Na Ibrahim Bakari
Unapokuwa Viwanja vya Ndege vya Dubai (UAE), Amsterdam (Uholanzi), Heathrow (London), na vingine ni kati ya viwanja vikubwa vya ndege ambavyo ndege kubwa za mataifa zinapishana, kutua na kupaa.
Ndege nyingi zinapishana viwanja hivyo na vingine ikiwemo Addis Ababa, Ethiopia kwa kuwa, sehemu kubwa ya abiria huunganisha ndege kwenda kona mbalimbali za dunia.Mazingira hayo yanampa kiu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kutaka kuona siku moja Tanzania inakuwa 'hub' kwa ndege mbalimbali kupishana, kupaa na kutua kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, (JNIA).
Hata hivyo, amesema mipango inafanyika ili Tanzania iwe kiungo muhimu kwa ndege kubwa za kimataifa.
Alisema usafiri wa anga ni kitovu muhimu cha mapato kwa kusafirisha watalii na mizigo ambayo pia itakuwa nafasi kwa wazalishaji kuongeza thamani ya mazao yao kupeleka nje na kupata fedha.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya ndege mpya aina ya Boing 737-9 max ambayo ni ya 15 kwa shirika hilo, Waziri Mkuu alitilia mkazo zaidi uzalendo, uadilifu na uwajibikaji katika kuliendesha shirika hilo na wadau wengine wa usafiri wa anga.
Ameitaka Wazara ya Uchukuzi kusimamia kikamilifu uwekezaji unaofanywa kwenye shirika ili kuleta matokeo chanya na tija na kuendeleza sekta nyingine mtambuka.
Amesisitiza watumishi kuongeza uzalendo na kila mmoja kuthamini uwekezaji kwa kubaini wabadhirifu ambao kimsingi hurudisha nyuma maendeleo ya shirika.
Waziri Mkuu akizungumza kwa hisia, amewataka viongozi na watendaji wa Shirika la Ndege Tanzania, kuhakikisha ndege zinaleta tija kwa kufanya safari ndefu na kuondokana na uahirishaji wa safari kila mara.
Aidha Waziri Mkuu ambaye amesema utaratibu unafanyika ili Uwanja wa Ndege JNIA Terminal II kuwa ya kitaifa, na ATC kuwa eneo lake huku akihimiza kuunganisha huduma za ndege na mikoa yote ya Tanzania.
Tayari Serikali imetenga fedha Shilingi bilioni 30 katika mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya ndege nchini.
Aidha Waziri Mkuu ameitaka Wizara kuongeza wataalamu wazalendo ambao wataleta matokeo mazuri kwa kuongeza vyuo vya mafunzo.
Amesema kwa sasa chuo kinachutumika zaidi kupata wataalamu wa ndege ni kile cha usafirishaji, NIT.
Kwa upande mwingine, wizara kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) imetakiwa kuhakikisha inadhibiti usalama wa ndege pamoja na zile za kimataifa na kuwa na wataalamu wanaoweza kushindana hadi ngazi za kimataifa.
Naye Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo zitakazosaidia kupata watalaamu wazalendo.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇