Na HEMEDI MUNGA, Iramba
VIJANA wamekumbushwa wajibu wao wa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ambae amewaumba hususan katika kipindi hichi ambacho wanazo nguvu za kufanya mengi ikiwemo ibada.
Aidha, wametakiwa kula rizki za halali ambazo Mungu amewajalia na kutenda matendo mema ya kumpendeza Mungu kwa sababu kufanya hivyo itakua sababu ya wao kwenda peponi.
Wito huo, ameutoa Shekhe wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Hassan Dahir alipokua akiongea na waumini wa Kata ya Shelui, wilayani Iramba mkoani Singida katika walima wa harusi.
Amesema mwanadamu ameheshimishwa sana na Mwenyezi Mungu kuliko viumbe wengine wote.
"Sisi binadamu tumetukuzwa na mfumo wetu ni ibada, hivyo tuzidi kumuogopa Mwenyezi Mungu," ameomba.
Akizungumzia kuhusu ndoa, Shekhe Dahir ameeleza lengo la ibada hiyo, ni kuendeleza kizazi kwa kuwa zipo sababu mbalimbali zinazowachukuwa wanadamu ikiwemo mauti kutokana na magonjwa, vita na ajali.
Pia, ameonesha mshangao dhidi ya wale wanaodaiwa kuwakataza watu kuzaa sana licha ya kuwepo kwa sababu hizo.
"Vinavyotuchukua vipo vingi, hivyo lazima tuzaliane kwa lengo la kuendeleza kizazi na udugu," amesisitiza.
Hata hivyo, amewataka wanaume kuendelea kutulia kwa lengo la kuchunga familia zao ikiwemo uchumi wao kwa kuepukana na kila aina ya koloni.
Ameweka wazi tabia ya kutumia ujana na kumzalisha mtu zaidi ya mmoja au sita bila utaratibu wa ndoa, hiyo ni fujo na haikubaliki katika jamii.
Pia, amewataka wazazi kuacha tabia ya ubaguzi wa kiuchumi hususan vijana wanapokua wamependana na kutaka kuoana.
"Wale ambao hamjaoa msitake kujipanga sana, oweni kwa sababu kutofanya hivyo mtajikuta katika kuongeza watoto wa mitaani," amesema.
Ameongeza tabia hiyo imekua ikileta shida ya upangaji wa bajeti sio tu kwa mtu mmoja moja hata kwa serikali kwa kuto fuata utaratibu wa kisayansi aliouelekeza muumba.
Mbali na hayo, amewapongeza waumini wa dini hiyo kwa kuvaa mavazi ya heshima kwa sababu wanaisalimisha na kuifundisha dunia maadili mema huku akionya na kulaani wale wanaotumia mavazi hayo kufanyia uchafu.
Shekhe wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Hassan Dahir akiwataka vijana kumcha Mwenyezi Mungu, wakati wa hafla fupi ya walima wa harusi iliyofanyika katika kata ya Shelui wilayani Iramba mkoani Singida. (Picha na Hemedi Munga)
Shekhe Ponda Rukumbwe wa Msikiti wa Taqwa mjini Kiomboi akiteta jambo na Shekhe Abdi Kilita wa Shelui, wakati wa hafla fupi ya walima wa harusi iliyofanyika katika kata ya Shelui wilayani Iramba mkoani Singida, Kulia ni Shekhe wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Hassan Dahir. (Picha na Hemedi Munga)
Baadhi ya Viongozi wa dini wakiwa katika walima wa harusi katika kata ya Shelui wilayani Iramba mkoani Singida. (Picha na Hemedi Munga)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇