Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ameainisha mipango ya serikali kwa mwaka mpya wa 2024, ikiwemo agizo la kuanzisha safari za SGR kati ya Dar es Salaam na Dodoma, na kuanza kazi kwa bwawa la umeme la Julius Nyerere.
Katika hotuba yake ya kuuaga mwaka wa 2023 na kuukaribisha 2024, Rais Dk. Samia ametaja masuala makuu yaliopewa umuhimu katika mwaka wa 2023 huku akielezea mipango ya serikali katika mwaka mpya.
Hotuba yake ilijikita katika masuala makuu 12 kuanzia amani na usalama, sera za kiuchumi hadi mabadiliko ya tabianchi.
Rais Samia amesema imani ya wawekezaji kwa Tanzania imeongezeka katika mwaka unaomalizika ambapo miradi 55 kati ya 504 iliyosajiliwa na kituo cha uwekezaji, TIC, ilikuwa ya upanuzi wa uwekezaji uliopo tayari, huku makusanyo ya kodi yakiongezeka kwa asilimia 8 hadi shilingi trilioni 22.6 ikilingnisha na mwaka 2022.
"Hivyo, jinsi uchumi wetu unavyokua, tutaendelea kuongeza makusanyo kupitia mifumo madhubuti ya ukusanyaji na kuhakikisha kodi inakusanywa kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria," alisema Rais Samia.
Sekta za uzalishaji zinazo jumuisha kilimo, madini na utalii, ambazo ndio tegemeo la uchumi, zimeendelea kuwekewa msisitizo, "ili kuwafikia wazalishaji wengi zaidi, hususan wale wadogo na kuchochea uzalishaji kuanzia ngazi za chini," alisema Rais Samia, na kuongeza kuwa wameongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 751 mwaka jana 2022 hadi sh. bilioni 970 mwaka uliomalizika, ongezeko sawa na asilimia 29.
"Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 17,148,290 msimu wa 2021/2022 hadi tani 20,402,014 msimu wa mwaka 2022/2023, hivyo kufikisha asilimia 124 ya kiwango cha utoshelevu wa chakula nchini," alisema Rais huyo mwanamke wa kwanza kuiongoza Tanzania. "Vilevile, tumehakikisha mazao makuu yanauzwa kwa njia ya minada ili kupata bei nzuri , na tumeanzisha mnada mpya wa
zao la chai."
Kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo
Rais Samia amesema serikali imeendelea na juhudi za kuwashirikisha vijana na wanawake katika kilimo ambapo jumla ya ekari 201,241 zimetengwa kwa shughuli hiyo.
Katika kuimarisha juhudi hizo, Rais Samia amesema serikali yake imeanzisha programu ya kilimo cha kisasa iitwayo Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) ili kuongeza uzalishaji, kuchochea viwanda vya usindikaji, na kutengeneza ajira kwa vijana.
Katika kutambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo kwenye sekta hii mwaka huu, Samia amesema serikali ilinunua mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji hao ili kuongeza tija zaidi na mchango wao kwenye sekta ya madini.
"Mwelekeo wa serikali ni ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini hapa nchini, hatua itakayotuwezesha kuongeza thamani na fursa zaidi za ajira," alisema Rais katika hotuba hiyo iliyotangazwa moja kwa kupitia kupitia televisheni.
Pia Rais Samia alizungumzia hatua zilizochukuliwa kuimarisha sekta ya utalii ambayo imechangia kiasi cha dola ma Marekani bilioni 3.22 kufikia Oktoba 2023 ikilinganishwa na dola za Kimarekani Bilioni 2.33 kipindi kama hicho mwaka 2022.
"Manufaa haya yametokana na juhudi za Serikali na wadau wa sekta hii. Hivyo, n itoe rai kwa watoa huduma kwenye sekta ya utalii , ku endele a kuimarisha huduma zao, na kwa Watanzania wa naoishi maeneo ya vivutio, tuendelee kudumisha ukarimu kwa wageni ili tuendelee kupokea watalii wengi zaidi."
Maendeleo ya sekta ya usafiri
Rais Samia ametoa agizo kwa mamlaka ya usafiri wa reli nchini Tanzania, kuhakikisha kwamba ifikapo mwisho wa Julai 2024, huduma za usafiri kupitia njia ya kisasa ya SGR ziwe zimeanza. "Wananchi wamechoshwa na vijisababu, wanataka kuona reli ikifanya kazi," alisema Rais.
Rais Samia alisema serikali imeendelea kuwekeza katika unenzi wa moindombinu ya barabara, madaraja na vivuko katika mikoa mbalimbali ya nchi, na kufahamisha kuwa ujenzi wa SGR kutoka Dar es Salaa, hadi Morogoro na kutoka Morogoro hadi Makutupora umekamilika kwa asilimia 90.
Aidha, mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, utawezesha ujenzi wa kipande cha Tabora hadi Kigoma na Uvinza hadi Musongati.
Kwenye usafiri wa majini, Rais amesema serikali imekamilisha ujenzi wa gati katika bandari mpya ya Karema kwenye Ziwa Tanganyika, inayotazamiwa kufungua uchumi, biashara, na muingiliano wa watu na DRC na hivyo kukuza uchumi wa Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi.
Kwa upande wa usafiri wa anga, Rais Samia amesema serikali ilikamilisha ununuzi wa ndege moja ya mizigo na moja ya abiria, huku mashirika mbalimbali ya ndege ya kimataifa kama vile Air France na Saudi Airlines yakivutiwa kuanza kutoa huduma za safari kwenda Tanzania. "Tunaamini uwekezaji huu utaimarisha sekta ya utalii na utakuza pia biashara ya kilimo cha maua na mbogamboga."
Kuanza kazi kwa bwawa la umeme la Nyerere Rais Samia amekiri juu ya changamoto ya mgao wa umeme ambao umegeuka sugu na kuathiri ukuaji wa uchumi wa taifa hilo la Afrika Mashariki. Amesema tatizo hilo ndiyo liliifanya serikali kuchukua uamuzi mwaka 2017 kuanzisha mradi za bwawa la umeme la Julius Nyerere, ambalo linatazamia kuingiza megawati 2,115 kwenyw gridi ya taifa.
Rais amefahamisha kuwa mwezi Februari mtambo wa kwanza wa kuzalisha umeme bwawani hapo utawashwa rasmi, na mtambo wa pili utawashwa mnamo mwezi Machi. Mitambo hiyo miwili itazalisha jumla ya megawati 470 na hivyo kufidia upungufu wa sasa ambao ni megawati 300.
"Ni imani yangu na Serikali kwa ujumla kuwa, hatua hizi zita leta ufumbuzi w a kudumu kwa suala la mgao wa umeme nchini," alisema Rais Samia na kuongeza kuwa serikali inaendelea pia kuwekeza kwenye vyanzo vingine vya umeme kama vile gesi, jua, na upepo , ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa nishati hiyo.
Uwekezaji kwenye sekta ya afya.
Rais Samia amesema nguvu kubwa imewekwa kwenye kuimarisha huduma za afya kwa kuajiri wataalam, ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendea kazi. Amesema mwaka 2023, serikali imeajiri jumla ya wataalam 17,309 na ilitenga jumla ya shilingi bilioni 190.9 kwa ajili ya kununua dawa.
Rais amesema uwekezaji unaofanywa wenye sekta ya afya umeleta matokeo yanayoonekana dhahiri, ambapo kuanzia mwezi Januari mpaka Novemba, 2023, jumla ya wananchi 15,386 wamepata huduma za CT Scan kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini kote na hii imesaidia katika kuimarisha mfumo wa rufaa na huduma za uchunguzi kwa Mikoa yote.
Jumla ya wagonjwa 200 wamepimwa kipimo cha MRI katika hospitali za rufaa za kanda ya Mbeya, Chato, na Mtwara. "Hospitali hizi hazikuwahi kuwa na kipimo cha aina hii, hivyo uwepo wa mashine za MRI zimeleta ahueni ya gharama kwa wananchi wa kanda husika," alisema rais.
Elimu, Diplomasia na Tabianchi
Rais pia amezungumzia juhudi za kuboresha sera na mitaala ya elimu, kushughulikia changamoto za malazi ya walimu, na kuongeza bajeti ya mikopo ya wanafunzi.
Kuhusu mahusiano ya kimataifa, Rais Samia ameelezea mafanikio katika mazungumzo ya kidiplomasia, kupata misaada ya kifedha, kuunda fursa za bidhaa za Kitanzania katika masoko ya kimataifa, na kurejea katika programu za maendeleo kimataifa.
Ametaja fursa za Tanzania kuwakilishwa katika mikutano muhimu ya kimataifa kama vile wa mataifa ya kundi la BRICS, Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya
Afrika, Jukwaa la Uchumi la Davos na mikutano ya Afrika na nchi mbali mbali zenye nguvu za kiuchumi.
Ametaja pia wageni kadhaa mashuhuri walioitembelea Tanzania, wakiwemo Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, Marais wa Indonesia, Hungary na Romasia pamoja na nchi jirani na rafiki za Afrika. Pia ametaja ziara alizozifanya nje ya nchi na kuorodhesha mafanilioni yaliotokana na ziara hizo.
Amehimiza uhifadhi wa mazingira, na kushughulikia changamoto zinazosababishwa na matukio ya hali ya hewa yanayohusiana na El Nino, na kuwataka wananchi waendelee na juhudi za kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka kama inavyoeleza ilani ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi, CCM.
Your Ad Spot
Jan 1, 2024
Home
featured
Kitaifa
RAIS DK. SAMIA ATAJA MAFANIKIO LUKUKI 2023, ATIRIRIKA MIPANGO KAMAMBE 2024, NI KATIKA HOTUBA YAKE KUAGA 2023 NA KUULAKI 2024
RAIS DK. SAMIA ATAJA MAFANIKIO LUKUKI 2023, ATIRIRIKA MIPANGO KAMAMBE 2024, NI KATIKA HOTUBA YAKE KUAGA 2023 NA KUULAKI 2024
Tags
featured#
Kitaifa#
Share This
About Bashir Nkoromo
Kitaifa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇