LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 7, 2026

DKT. RWAKATARE ATOA MSAADA KWA MABINTI 300 WA FDC IFAKARA

  Mbunge wa Jimbo la Mlimba,Mhe. Kellen Rose Rwakatare, ametembelea mabinti 300 wanaosoma katika Chuo cha Maendeleo (FDC) Ifakara na kuwapatia mahitaji mbalimbali muhimu yatakayowasaidia kuendelea na masomo yao ya ufundi stadi.

Katika ziara hiyo, Mbunge huyo alipata fursa ya kukutana na wanafunzi hao, kuzungumza nao na kusikiliza changamoto wanazokutana nazo katika safari yao ya elimu ya ufundi. Alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwatia moyo mabinti hao kuendelea kujifunza kwa bidii na kutumia kikamilifu fursa waliyoipata ya kupata elimu itakayowasaidia kujitegemea kiuchumi.

Aidha, alisisitiza kuwa juhudi hizo zinaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha vijana, hususan wasichana, kupata elimu na ujuzi utakaowasaidia kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

Akizungumza na wanafunzi hao, Mhe. Rwakatare aliwahimiza kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu pamoja na kutumia vyema fursa waliyoipata ili waweze kuwa chachu ya mabadiliko katika familia na jamii zao.

Ziara hiyo pia ilisindikizwa na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Kilombero, ambao walipongeza juhudi za Mbunge huyo katika kuunga mkono elimu ya ufundi stadi kwa vijana wa kike, wakieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza fursa za ajira na kujitegemea kwa vijana katika jamii.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages