Na HEMEDI MUNGA, Igunga
WANANCHI wilayani Igunga mkoani Tabora, wametakiwa kutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika pindi wanapoona haki zao zinavunjwa au zinaelekea kuvunjwa na sio kujichukulia sheria mkononi.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo wale wa dini, wakuu wa Taasisi, Idara, vitengo, waheshimiwa Madiwani, watendaji wa kata na vijiji katika ukumbi wa Maxwell wilayani hapa, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Mohamed Khamis Hamad ametoa elimu kuhusu majukumu ya tume hiyo.
Aidha, amesema moja ya haki za binadamu ni maswala ya maendeleo ambapo kila mmoja anahitaji huduma za kijamii ikiwemo umeme, maji, chakula na nyinginezo.
Amesema kuundwa kwa tume hiyo ambayo inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kielelezo kuwa serikali inazingatia vizuri mambo ya haki za binadamu nchini.
Hata hivyo, Hamad ameweka wazi kuwa Tume hiyo, inawajibu wa kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu na wajibu kwa jamii kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi.
Aidha, ametaja baadhi ya wajibu mwingine kuwa ni kupokea malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na kufanya uchunguzi mbalimbali kuhusu haki za binadamu na utawala bora.
" Malalamiko ambayo mtu au mwananchi yoyote anaona kunauvunjifu wa haki za binadamu anaweza kuwasilisha katika tume hiyo," amesisitiza.
Mbali na majukumu hayo, ameongeza kuwa tume hiyo inajukumu la kutoa na kueneza elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na utawala bora ikiwemo kumchunguza kiongozi yoyote aliyeshikilia ofisi ikidaiwa kuwepo tuhuma za uvunjaji wa haki hizo.
Akizungumzia kuhusu haki hizo, Hamad ameweka wazi kuwa ni zile haki za msingi ambazo binadamu anahitaji kuzipata kwa sababu tu yeye ni binadamu.
"Ndugu zangu viongozi tufahamu kuwa kwa kuzaliwa mwanadamu kunamambo ya msingi anastahiki kuyapata kwa sababu ni stahiki zake," amebainisha.
Amefafanua kuwa binadamu yoyote anahitaji kuishi, kula chakula kizuri, kupata maji safi na salama na kukaa katika mazingira safi haki ambazo hazihitaji kupewa na sheria wala katiba ambapo binadamu anakuwa nazo kwa sababu yeye ni binadamu.
Ameeleza Jumuiya za Kimataifa zikaziwekea mikataba anuai na maazimio kwa kuziorodhesha haki hizo ikiwemo kuziwekea mifumo ya kuzisimamia.
"Sisi hapa kwetu Tanzania kwa sababu ni waumini wa haki za binadamu tukaziweka kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kuziwekea mazingira na mifumo ya kuzisimamia," amedokeza.
Amebainisha kuwa katiba ya Tanzania ibara ya 12 inaeleza kwamba binadamu wote wamezaliwa huru na wote ni sawa, binadamu wote ni sawa mbele ya sheria na kutoa haki ya kuishi.
Aidha, ameongeza kuwa katiba hiyo inatoa haki ya kuwa huru, haki ya faragha, mtu anaweza kwenda anakotaka, uhuru wa kutoa maoni kwa mujibu wa sheria, kuamini dini anayotaka, uhuru wa kushirikiana na mtu mwingine, haki ya kufanya kazi na uhuru wa kushiriki shughuli za umma.
Amesema viongozi wanao wajibu wa kuwahimiza wananchi kushiriki katika uchaguzi kwa sababu ni haki na nimaendeleo yao kwa kuwa watapata viongozi watakaosaidia kupanga mipango anuai ya kuleta maendeleo.
Hata hivyo, Hamad ametahadharisha kuwa haki hizo zinazo wajibu wake ikiwemo wajibu wa kushiriki kazi kwa mtu aliyepata kazi, wajibu wakutii sheria, wajibu wa kulinda mali za umma na wajibu wa ulinzi wa Taifa.
Pia, Hamad ameeleza kuhusu Utawala bora kuwa ni matumizi ya mamlaka kisiasa, kiuchumi au vinginevyo katika kusimamia rasilimali za Taifa kwa kufuata misingi ya uwazi, uwajibikaji, ushirikishwaji, haki za binadamu na utawala wa sheria.
Amebainisha ushirikishwaji, maridhiano, mwitikio, matokeo bora ya ufanisi, uwajibikaji, uwazi, usawa, utawala wa sheria, maono ya kimkakati na uadilifu ni viashiria vinavyoonesha nchini kunautawala bora.
"Sisi viongozi tujitathimini kwa kiasi gani katika jamii zetu kwa kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, kata na kuendelea tunazingatia misingi ya utawala bora," ametoa rai.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇