LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 23, 2024

RC ANDENGENYE AIPONGEZA SERIKALI KWA MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA KILIMO










 Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Kilimo kwa kuendelea kufanya Mapinduzi makubwa kwenye Sekta hiyo kwa lengo la kuwawezesha wakulima kufanya Kilimo chenye tija. 


Mhe. Andengenye ametoa kauli hiyo alipozungumza kwenye hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Maafisa Ugani Kilimo Mkoa wa Kigoma na kusisitiza nyenzo hizo kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Serikali.


Amesema sekta hiyo ni muhimu kwa ustawi wa jamii mkoani humo kutokana na zaidi ya Asilimia 70 ya wakazi kutegemea Kilimo kama chanzo kikuu cha Uchumi kwa ajili ya kuwawezesha kuendesha maisha yao ya kila siku.


Kupitia hafla hiyo Mkuu wa Mkoa amegawa magari mawili yaliyotolewa na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe ili kufanya usimamizi wa shughuli za kilimo sambamba na kugawa mavazi maalum kwa maafisa Ugani Kilimo 179 wanaotekeleza majukumu yao mkoani humo.


Aidha Andengenye amezikumbusha Halmashauri kutekeleza maagizo ya Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe ikiwemo Halmashauri ya Kigoma Ujiji kutenga eneo ili Wizara ya Kilimo iweze kutekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kuratibu shughuli za umwagiliaji nchini.


Sambamba na agizo hilo, Mhe Andengenye ameitaka halmashauri ya wilaya Kibondo kutekeleza agizo la kutenga Eneo ili serikali iweze kufanya ujenzi wa Soko la kisasa la zao la Muhogo huku halmashauri ya Buhigwe ikitakiwa kuandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata zao la Tangawizi.


Aidha Mhe. Andengenye amezielekeza halmashauri zote mkoani humo kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa masoko ya kimkakati kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kuyafikia masoko hayo na kufanya biashara za mazao yao kwa tija.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages