LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 24, 2024

DC MWENDA AWAFUNDA VIJANA NCHINI




 Na HEMEDI MUNGA, Iramba 


HOTUBA ya Mwalimu Julius Nyerere alioitoa mwaka 1988 wakati wa maadhimisho ya miaka 11 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani  Tabora imetajwa kuwa msingi wakupata  mioyo ya kujitolea kwa vijana wakiwemo wale wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho.


Aidha, vijana wa sasa wametakiwa waweze kujitoa kwa lengo la kukijenga Chama Chao.


Akizungumza  katika kikao cha Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama hicho, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda amesema Mwalimu Nyerere wakati akihutubia katika maadhimisho hayo, alikumbusha yale waliyoyapitia wakati wanapambania nchi hii ipate uhuru.


"Ni katika hotuba chache ambazo Mwalimu Julius Nyerere alihuzunika  kwa kuwakumbuka wenzake ambao baadhi yao walikua wamekwisha poteza uhai kwa kupigania uhuru," amesema.


Amebainisha kuwa watu waliojitoa kipindi hicho hawakuwa na mali wala elimu, lakini walikua na moyo wa kujitolea.


Ameweka wazi,  hawakuwa wanataka kulipwa, hawakudai uhuru kwa lengo la kupata uongozi ispokua kwa lengo la umma wao jambo ambalo kwa Umoja wa Vijana moyo unaoitwa wa kujitolea umeanza kufifia katika dhana ya umoja huo.


DC Mwenda ameeleza kuwa kijana wa leo, ukimuona yuko mbelembele basi anawaza fulusi, kunacheo anakitazamia au mpango ameutega.


"Bila ya cheo na hela humpati kijana kwenye kazi za chama, lazima niwakumbushe wajibu wetu wa msingi ni kujitoa kwa ajili ya chama chetu," amesisitiza.


Mbali na hayo, Mwenda amesema kama kuna jumuiya ambayo anaunasaba nayo na kuiangalia kwa macho mawili ni Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa chama hicho.


Amewafahamisha wajumbe hao,  utaratibu wa utendaji kazi wa  CCM umewekwa kama daraja ambalo linawaunganisha wananchi na serikali yao walioichagua.


Ameeleza wajibu wakwanza wa chama hicho kwa wananchi ni kupokea maoni, mawazo na matarajio yao juu ya serikali inayowaongoza.


Pia, ametaja wajibu wapili wa kuielekeleza serikali ni nini wananchi wanataka kutoka kwenye serikali yao huku wajibu wa tatu ni kurudi kwa wananchi kuwaeleza serikali yao inafanya nini na kwa nini inayafanya hayo.


Amedokeza kuwa serikali inajenga Reli ya Kisasa (SGR), kununua ndege, kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, kuongeza ruzuku kwenye kilimo, kujenga barabara na  kupeleka umeme kila kijiji ni wajibu wa Chama kwenda kuwaeleza wananchi kwa nini inayafanya haya.


"Ikiwa ni wajibu wa chama, basi ni wajibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenda kuwaeleza wananchi serikali yao inafanya nini kwa ajili ya maendeleo yao," amesisitiza.


Amesema wajibu huu umesahaulika kwa vijana kwa sababu vijana wenyewe hawana ufahamu wa nini serikali yao inafanya licha ya takwa la kikatiba kuyaeleza hayo kila baada ya miezi mitatu, kitu ambacho kinafanyika.


"Mimi ni kijana mwenzenu wajibu wangu wa kwanza ni kukumbusha juu ya wajibu huu, lazima tuoneshe kuwa Singida inaovijana na wanaweza kuhangaika na wapinzani kabla ya Chama hakija fungua mdomo," amesisitiza.


Mwaka 1988, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akiwa bado ni Mwenyekiti wa Chama hicho, alialikwa kama mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambapo aliwashukuru wazee kwa moyo wa kujitolea.


Mwalimu Nyerere alishuhudia mioyo iliyojitolea ambayo ilikua tayari kuondoka katika dunia kuliko kutawaliwa, hivyo waliweka rehani maisha yao, mali zao, familia zao, utu na heshima zao kwa maisha ya wengi.

Mkuu wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida, Suleiman Mwenda akiwakumbusha  Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa na mioyo ya kujitolea, wakati wa kikao cha Baraza hilo, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano mjini Kiomboi.  (Picha na Hemedi Munga)

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakifurahia maelekezo ya viongozi wao, wakati wa kikao cha Baraza hilo, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mkoani Singida. (Picha na Hemedi Munga)

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages