Mkurugenzi wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema awali upimaji huo ulikuwa umepangwa kufanyika kwa siku moja katika Hospitali ya Dar Group lakini kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza, taasisi imeamua kuongeza muda ili kuhakikisha watu wengi zaidi wanapata nafasi ya kupimwa.
“Tumeona mwamko mkubwa wa wananchi. Kwa siku leo tumewahudumia watu 232. Ili kutimiza dhamira ya kuelimisha na kuzuia magonjwa ya moyo, tumeongeza siku mbili ili wananchi wengi zaidi wapate huduma hizi muhimu”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alibainisha kuwa takwimu zinaonyesha watoto 10,000 huzaliwa nchini wakiwa na matatizo ya moyo kila mwaka, ambapo zaidi ya 4,000 huhitaji upasuaji wa haraka. Kwa watu wazima changamoto kubwa zinatokana na ulaji usiozingatia lishe bora, kutokufanya mazoezi, uvutaji sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi na magonjwa nyemelezi kama kisukari na shinikizo la damu.
Dkt. Kisenge alisema JKCI inaendelea na kampeni yake ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi ijulikanayo kwa jina la Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services ambayo tayari imeshafika katika mikoa 23 na kuwafikia zaidi ya watu 23,000 kwa kutoa elimu na huduma za upimaji na matibabu ya moyo.
Dkt. Kisenge aliwataka Watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha, ikiwemo kufanya mazoezi, kula vyakula vyenye lishe bora na kupima afya mara kwa mara ili kulinda afya ya moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa JKCI-Dar Group Dkt. Tulizo Shemu alisema gharama za matibabu ya moyo ni kubwa, hivyo wananchi wanapaswa kujikinga mapema kwa kufanya vipimo vya afya mara kwa mara ili kama watakutwa na matatizo ya moyo waanze matibabu mapema kabla ya changamoto hazijawa kubwa.
“Kuzibua mshipa wa moyo hugharimu zaidi ya Sh milioni 6, na kifaa cha kusaidia umeme wa moyo kinaweza kugharimu hadi Sh milioni 10. Njia rahisi na nafuu zaidi ni kuzuia ugonjwa kabla haujawa mkubwa”, alisema Dkt. Shemu.
Naye Daktari Bingwa wa Moyo kwa Watoto wa JKCI-Dar Group Eva Kuganda alisema katika kambi hiyo wanafanya upimaji kwa watoto na kuwaomba wazazi wenye watoto wawapeleke kupima afya zao.
“Katika upimaji wa watoto umeonyesha baadhi yao wana matatizo ya moyo bila kuwa na dalili zozote. Hii inaonyesha umuhimu wa vipimo mapema ili matatizo yashughulikiwe kabla hayajawa makubwa”, alisema Dkt. Eva.
Kwa upande wa wananchi waliojitokeza kupima afya za mioyo yao, wengi walieleza kuridhika na huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kuelewa hali ya afya zao pia elimu waliyopewa ya matumizi sahihi ya dawa, jinsi ya kuutunza moyo na lishe bora wataitumia katika maisha yao ya kila siku.
“Kwa sisi wananchi ambao hatuwezi kumudu gharama za upimaji, JKCI imeturahisishia sana. Tungeomba serikali iendelee kuipa nguvu taasisi hii ili iweze kutoa elimu na matibabu kwa wananchi wasiojiweza,” alisema Kassim Likaukwa, mkazi wa Temeke.
“Nilikuwa nikitembea kidogo moyo wangu unaenda kasi, lakini baada ya upimaji na maelezo niliyopata hapa, nimeweza kuelewa hali yangu na kuanza kuchukua tahadhari za kiafya”, alisema Grace Shirima mkazi wa Tegeta.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Usipuuze Mapigo ya Moyo: Zingatia kinga, uchunguzi wa mapema na maisha yenye afya”.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇