*
*Asema CCM itaongeza kasi kusimamia Serikali kwa weledi, bila kiburi, wala kuwatukana watendaji*
*Asisitiza Watanzania wanatambua CCM ndiyo Chama kiongozi, hakuna haja ya kutukana kusimamia Ilani ya Uchaguzi*
*Awataka wanasiasa kutambua watapimwa kwa hoja, sio maandamano*
Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Dkt. Emmanuel John Nchimbi amewataka viongozi wa CCM kuongozea kasi ya kutimiza wajibu wa Kikatiba na kikanuni wa kuisimamia Serikali na watendaji wake wanapotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kwa weledi na heshima, bila kiburi wala kuwatukana.
Ndugu Nchimbi amesema kuwa katika kuisimamia Serikali inapotekeleza wajibu wake kupitia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 - 2025, wanaCCM wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuelezea mafanikio na kazi kubwa inayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Ndugu Nchimbi pia amesisitiza jinsi ambavyo milango ya CCM, ikiwa ni pamoja na kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama, iko wazi kwa ajili ya kushirikiana na vyama vingine vya siasa na kuzungumza masuala mbalimbali kwa ajili ya maslahi ya taifa, huku akisema kuwa wanasiasa wanaohamasisha maandamano badala ya kujenga hoja katika majadiliano, ni waoga na wanakwepa mijadala.
Katibu Mkuu Dkt. Nchimbi ameyasema Jumamosi, Januari 20, 2024 wakati akiwahutubia maelfu ya wananchi mbalimbali wa Jiji la Dar Es Salaam, wakiwemo viongozi, wanachama na wafuasi wa CCM waliojitokeza kwa wingi Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar Es Salaam, kumlaki wakati wa mapokezi ya kumpongeza kwa kuteuliwa kushika dhamana hiyo ya Mtendaji Mkuu wa CCM.
“Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kutimiza ahadi zake na kuisimamia serikali. Ninawaahidi, kwa kushirikiana na viongozi wenzangu, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama, tutaendelea kukiimarisha chama lakini pia kuhakikisha hatumuangushi Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa Chama kwa imani yake aliyotupatia. Chama chetu kitaendelea kupata ushindi kwa sababu tumefanya kazi kubwa na zinazoeleweka.
“Tuendelee kufanya kazi usiku na mchana, kazi ya kutafuta ushindi wa chama chetu. Tufanye kazi kwa juhudi na umakini zaidi katika maeneo yaliyobakia. Wakati huo huo Chama chetu kisikwepe wajibu wa Kikatiba na Kikanuni kuisimamia Serikali, kwa weledi bila kutukana. Tuongoze kwa weledi, ili watendaji wa Serikali wafanye kazi vizuri na wajue kuwa tunawapenda na kuwaheshimu. Isipokuwa tu wote tuongeze kasi ya kuwatumikia wananchi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi,” amesema Ndugu Nchimbi.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa Watanzania kudumisha utaifa wao na kuenzi tunu za amani na utulivu kuwa ndiyo msingi wa maendeleo na alama kubwa ya Tanzania duniani, Katibu Mkuu Dkt. Nchimbi amsema kuwa milango ya CCM na hususan kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, iko wazi wakati wowote utakapohitajika ushirikiano baina ya vyama vya siasa, kwa maslahi ya taifa.
“Tunavyo vyama vya siasa nchini, tuendelee kushirikiana navyo. Milango ya ofisi yangu iko wazi. Wote tuna nia moja. Tutaendelea kushirikiana nao. Lakini kushirikiana nao haimaanishi kupunguza kasi ya kutafuta ushindi, kuongeza wabunge bungeni na madiwani, Serikali za Mitaa na ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa Rais mwakani.
“Vyama vya siasa, wanasiasa na wadau wote wa maendeleo dhamira ya mazungumzo ni muhimu ikaakisi kote. Kukimbia na kukwepa mazungumzo sio ujasiri. Huo ni uoga. Hoja hujengwa kwa mdomo sio kwa miguu. Tunataka tuwapime kwa hoja zao, sio kwa miguu yao kuandamana. Vyama vya siasa vijitofautishe na mashindano ya urembo ambako hupimwa kwa jinsi wanavyotembea. Tutumie ubongo kufikiria, sio miguu,” amesema Ndugu Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi pia alitumia hadhara hiyo pia kuwapatia pole wakazi wa Dar Es Salaam kutokana na athari za mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia siku ya mapokezi hayo, akimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Ndugu Albert Chalamila kuhakikisha serikali mkoani humo inachukua juhudi za makusudi kuwasaidia wananchi kutokana na athari kubwa zilizosababishwa na mvua hiyo.
Amesisitiza kuwa katika utendaji kazi wake, daima amekuwa mtu anayependa vitendo zaidi, kuliko maneno, kwa sababu tija inayokusudiwa na kutumainiwa na wananchi, kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote, itapatikana kupitia vitendo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar Es Salaam Ndugu Abbas Mtevu amesema chama kinatarajia kushinda kwa kishindo mitaa yote 574 ya mkoa wa huo.
Halikadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Ndugu Albert Chalamila amesema wanatekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025, hivyo viongozi wanapoanza kampeni hawatapata tabu kujieleza kwa wananchi, kwa sababu kazi zinajieleza zenyewe, huku pia akiahidi kuwa hata miundombinu iliyoathirika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku, itafanyiwa kazi ndani ya saa 24 kurejesha hali vizuri.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇