Na Bashir Nkoromo, CCM Blog.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam, Saad Mtambule, amezima kwa burasa kubwa mgogoro uliokuwa umepamba moto baina ya Wananchi wa Mtaa wa Mbezi Beach 'A' Kawe na Mkandarasi aliyepewa vibali vya kuchimba mchanga mtoni huku wananchi hao wakiwa hawakushirikishwa mwanzoni mwa mchakato.
DC Mtambule amefanikiwa kuzima mgogoro huo leo Agosti 14, 2024, baada ya kutembele eneo la Mbezi darajani ambalo Mkandarasi huyo, Kampuni ya MEG Business Solution Ltd, amepewa vibali vya kuchimba mchanga, lakini wananchi wakazuia uchimbaji wakilalamika hawakushirikishwa katika hatua za mwanzo wa mchakato wa kufanyika uchimbaji huo.
Wananchi walizunia uchimbaji huo wiki iliyopitaa baada ya kuona kwa kustukizwa tingatinga likiwa mtoni kuandaa miundombinu ya kuchimba mchanga ikiwemo barabara ya muda iliyotemgenezwa kupitia eneo la JWTZ Lugalo hadi mtoni. Kwa mujibu wa vibali uchimbaji ungeanza Agosti 2, 2024,
Hoja ya wananchi kupinga uchimbaji huo, mbali na kulalamikia kutoshirikishwa walisema wanahofia ungeathiri kingo za mto hivyo kusababisha mafuriko nyakati za mvua ambayo wanahofu yataweza kuwa makubwa zaidi kuliko yaliyowafika wakati wa mvua zilizopita.
DC Mtambule akiwa na maafisa mbalimbali wakiwemo wa TANROADS, NEMC, Idara ya Mazingira Manispaa ya Kinondoni na Mamlaka ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, pamoja na mambo mengine alitaka kujua kutoka kwa wananchi kwa nini wanazuia uchimbaji huo.
Kwa nyakati tofauti, wananchi walimueleza DC, hawapingi kufanyika uchimbaji mchanga, lakini hawaafiki uchimbaji huo kufanyika kwa kuwa hawakuhsirikishwa kwenye mchakato katika hatua za mwanzo kama inayopaswa kufanyika wakati inapofanyika miradi inayowagusa wananchi.
Walisema, hatua ya kutoshirikishwa katika hatua za awali kunawafanya wajawe na shaka kwamba uchimbaji mchanga mtoni utafanywa bila kuzingatia hatma ya mazingira ya eneo lao na makazi yao hasa kuhusu mafuriko.
Baada ya DC Mtambule kuwasikiliza wananchi kwa makini alitoa nafasi pia kwa viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa mtaa huo wa Mbeazi Beach A, ambaye katika maelezo yake alithibitisha kwamba wananchi hawakushirikishwa.
Watendaji nao kutoka taasisi mbalimbali waliofuatana na DC nao walipata nafasi ya kuzungumzia utekelezaji wa mradi huo, baadhi yao wakasisitiza kwamba utazingatia hali zote ili kutoathiri mazingira na makazi ya wananchi.
Baada ya kusikiliza pande zote kwa takriban saa 2, DC Mtambule, akasema, amebaini kwamba changamoto iliyopo kubwa ni wananchi hao kutoshirikishwa, hivyo akaamuru mkandarasi kusimamisha kazi na kuondoa vifaa vyote mtoni ikiwemo tingatinga ili kuruhsu mchakato uanze upya.
"Sasa pamoja na maelezo mazuri na lengo zuri la mradi huu, nimeona kuwa hapa mgogoro umetokana na wananchi kutoshirikishwa wakati mchakato ukianadaliwa, hivyo kuanzia sasa Mkandarasi simamisha kuendelea na shughuli yoyote hapa mtoni, na mchakato urudi kuanzia kwa wananchi.
Kama mnavyoona mvua hazipo mbali kuanza kunyesha, hakikisheni mnafanya haraka katika michakato hii na wananchi, ili maafikiano yakikamilika muanze kabla mvua hazijaanza". akasema DC Mtambule.
Eneo ambalo uchimbaji huo wa mchanga unatakiwa kufaywa na Mkanarasi katika mto Mbezi, ni la kuanzia lilipo daraja la Kawe darajani, mtaa wa Mbezi Beach A, Darajani, barabara kuu kutoka Mwenge - Tegeta hadi Bagamoyo na inaelezwa mchanga huo ni kwa ajili ya kumuuzia mkandarasi wa ujenzi wa Barabara mabasi ya Mwendokasi, Mwenge-Tegeta.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule akipokea vibali kutoka kwa Emmanuel Lyimo wa Kampuni ya MEG Business Solution Ltd, baada ya kuhitaji kuviona kama kweli vipo.
DC Mtambule akisoma kwa makini moja ya vibali hivyo. DC Mtambule akitoa maelekezo ya kusimama uchotaji mchanga hadi mcakato utakapoanzia kwa Wananchi.
DC Mtambule akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkandarasi.DC Mtambule akikagua eneo utakakoanzia uchimbaji mchanga ikiwa wananchi wataafiki.
Mwananchi akizungumza hoja zake mbele ya DC Mtambule.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbezi Beach A akizungumza Mbele ya DC Mtambule aliyetaka aelezwe kwa nini Wananchi hawakushirikishwa katika hatua za awali.
Mkazi wa Mtaa wa Darajani akieleza alivyoathiriwa na mafuriko yaliyopita.
Mwenyekiti shina namba 8 akiekeza wanachotaka wananchi kifanyike kabla ya uchimbaji mchanga kuganyika.
Mkazi wa Mbezi Darajani, akimshukuru DC kwa hatua aliyofanya kufika kusikiliza wananchi na kuutatua mgogoro.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇