwa na kukabidhiwa ofisi, Mwanri alitumia muda wake kupitia mafaili na kutambua majukumu anayopaswa kuyatekeleza kwa vitendo.

Aliwataka wananchi wa Siha kutomwona kama mtu wa kusukuma ndani, bali ni mtu wa kusimamia haki na mcha Mungu na ana wajibu wa kuwatumikia Watanzania na siyo Wanakilimanjaro pekee.

“Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, anamtegemea  Mwanri katika mambo mbalimbali na ndiyo maana amemrudisha ndani ya Chama kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu na hii ni heshima kubwa kwa wananchi wa Siha, niwaombe tumuunge mkono," alisema Boisafi.

Aliwataka viongozi wa Chama kuanzia ngazi ya shina kuwa walinzi wa kusimamia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kuangalia thamani ya fedha iendane na thamani ya mradi husika.

Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel, alisema jimbo lipo salama na kumwomba Mwanri kuendelea kushughulikia matatizo katika majimbo mengine.


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages