Mar 17, 2025

WATANZANIA, WADAU WA ELIMU TUIUNGE MKONO TET KUFANIKISHA 'KITABU KIMOJA, MWANAFUNZI MMOJA'

Na Bashir Nkoromo, Blog ya Taifa ya CCM
Mapema tu baada ya uhuru mwaka 1961, Rais wa kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza maadui watatu wakubwa wa taifa kuwa ni ujinga, umasikini na maradhi.

Kupambana na maadui hao aliweka msisitizo mkubwa katika elimu kwa watoto na watu wazima, akinuia wajue angalau kusoma, kuandika na kuhesabu, na kwa kiasi chake kwa mazingira ya wakati huo alifanikwa.

Mwalimu pia alitaja katika baadhi ya maandiko yake vitu vinavyohitajika ili nchi iendelee, kuwa ni pamoja na Watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Baada ya Mwalimu Nyerere, kuona kuwa maadui wakubwa wa taifa ni ujinga, umasikini na maradhi, alianisha njia ya kuwaondoa kuwa ni taifa kuwa na watu walioelimika, ndiyo sababu akaweka msisitizo mkubwa katika elimu kwa watoto na watu wazima.

Mwalimu Nyerere alikuwa sahihi, maana hata alipoandika kuwa ili nchi iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, alijua kuwa hayo hayawezekani bila elimu, maana hata nchi iwe na watu lakini wasioelimika hawataleta maendeleo, hata ardhi iwepo yakutosha kama hakuna wananchi wenye elimu ya kuiendeleza haitaleta maendeleo, na hata siasa safi na uongozi bora haviwezekani kama nchi ina wanasiasa na viongozi mbumbumbu!

Ukweli ni kwamba maono hayo yaliyosemwa na kuandikwa na Mwalimu Nyerere baada ya nchi kupata uhuru zaidi ya miaka 60 iliyopita, bado ni ya muhimu na yanahitajika zaidi wakati huu kuliko wakati ule ambao nchi ilikuwa bado ina watu wachache na mahitaji ya matumizi ya sayansi na teknolojia hayakuwa makubwa kama sasa.

Kwa kutambua na kwa kuzienzi falsafa za Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Serikali za Awamu zote hususan ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, zimekuwa zikipambana kujenga misingi bora kuhakikisha utoaji elimu nchini unaimarika na kuwa endelevu ili kwenda mbali zaidi ya lengo lile la walau watu wajue kusoma, kuandika na kuhesabu, sasa iwe elimu bora badala ya bora elimu.

Yapo mambo mengi ambayo serikali imefanya na inaendelea kufanya katika kutanua wingo wa utoaji elimu ikiwemo kutoa elimu bila ada na kuongeza au kuboresha miundombinu ya kusoma na kujisomea, lakini bado changamoto zipo zikiwemo uchache wa vitabu kwa wanafunzi, changamoto ambayo nayo serikali inapambana nayo kuhakikisha inafutika.

Katika kupambana na changamoto hiyo, Serikali imeipa jukumu taasisi yake ya Elimu (Taasisi ya Elimu Tanzania - TET) pamoja na mambo mengine kuivalia njuga changamoto hiyo ya uchache wa vitabu kwa wananfunzi na kuhakikisha inafikia wakati kila mwanafunzi kuanzia shuleni ya Awali, Msingi na Sekondari anakuwa na kila kitabu kinachohitajika.

TET chini ya Mkurugenzi wake Mkuu Dk. Aneth Komba, kwa kutambua wajibu wake, inaonekana imeshalipokea jukumu hilo na tayari imeshaanza kulifanyia kazi tena siyo kwa maneno bali kwa vitendo.

Kwa kujua kuwa jukumu hilo la vitabu ni muhimu, Mwaka huu TET katika kuadhimisha miaka 50 ya uwepo wake, suala la vitabu imelipa kipaumbele na kulifanya ndiyo agenda kuu ya kubeba maadhimisho hayo kwa kuyapa kaulimbiu ya 'Kitabu kimoja, Mwanafunzi mmoja'.

Katika Maadhimisho hayo ambayo TET iliyaanza mapema mwezi huu (Machi), iliandaa Matembezi ya Hisani ambayo iliyapa Kaliumbiu hiyo ya 'Kitabu Kimoja, Mwanafunzi mmoja' ambayo yalifanyika Machi 7, mwaka huu (2025), yakiongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, yalianzia Ofisi za TET Mikocheni jijini Dar es Salaam, na kwenda Millenium Tower na baada ya mzunguko mrefu yakarejea Ofisi hizo za TET ambako yaliishia.

Mwishoni mwa matembezi hayo, Waziri Mkuu alitoa maelekezo na nasaha nyingi chanya zitakazowezesha TET kuchapisha vitabu vingi kwa gharama nafuu, lakini akapongeza kaulimbiu ya maadhimisho hayo
'Kitabu Kimoja, Mwanafunzi mmoja', akisema inawiana na malengo ya kitaifa ya kuhakikisha kuwa watoto wa Tanzania wanapata elimu bora.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba alimwambia Waziri Mkuu kwamba taasisi hiyo imedhamiria kuhakikisha vinapatikana vitabu vya kutosha ili kila mwanafunzi kuanzia shule za Awali, Msingi na Sekondari anakuwa na kitabu na kuondoa kabisa hali ya sasa ya watoto kushea au kunyang'anyana vitabu madarasani.

Alisema kutokana na dhamira hiyo ambayo ndiyo ya Serikali, TET imeamua maadhimisho ya miaka yake 50 kuyafanya sanjari na kampeni ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuchapisha vitabu na kununua kopyuta kwa ajili ya kuhifadhi vitabu.

Dk. Aneth akasema, Kampeni hiyo inalenga kukusanya fedha Sh. Sh. bilioni 297 kwa ajili hiyo ya kuchapisha vitabu na kununua kompyuta za kuhifadhi vitabu, na kwamba ili kutoa nafasi kwa Watanzania hususan wadau wa elimu wengi kuchangia, Maadhimisho na kampeni hiyo ya
'Kitabu Kimoja, Mwanafunzi mmoja yanatarajiwa kuhitimishwa Juni mwaka huu.

Hapo Dk. Aneth anamaanisha kuwa kwa takribani miezi minne (4), kampeni ya kukusanya fedha (Sh. Sh. bilioni 297) sanjari na maadhimisho ya miaka 50 ya TET, milango itakuwa wazi kwa ajili ya kutoa nafasi kwa kila Mtanzania anayethamini elimu bora, kujitokeza kuchangia ili kiasi hicho cha fedha kiweze kupatikana ili vitabu vichapishwe na kompyuta za kuhifadhi vitabu zinunuliwe.

Bila shaka TET imeamua kuchangisha fedha kwa sababu inatambua kuwa jambo kubwa kama hilo la kuhakikisha 
'Kitabu Kimoja, Mwanafunzi mmoja' , lina uhitaji wa kuchangiwa na Wananchi badala ya kusubiri serikali peke yake kulikamilisha kwa muda unaohitajika, kwa sababu, mbali ya elimu kuna sekta nyingine ambazo nazo zinahitaji fedha kutoka serikalini ili ziweze kutoa huduma bora.

Inafahamika kuwa Watanzania wengi tu wepesi kutoa michango mbalimbali, lakini isivyo bahati wengi wetu ni wepesi zaidi kuchangia shughuli za kijamii kama harusi, lakini wazito kuchangia shughuli za Jamii kama elimu na masuala ya afya, kwa hiyo sasa ni vema Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake akajitolea kuchangia kampeni hii ya 'Kitabu kimoja, Mwanafunzi mmoja'.

Uzuri wa kuchangia kampeni hii ni kwamba, siyo tu utakuwa umechangia taifa, bali utakuwa umejichangia hata wewe kwa maana ya mwanao, mjukuu au kitukuu, maana kampeni hii ikifanikiwa ni mwanao, mjukuu au kitukuu chako atakayepata fursa ya kusoma kitabu kimoja badala ya kunyang'anyana kitabu na wanafunzi wenzake darasani.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakiwa wameshika bango la kampeni maalum ya 'Kitabu Kimoja, Mwanafunzi mmoja' yenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuchapa na kusambaza vitabu vya kiada kufikia uwiano wa kitabu kimoja, mwanafunzi mmoja, Mikocheni Jijini Dar es Salaam , Machi 07, 2025.Kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga,  na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba, Mwenyekiti wa Baraza la TET Prof. Maulid Mwatawala.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages