LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 20, 2024

WAZIRI SIMBACHAWENE AKERWA WANAOLIMA MILIMA YA KIBAKWE, AHOFIA VYANZO VYA MAJI KUWA HATARINI KUTOWEKA

Na Isungu Helela, Kibakwe
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene amekerwa na wananchi wanaoendesha shughuli za kilimo katika milima ya Kibakwe huku akihofia kama hatua za haraka hazitachukuliwa vyanzo vya maji vitakuwa hatarini kutoweka.

Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo akizungumza na wananchi kwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Lutarawe, Njiapanda na Kikuyu, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, leo.

Amesema
vyanzo hivyo vya maji ni tegemeo pekee la wakazi wa Jimbo hilo na kwamba maji yanayotoka katika milima hiyo yana manufaa makubwa kwa watu wote ilhali mazao yanayolimwa katika milima hiyo ni kwa ajili ya manufaa watu wachache.

Amesema vyanzo hivyo vya maji ndio vyanzo pekee vinavyotegemewa lakini kasi ya ukataji miti inazidi kushamiri juu ya milima hiyo kwa ajili ya kilimo, hali inayotishia maisha ya watu wote kwa ajili ya maslahi ya watu wachache.

Kufuatia hatua hiyo Mhe. Simbachawene amewataka Madiwani kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji kuzungumza na wanaolima juu ya  milima hiyo na kama hawatawaelewa basi sheria kali zichukuliwe dhidi yao kwani wanahatarisha uhai wa wananchi wa Kibakwe na taifa kwa ujumla.

"Milima mingi imebaki vipara miti mingi imekatwa kwa ajili ya kilimo hali inayochangia wakati wa mvua maji kushuka kwa kasi kutoka milimani na kusababisha uhalibifu wa miundombinu ya barabara, hii sio sawa kabisa, nawaagiza viongozi chukueni hatua za haraka kwani mnawajua kwa majina wanaoyafanya hayo" amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Kutokana na uharibifu huo, Mhe.Simbachawene amesema tatizo la maji katika jimbo hilo halitaisha hata kama Serikali itatoa fedha kwa vile vyanzo vya maji vinazidi kuharibiwa.

Mhe. Simbachawene amesema juhudi anazozifanya za kuwaletea miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule, barabara pamoja na umeme itakuwa haina maana kama vyanzo hivyo vitatoweka kwani maji ni uhai.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ipera, Mhe. Festo Muyuguye amesema Waziri Simbachawene analitendea haki Jimbo la Kibakwe hususani Kata ya Ipera katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo umeme, ujenzi Kituo cha Afya, gari la kubebea wagonjwa pamoja ujenzi wa shule za Sekondari.

Hivyo Mhe. Muyuguye ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Kata ya Ipera wasikubali kuyumbishwa na yeyote bali wawalinde Viongozi wao kwa nguvu zote.
 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza leo na wananchi wa Kijiji cha Lutarawe, Kata ya Ipera, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi.
Baadhi ya  wananchi na viongozi wa Kijiji cha Lutarawe, Kata ya Ipera, Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma wakiwa wameongozana na  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, wakati wa ziara yake ya kikazi. 
Meneja wa TARURA wa wilaya ya Mpwapwa Mhandisi Emmanuel Lukumay akisalimiana na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kikuyu mara baada ya kuwasili, ikiwa ni ziara  ya kikazi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages