Na Bashir Nkoromo, CCM Official Blog
Kufuatia Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020/2025, kuelekeza Serikali kuimarisha Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kuongeza bajeti ili kukidhi mahitaji ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara za mijini na vijijini, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Wakala hiyo imepata mafanikio makubwa.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seif, akieleza utendaji na mafanikio ya Wakala hiyo ndani ya miaka mitatu, katika Kikao Kazi baina yake na Wahariri na Wandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali, kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, leo Septemba 2, 2024.
Mhandisi Seif amesema kufuatia kuitika maelekezo ya Ilani ya CCM, Serikali imeongeza bajeti ya Ujenzi na Matengenezo ya barabara zaidi ya mara tatu kutoka wastani wa Sh. Bilioni 275 miaka minne iliyopita hadi kufikia Sh. Bilioni 850 kuanzia mwaka 2021/22.
Amesema, wakati Ilani hiyo iliagiza Serikali kuongeza mtandao wa barabara unaohudumiwa na TARURA kutoka kilometa 108,946 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwezesha maeneo mengi ya Vijijini kufikika kwa urahisi, Mtandao wa barabara za wilaya umeongezeka kutoka kilometa 108,946 hadi kufikia kilometa 122,429.77 na umetangazwa rasmi kwenye gazeti la Serikali Na 563 la Juni 25, 2021.
Mhandisi Seif amesema, pia ilani iliagiza kuongezwa kiwango cha barabara za changarawe kutoka kilometa 24,494 hadi kufikia kilometa 35,000 ifikapo 2025 na kwamba katika kutekeleza agizo hilo, hadi Juni 2024 mtandao wa Barabara za Wilaya za changarawe umefikia kilometa 42,059.17.
Akiendelea kueleza, Mhandisi Seif amesema, katika agizo la Ilani ya CCM kuelekeza kuongezwa urefu wa barabara za mijini na vijijini zilizojengwa kwa kiwango cha lami kutoka kilometa 2,025 hadi kufikia kilometa 3,100 ifikapo mwaka 2025, hadi kufikia Juni 2024 mtandao wa barabara za wilaya za lami umefikia kilometa 3,337.66.
Mhandisi Seif amesema vilevile agizo lingine kwa Serikali kuweka utaratibu utakaozitaka Halmashauri kutenga fedha kutoka katika mapato ya ndani kwa ajili ya kazi za ujenzi wa miundombinu ya barabara za vijijini na mijini, nalo limekelezwa kwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI kuagiza Halmashauri zote zenye mapato zaidi ya Sh. Bilioni 5 kutenga asilimia 10 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya Barabara za wilaya katika Halmashauri zao.
Aidha kuhusu Ilani ya CCM kuelekeza kufanyika tafiti za matumizi ya teknolojia sahihi katika ujenzi wa barabara za mijini na vijijini ili kujenga barabara kwa teknolojia sahihi na gharama nafuu, Mhandisi Seif amesema, sasa TARURA inatumia malighafi za ujenzi miundombinu ya barabara zinazopatikana maeneo ya kazi kama mawe ambapo gharama zinapungua kwa zaidi ya asilimia 50 na kueleza kuwa jumla ya madaraja 275 na kilometa 22.5 za barabara zimejengwa kwa kutumia mawe yanayopatikana maeneo ya kazi.
Alisema, pia TARURA inaendelea kufanya majaribio ya teknolojia mbalimbali ili kutumia udongo uliopo eneo la kazi badala ya kusomba kutoka mbali lakini pia kutunza mazingira.
Alisema, teknolojia hizo ni pamoja na ECOROADS, Ecozyme na GeoPtymer, na hadi sasa kwa kutumia Teknolojia hiyo ya ECOROADS katika Jiji la Dodoma imejengwa kilometa moja ya barabara na wilaya ya Chamwino zimejengwa kilometa 6.95 ambazo zote zimekamilika huku katika wilaya ya Mufindi zikiwa zinajengwa kilometa 10, na Rifiji kilometa 32.
Pia alisema, kwa kutumia Teknolojia ya Ecozyme, katika wilaya ya Itilima zinajengwa Kilometa 5.2 na mkandarasi yupo eneo la kazi na anaendelea na utekelezaji.
Akizungumzia Ujenzi wa Daraja na Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, Mhandisi Seif amedokeza kuwa kuna takriban Kaya 314 ambazo zimetambuliwa kuwa zitaathirika na Ujenzi wa Daraja na Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi ambapo mchakato wa kuandaa daftari la fidia utaanza mwezi huu wa tisa.
Amesema, lengo la mradi ni kukabiliana na mafuriko katika Bonde la mto Msimbazi ambapo eneo la chini la Mto Msimbazi linatarajiwa kuongezewa kina na kupanuliwa ili kuruhusu maji kwenda baharini kwa kasi inayotakiwa.
“Mradi huu umeanza rasmi tarehe 16 Februari 2023 ambapo utatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia (Dola za Marekani milioni 200), Serikali ya Hispania (Euro milioni 30), na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi (Euro milioni 30).”Amefafanua Mhandisi Seif na kwamba hadi sasa asilimia 98 ya watu ambao wanaathirika na mafuriko wamelipwa fidia na wameondoka.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza TARURA kwa jinsi ilivyoendesha uhamishaji wananchi waliokuwa wakiishi kwenye maeneo ya bonde la Mto Msimbazi, akisema pongezi hizo amezitoa kwa sababu hadi sasa hakuna mwananchi walioandamana au kulalamika. " inaonekana malipo waliyopewa hayakuleta malalamiko, yalikuwa manono.” akasema Balile.
Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seif, akieleza utendaji na mafanikio ya Wakala hiyo ndani ya miaka mitatu, katika Kikao Kazi baina yake na Wahariri na Wandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali, kilichofanyika Jijini Dar es Salaam, kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, leo Septemba 2, 2024. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina Sabato Kosuri.Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seif, akienedela kueleza utendaji na mafanikio ya Wakala hiyo.
Baadhi ya Washiriki wa Kikao Kazi hicho.
Baadhi ya Washiriki wa Kikao Kazi hicho.Baadhi ya Washiriki wa Kikao Kazi hicho.Kosuri akitoa nafasi kwa washiriki kuuliza maswali au kutoa ushauri.
Baadhi ya Washiriki wakiomba kuuliza maswali.
Mhandishi Seif akijibu maswali.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile akitoa neno la shukurani.
Kaimu Meneja Uhusiano TARURA Catherine Sungura, akizungumza.Mhandishi Seif akikamilisha mazungumzo mwishoni kikaokazi hicho.
Kosuri akifunga kikaokazi hicho.
WASILISHO KAMILI LA TARURA👇
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇