LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 6, 2026

MARIA NYERERE AKABIDHIWA TUZO YA MUMEWE, ATOA NENO...

  MAMA wa Taifa, Maria Nyerere, ametoa wito mzito kwa Watanzania kudumisha mshikamano na kutumia mazungumzo kama njia pekee ya kuvuka changamoto zinazolikabili taifa kwa sasa.

Akizungumza jana Januari 5, 2026, nyumbani kwake Msasani wakati anakabidhiwa tuzo ya Mwalimu Julius Nyerere iliyotolewa na Angola kwa mchango wake wakati nchi hiyo inapigania uhuru, Mama Maria amewataka Watanzania kutoishi kwa kukata tamaa, bali kutambua hatua ambazo nchi imepitia tangu enzi za Mwalimu Nyerere.
Mama Maria amechambua historia ya nchi kupitia makundi matatu, akisisitiza kuwa kila kizazi kina deni kwa taifa lake:
Alisema kundi la Kwanza ni lile lililopigania na kuleta Uhuru wa Bendera, likiongozwa na waasisi wa taifa hili.
Alilitaja kundi la pili: Ambalo lilijenga Misingi ya nchi, kuweka mifumo ya utawala na huduma za kijamii.
Kundi la Tatu alisema ni kizazi cha sasa, ambacho alikielezea kuwa kina jukumu la Kuendeleza na Kuona Mwanga Mkubwa Zaidi wa maendeleo.
"Msikate tamaa. Kundi la kwanza lilitupa uhuru wa bendera, la pili likajenga misingi. Hili la tatu sasa linaona mwanga mkubwa zaidi. Tunachohitaji ni kukubaliana wote, tukae chini na kuzungumza ili kuelewana namna ya kuifikisha nchi mbele," alisema Mama Maria.
Kauli hizo amezitoa wakati akipokea nishani ya heshima iliyotolewa na Serikali ya Angola kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kama ishara ya kuthamini mchango wake katika ukombozi.
Nishani hiyo ilikabidhiwa kwake na Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, akiwa na Balozi wa Angola nchini, Domingos De Almeida Da Silva Coelho. Tukio hilo limeonekana kuwa kielelezo kuwa misingi iliyowekwa na kundi la kwanza na la pili bado inaheshimika kimataifa.


 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages