LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 23, 2024

RC ANDENGENYE AFANYA ZIARA YA KUKAGUA UJENZI WA MIRADI MBALIMBALI KIGOMA

 Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya nyongeza kutoka mradi Mkuu wa Barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa Km. 260 kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili kuendana na malengo ya serikali katika kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi.


Andengenye amesema hayo akiwa wilayani Buhigwe kwenye ziara yake ya kukagua miradi hiyo inayotekelezwa kwa Thamani ya Shilingi Bil. 20 katika wilaya za Buhigwe, Kasulu na Kibondo ambapo miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Masoko, Stendi, Miundombinu ya Maji, Elimu na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za Afya.


Amesema wakandarasi hao wanapaswa kuzingatia makubaliano yao na serikali ili kuhakikisha miradi hiyo ya nyongeza inakamilika sambamba na ujenzi wa barabara ya Kabingo, Kasulu hadi Manyovu.


Upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma Mha. Narcis Choma amesema kupitia utaratibu huo, katika wilaya ya Buhigwe inatekelezwa Miradi ya ujenzi wa Soko la Mnanila, stendi ya mabasi Buhigwe, matanki ya kuhifadhi Maji katika vijiji vya Bweranka na Kibwigwa pamoja na ujenzi wa Shule ya Sekondari Kidato cha Tano na Sita Buhigwe.


Mha. Choma amesema miradi hiyo itakapokamilika wananchi wataona thamani ya ziada ya utekelezaji wa miradi ya barabara katika maeneo yao ikiwemo ujenzi na maboresho ya miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma za jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye akikagua miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa Thamani ya Shilingi Bil. 20 katika wilaya za Buhigwe, Kasulu na Kibondo ambapo miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Masoko, Stendi, Miundombinu ya Maji, Elimu na uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za Afya.













No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages