LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 22, 2024

UBORESHAJI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA WASOGEZWA, SASA KUANZA JULAI 20, 2024 KIGOMA

Na Mwandishi Maalum, Kigoma.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza kusogezwa mbele shughuli ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura hadi Julai 20, 2024 badala ya Julai Mosi, 2024 iliyokuwa imepangwa awali.


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele amesema leo mkoani Kigoma, kwamba uzinduzi utafanyika siku ya Jumamosi, Julai 20, 2024 mkoani Kigoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.


Mhe. Mwambegele ameeleza kwamba uamuzi huo wa Tume umetokana na kuzingatiwa kwa maoni ya wadau waliyotoa wakati wa mikutano iliyofanyika Jijini Dar es Salaam na Kigoma.


“Tume imezingatia maoni na ushauri wa wadau. Hivyo, uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utaanza tarehe 20 hadi 26 Julai, 2024 badala ya tarehe 01 hadi 07 Julai, 2024, mkoani Kigoma na uzinduzi utafanyika siku hiyo ya tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb),” amesema Mh. Mwambegele.


Akizungumzia maoni hayo ya wadau, Mhe. Mwambegele amesema Tume imefanya mikutano tisa ya wadau ngazi ya Taifa mkoani Dar es Salaam kati ya tarehe 07 hadi 15 Juni, 2024 na mkutano mmoja wa wadau ngazi ya mkoa kwa mkoa wa Kigoma uliofanyika tarehe 19 Juni 2024.


Amewataja wadau waliokutana na Tume kuwa ni pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, wanawake na Wazee wa Kimila.


“Vyama vya siasa vilitoa maoni na ushauri wa kupatiwa muda wa kutosha kwa ajili ya kuwapata mawakala wa uandikishaji ili mawakala hao waweze kushiriki katika zoezi kikamilifu. Aidha, vyama viliishauri Tume isogeze mbele muda wa kuanza kwa zoezi la uboreshaji ili kutoa fursa kwa wao kuhamasisha wananchi na wafuasi wao kujitokeza katika zoezi hilo,” amesema Jaji Mwambegele.


Amewataja wadau wengine waliotoa maoni kuwa ni pamoja na taasisi na Asasi zilizoomba kibali cha kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji ambazo zilieleza kuwa kibali kinapotolewa na Tume huwa ni muda mfupi kufikia zoezi la uboreshaji kuanza na wakashauri Tume ione namna ya kutoa kibali kwa muda utakaowawezesha kupata fedha kutoka kwa wafadhili ili zoezi likianza nao waanze kutoa elimu hiyo.


Kwa upande wa Taasisi na Asasi zilizoomba kibali cha kuwa waangalizi wa uandikishaji wakati wa uboreshaji, zilieleza kuwa kibali kinapotolewa na Tume huwa ni muda mfupi kufikia zoezi la uboreshaji kuanza na wakashauri Tume ione namna ya kutoa kibali kwa muda utakaowawezesha kupata fedha kutoka kwa wafadhili ili zoezi likianza nao waanze kazi ya kutazama namna zoezi linavyoendeshwa.


Maoni mengine ya wadau yaliyopelekea Tume kufikia uamuzi huo wa kusogeza mbele tarehe ya kuanza na kuzindua uboreshaji wa Daftari ni yale ya kuishauri Tume ijipe muda wa kutosha kutoa elimu ya mpiga kura kwa wadau na wananchi kabla ya kuanza kwa zoezi lenyewe, ili wananchi wengi waweze kuelewa zoezi husika na hivyo kuwawezesha kujitokeza kwa wingi wakati zoezi litakapoanza.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele akizungumza na waandishi wa Habari mkoani Kigoma leo tarehe 22 Juni, 2024 kuhusiana na kusogezwa mbele kwa uzinduzi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo sasa utafanyika tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele akizungumza na waandishi wa Habari mkoani Kigoma leo tarehe 22 Juni, 2024 kuhusiana na kusogezwa mbele kwa uzinduzi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo sasa utafanyika tarehe 20 Julai, 2024 mkoani Kigoma. Pamoja na e ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk.
Baadhi ya wajumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wakiwa katika mkutano huo leo
Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo.
Baadhi ya Wajumbea na Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
Baadhi ya Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages