LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 1, 2024

MACHA AWAONYA WANAOIBUA MASHINDANO YA MICHEZO KUSAKA UBUNGE, UDIWANI KABLA YA MUDA, ASEMA HAO NA WENGINE WATAKAOVUNJA KANUNI KUTEMWA 2025

Ubungo, Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara  Anamringi Macha amesema wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, wakibainika wamevunja kanuni, Chama kitawachukulia hatua za kinidhamu. 


Amewataka wanachama wote wenye nia ya kuwania uteuzi wa kugombea nafasi za uwakilishi katika vyombo vya maamuzi kupitia CCM, kusubiri wakati sahihi ambao utatangazwa kwa mujibu wa taratibu za Kikatiba, Kanuni, Miongozo na maelekezo mbalimbali ya Chama.


Macha ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa CCM, ameyasema hayo jana Disemba 31, 2023, wakati akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Jimbo la Ubungo, mkoa wa Dar es Salaam.


Katika Mkutano huo uliofanyika Mrina Hakk,  Mbunge wa Ubungo, Prof. Kitila Mkumbo alisoma wasilisho la taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025, kwa mwaka 2023, 


Macha pia aliwataka wanachama wa CCM kuwapa ushirikiano viongozi walioko madarakani ili waendelee kutimiza majukumu yao kwa ufanisi bila bughudha.


"Miaka bado haijaisha maana kuna watu wanafikiri imeshaisha na hata kama tunaelekea sasa kwenye uchaguzi lakini muda wa uchaguzi bado haujafika, miaka iliyoisha ni mitatu ambayo ni kama asilimia 65 ya muda wa kiongozi madarakani bado miwili 2024-25.”


Si sahihi wakatokea watu kuanza kufanya kampeni za chinichini kwa sasa, nawaambia muda wa kufikiria ubunge kwa jimbo bado, kufikiria udiwani na wakati madiwani wapo na bado muda wao wa kazi upo...badooo, 


Huu bado ni muda wa wale waliopo madarakani hivyo tuwaache waendelee kufanya kazi zao kikamlifu katika kutekeleza Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM 2020/25,” alisisitiza Macha na kuongeza;


"Nitumie nafasi hii kutoa mwito kwa Ofisi za CCM mikoa yote kwamba fuatilieni sana wale wote ambao wanapitapita huko kutafuta udiwani nje ya utaratibu ili siku ikifika tuwaambie kwa kwaheri kwa sababu moja ya tatizo kubwa ni kutoweka kumbukumbu hivyo tuwaite na tuwaambie kuwa wanachofanya sio sahihi.” 


Amesema CCM Makao Makuu inawafuatilia kwa karibu wanachama wote wanaojipitisha pitisha wakitaka kuwania ubunge au Udiwani kinyume cha taratibu. 


“Tutawaeleza Wanachama wetu nchi nzima kwamba wale wote ambao wanajaribu kuanza kuvunja taratibu za kutafuta uongozi, wao waendelee ila mwezi wa 9 mwaka 2025 watakuja kujuta tutawaweka pembeni. 


Unakuta mbunge yupo bungeni halafu unasikia huko Ubungo kumeanzishwa mbuzi cup. Achaneni na hizo ligi za uongo kama kweli unasaidia Chama, fika kwa Katibu wa Chama aongee na Mwenyekiti waone na waseme huyu ni mpenzi wa Chama Cha Mapinduzi anatoa hiki kusaidia au kuchangia na sio kukimbizana usiku usiku,” alisema  Macha.


Mbali ya kupokea taarifa  ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kutoka kwa mbunge, Macha pia alikabidhi pikipiki nane kwa ajili ya Ofisi za CCM kwenye kata zote nane za jimbo hilo ili kurahisisha shughuli mbalimbali za utendaji, zikiwa zimetolewa na  Mbunge wa Jimbo la Ubungo,  Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji. 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Anamringi Macha, akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Jimbo la Ubungo, mkoa wa Dar es Salaam, jana, Disemba 31, 2023..
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Anamringi Macha, akipongezwa na Mbunge wa Jim o la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo baada ya kuzungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Jimbo la Ubungo, mkoa wa Dar es Salaam, jana, Disemba 31, 2023. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam Abbas Mtemvu.
Wajumbe wakiwa kwenye mkutano huo.
Wajumbe na waalikwa wakiwa kwenye mkutano huo.
'Wapambe' wakimpongeza Mbunge wa Ubungo Prof Kitila Mkumbo baada ya kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwenye Mkutano huo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Anamringi Macha akifurahia moja kati ya Pikipiki nane kabla ya kuzikabidhi kwa ajili za Ofisi za CCM kata zote nane za jimbo la Ubungo kurahisisha shughuli mbalimbali za utendaji, zikiwa zimetolewa na  Mbunge wa Jimbo hilo Prof. Kitila Mkumbo, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.
 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages