LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 16, 2024

SIMBACHAWENE: SERIKALI IMETOA SH. BIL 696 KWA KAYA MASIKINI





 WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema hadi kufikia Juni mwaka jana serikali ilikuwa imetoa sh. bilioni 696.7 kwa ajili ya kupunguza na kuondoa umaskini kwa kaya zipatazo milioni 1.37  katika vijiji, mitaa na shehia 17,260.

 Simbachawene amesema hayo jijini hapa jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

 Alisema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita na awamu zilizopita zinazoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kupunguza na kuondoa umaskini wa kipato.

  Amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ulianzishwa na serikali ya J mwaka 2000 kama mojawapo ya mikakati ya kupambana na umaskini kwa kutumia dhana ya ushirikishaji jamii.

 “TASAF imekuwa ikitekelezwa kwa awamu tangu kuanzishwa kwake. Awamu ya Kwanza ya TASAF ilianza mwaka 2000 – 2005 na ilijumuisha maeneo ya utekelezaji 42 ambapo 40 ni ya Tanzania Bara na mawili  ya Zanzibar (Unguja na Pemba).

 Ameongeza kuwa :”Jumla ya miradi 1,704 ya huduma za jamii yenye thamani ya sh. bilioni 72 ilitekelezwa kupitia mpango huu wa TASAF I. Awamu hii ilitekelezwa kwa mafanikio makubwa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu za kijamii katika sekta mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, miundombinu na afya,”.

 Simbachawene alisema awamu ya Pili ya TASAF ilianza utekelezaji mwaka 2005 hadi 2013 katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar.

 Amefafanua kuwa  jumla ya miradi 12,347 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 430 ilitekelezwa wakati wa Awamu hii ya Pili ya TASAF (TASAF II).

 

“Katika kipindi cha utekelezaji wa TASAF Awamu ya Kwanza na ya Pili, wananchi walishiriki vyema kutekeleza miradi mbali mbali iliyoboresha upatikanaji wa huduma za jamii. Mbali na miradi ya kuboresha miundombinu kama vile barabara, maji, masoko, huduma za afya, elimu, ustawi wa jamii na mazingira, wananchi katika makundi mbali mbali walitekeleza miradi ya kuongeza kipato ambayo iliwasaidia kukabiliana na umaskini.

 Ameongeza kuwa :”Katika Kipindi cha Pili hadi kufikia Juni 2023 kiasi cha sh. bilioni 696.7 zimehawilishwa kwa kaya za walengwa zipatazo 1,371,916 katika vijiji, mitaa na shehia 17,260,”

 TAKUKURU

Simbachawene amesema katika miaka 60 ya Muungano, serikali inayoongozwa na Rais,  Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa ili wananchi waweze kupata huduma bora.

Alisema TAKUKURU kwa kutambua kuwa Skauti ni suala la Muungano kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ziumeunda timu ya uratibu ya kitaifa yenye Wajumbe kutoka Chama cha Skauti Tanzania (CST), ZAECA na TAKUKURU ili kuimarisha ushirikiano katika jitihada za kupambana na rushwa.

 “Ushirikiano huu ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa kwa kuwa Skauti wapo katika kundi la vijana na ni “Jeshi kubwa” ambalo tumeshuhudia likitoa mchango chanya katika matukio mbalimbali ya kijamii na kitaifa,”alisema .

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages