Na HEMEDI MUNGA, Iramba
OFISA Elimu wa mkoa wa Katavi (REO), Upendo Rweyemamu amepongeza Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi Awali wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida, Rose Kibakaya kwa kutodaiwa na walimu fedha za likizo.
Aidha, amempongeza Ofisa Elimu huyo, kwa kuwa na utaratibu wa kuwalipa walimu fedha za likizo kwa wakati kabla hawajaanza likizo zao.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk. Charles Msonde, katika kikao kazi cha kuhamasisha ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika mamlaka za serikali za mitaa kilichofanyika katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri hiyo mjini hapa, Upendo amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa nia ya dhati ya kutatua malalamiko ya walimu.
Amesema walimu wote nchini wamekuwa na changamoto zinazofanana ambazo serikali imekusudia kuzitatua zote.
Upendo ametaja baadhi ya changamoto hizo ni kupanda madaraja, Kubadilishiwa muundo baada ya kujiendeleza kielimu, madai au mapunjo ya mshahara.
Nyingine ni kulipwa stahiki za likizo, kulipwa stahiki za uhamisho na matumizi ya lugha zinazodaiwa kutokuwa za staha kutoka kwa baadhi ya viongozi.
"Changamoto zote hizi, serikali imeamua kuzifanyia kazi na kuziondoa kabisa kwa lengo la kuwaacha walimu wakifanya kazi kwa furaha," amesema.
Pia, amewatoa hofu viongozi hao, kwa sababu mambo yameishaanza na yanaendelea kwa lengo la kuhakikisha kila mwalimu nchini hahangaiki kupanda madaraja.
"Nimeelekezwa nitamke kwamba, ifikapo mwezi Julai 01, 2024 walimu 54,000 watapanda kwa mserereko na walimu 52,000 watapanda kawaida," amethibitisha.
Hivyo, amewataka walimu hao, kutimiza haki yao ya kufanya kazi kwa lengo la kupata maboresho wanayoyahitaji katika kipindi hiki ambacho serikali inawahangaikia.
Kwa upande wa Ofisa Elimu wa mkoa huo (REO), Dk. Elipidius Baganda amemuhakikishia kiongozi huyo, yote aliyoyaelekeza watayafanyia kazi.
"Niwaombe viongozi wote tukayafanyie kazi tuliyoelekezwa na kuendelea kutembea kifua mbele, kwa sababu viongozi wote wametengenezwa na Mwalimu, hivyo mwalimu ni mtu mkubwa," amesema.
Dk. Baganda amemnukuu Mwalimu Nyerere kuwa, unavyoniona nilivyo sikuzaliwa hivi, nipo kama nilivyo kwa sehemu kubwa ya ualimu.
Naye Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Mbelekese wilayani hapa, Sebastian Gunda amemshukuru kiongozi huyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote aliyowapatia.
"Ninaamini siku zimebakia chache kwa sababu tarehe mosi sio mbali, hivyo tumeyapokea maelekezo yako," amesema.
OFISA Elimu mkoa wa Katavi (REO), Upendo Rweyemamu akimtunuku zawadi ya pesa Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi Awali wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida, Rose Kibakaya kwa kutodaiwa na walimu fedha za likizo, wakati wa kikao kazi cha kuhamasisha ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika mamlaka za serikali za mitaa kilichofanyika katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
OFISA Elimu mkoa wa Katavi (REO), Upendo Rweyemamu akieleza alivyoguswa na utendaji kazi wa Mkuu wa Divisheni ya Elimu Msingi Awali wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida, Rose Kibakaya kwa kutokua na madai ya likizo kwa walimu, wakati wa kikao kazi cha kuhamasisha ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika mamlaka za serikali za mitaa kilichofanyika katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
Baadhi ya Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wakifuatilia maalekezo ya OFISA Elimu mkoa wa Katavi (REO), Upendo Rweyemamu, wakati wa kikao kazi cha kuhamasisha ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika mamlaka za serikali za mitaa kilichofanyika katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
Baadhi ya Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wakifuatilia maalekezo ya OFISA Elimu mkoa wa Katavi (REO), Upendo Rweyemamu, wakati wa kikao kazi cha kuhamasisha ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu wa shule za msingi na sekondari katika mamlaka za serikali za mitaa kilichofanyika katika ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇