LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 6, 2025

TANZANIA YAZITAKA TAASISI, MATAIFA YA NJE KUTAMBUA KUANZISHWA KWA TUME YA UCHUNGUZI

 Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa imepokea na kuyazingatia matamko ya umma yaliyotolewa nyakati mbalimbali na Wadau wa maendeleo na Nchi Rafiki za Ubelgiji, Kanada, Denmark, Ujumbe wa Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa, Ghana, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Poland, Slovakia, Hispania, Uswizi, Sweden, Ufalme wa Muungano (Uingereza), Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Marekani na Taasisi ya Thabo Mbeki kuhusu Tanzania na matukio yaliyojitokeza siku ya uchaguzi tarehe 29 Oktoba 2025.


Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini imeeleza kuwa Tanzania imepokea kwa wasiwasi hasa maudhui ya matamko haya, licha ya mazungumzo ya wazi yaliyofanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wajumbe wa Jumuiya ya Kidiplomasia waliowekwa Nchini Tanzania yaliyofanyika tarehe 28 Novemba 2025. 

Imeeleza zaidi kuwa pamoja na kwamba Tanzania inatambua mchango wa Jumuiya ya kimataifa katika kuimarisha demokrasia na maendeleo ya kijamii na kisiasa Nchini, ni muhimu pia kutambua kuanzishwa kwa Tume ya Uchunguzi ambayo itachunguza matukio ya vurugu za baada ya uchaguzi na kutoa ripoti.

Uchunguzi na ripoti hiyo vitatoa uelewa juu ya matukio yaliyotokea na kuwa msingi wa ushirikiano wa kujenga mustakabali bora na kwamba Tanzania itaendelea kujikita katika ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya amani na maendeleo na inatoa wito kwa Wadau wote kuruhusu mifumo ya kitaifa kutekeleza hatua na maamuzi yaliyowekwa na Serikali.

Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapenda kuihakikishia jumuiya ya kimataifa na Wadau wa maendeleo kuhusu utayari na dhamira yake ya kuendelea kushirikiana katika masuala yote ya maslahi ya pande zote kama Washirika wenzao. 


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages