LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 3, 2024

DG ANETH: MITAALA ILIYOBORESHWA ITAKIDHI MAHITAJI HALISI YA JAMII, YAMEONGEZWA MAUDHUI YA KISASA NA KUONDOLEWA YALIYOPITWA NA WAKATI

Na Bashir Nkoromo, Official CCM Blog, Morogoro
Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba amesema, maboresho yaliyofanyika katika mitaala ya Elimu ya Awali na Msingi, yameongezwa maudhui ya kisasa na kuondoa yaliyopitwa na wakati na pia kuondoa kujirudia kwa maudhui katika somo baina ya masomo.

Pia umepunguzwa wingi wa maudhui katika kila somo ili uwiane na muda wa kufundishia na mahitaji ya halisi ya jamii kwa kuzingatia mifano mizuri kutoka mataifa mbalimbali.

Dk. Aneth amesema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Mitaala hiyo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi-Elimu wa mikoa na Maafisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri nchini kote, iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Bernard Bendel, Kola B Mjini Morogoro, leo Janauari 3, 2024.

Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha viongozi hao kuelewa maboresho mahsusi ya mitaala yaliyofanyika, ikiwemo maboresho katika Muundo wa Elimu, Dira na malengo makuu ya Elimu nchini, Malengo ya Elimu ya Awali na Msingi, Maeneo ya Ujifunzaji, umahiri na masomo katika ngazi ya elimu ya awali na msingi mtawalia, ili waweze kusimamia utekelezaji wa mitaala hiyo kwa ufanisi, katika maeneo wanayotoka.

Akiendelea kueleza kuhusu Dk. Aneth alisema wameboresha maeneo ya ujifunzaji ya Elimu ya Awali na msingi na kwa sasa maeneo ya ujifunzaji katika ngazi ya elimu ya Awali ni matano akiyataja kuwa ni •Utamaduni, Elimu ya Imani, Sanaa na Michezo, •Lugha na Mawasiliano, •Stadi za awali za maisha, •Afya na Mazingira, •Stadi za awali za Kihisabati, Kisayansi na TEHAMA.

"Aidha, maeneo ya ujifunzaji kwa Elimu ya Msingi Darasa la Kwanza na la Pili nayo yameboreshwa na sasa ni matatu ambayo ni Lugha, mawasiliano na stadi za hisabati, Utamaduni, Imani, Afya, Mazingira, sanaa na michezo.

Kwa upande wa Darasa la 1- 6 maeneo ya ujifunzaji ni matano ambayo ni Lugha na mawasiliano, Hisabati, Sayansi ya Jamii, Sayansi na Teknolojia na Sanaa na Michezo", akasema Dk. Aneth.

Akafafanua kuwa, maeneo hayo katika ngazi ya Elimu ya Msingi Darasa la 1- 6 yamebeba masomo ya Kiswahili, Kiingereza, lugha za kigeni za Kiarabu, Kichina na Kifaransa, Hisabati, Historia ya Tanzania na Maadili, Jiografia na Mazingira, elimu ya Dini, Sayansi na Sanaa na Michezo.

Alimwambia Mgeni rasmi kwamba Washiriki pia watachambua Mtaala wa elimu ya Awali na Msingi pamoja na Muhtasari wake kuwawezesha kujifunza juu ya utekelezaji wa mitaala katika ngazi ya darasa.

"Mfano watapitishwa juu ya muda wa utekelezaji wa mtaala kuanzia muda wa kipindi mpaka saa na siku ambazo zinatakiwa katika kutekeleza mtaala kwa mwaka na kwa ngazi husika. Kwa mfano mtaala wa elimu ya awali unasema kuwa Mwaka wa masomo una siku 194 sawa na wiki 39 zenye mihula miwili ya masomo.

Muda wa ujifunzaji kwa siku ni saa tatu na nusu na muda wa kipindi ni dakika ishirini. Hivyo mtaala unabainsiha muda wa Vipindi vya masomo na muda wa kufanya shughuli nyingine za ujifunzaji ikiwemo kucheza, kujisomea na kupumzika", alifafanua Dk. Aneth.

Alisema pia washiriki watapitishwa katika mambo kadhaa ikiwemo (i) Namna ya Kuchopeka matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji wa kila umahiri na masomo, (ii) Kutumia teknolojia na kufaragua zana katika ufundishaji na ujifunzaji. (iii) Kuchopeka masuala mtambuaka mbalimbali katika Masomo Bobezi.

Alitaja baadhi ya Masuala mtambuka yaliyochopekwa katika ngazi ya Elimu ya Awali na msingi kuwa ni; Mazingira, Afya, Elimu jumuishi, Elimu ya jinsia, Elimu ya ya Amani na maadili, Haki na wajibu wa mtoto, Haki za binadamu, Ulinzi na usalama, Usalama barabarani, Elimu ya fedha, Elimu ya mapambano dhidi ya rushwa na Ushirika na masuala ya muungano.

Aliyefungua mafunzo hayo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe, ambaye aliwasihi washiriki wote kuzingatia kwa makini mafunzo hayo ili kukidhi azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha Watanzania wanapata elimu bora na siyo bora elimu.

Mafunzo kwa Viongozi hao, yamefuatia mengine yaliyofanyika  katika ukumbi huo kwa Wawezeshaji na walimu wa shule za msingi zisizokuwa za serikali ambayo yalifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo.

Taasisi zilizotoa washiriki wa mafunzo hayo walikuwa ni Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Tume ya Kikristu ya Huduma za Jamii Tanzania (CSC), Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), Tanzania Association of Private Investors (TAPIE), Baraza la Sunnah Tanzania (BASUTA), Mrtandao wa Elimu Tanzania (TENMET).

Nyingine zilikuwa Tanzania Association of Women Owners of School and Colleges (TAWOSCO), Umoja wa Wazazi wa CCM Tanzania, Tanzania School Empowerment and Service Organiation (TASESO), Shule za Wasabato na Shule za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akifungua mafunzo ya Mitaala hiyo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi -Elimu wa mikoa na maafisa elimu ya Msingi wa Halmashauri nchini kote, iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Bernard Bendel, Kola B Mjini Morogoro, leo Janauari 3, 2024. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba, akieleza muktadha na maudhui ya Mitaala iliyoboreshwa kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe kufungua mafunzo ya Mitaala hiyo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi -Elimu wa mikoa na maafisa elimu ya Msingi wa Halmashauri nchini kote, iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Bernard Bendel, Kola B Mjini Morogoro, leo Janauari 3, 2024.
Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ya MitaalaTET Dk. Fika Mwakabungu akiongoza itifaki wakati wa
mafunzo ya Mitaala hiyo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi -Elimu wa mikoa na maafisa elimu ya Msingi wa Halmashauri nchini kote, iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Bernard Bendel, Kola B Mjini Morogoro, leo Janauari 3, 2024.
Kiongozi wa Uongozi wa Shule ya Msingi ya Bernard Bendel yalifanyika mafunzo hayo alipokuwa akiwakaribisha wote waliohudhuria.
Baadhi ya wawezeshaji na viongozi mbalimbali wakaiwa kwenye mafunzo hayo.
Washiriki mbalimbali wakiwa kwenye mafunzo hayo. Washiriki mbalimbali wakiwa kwenye mafunzo hayo. Washiriki mbalimbali wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mkurugenzi Msaidizi Elimu, OR -TAMISEMI Susana Nussu Nyarubamba.
Mwenyekiti wa Maafisa Elimu Taifa Michael Ligola
PICHA ZA KUMBUKUMBU👇
==========
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba wakati akitoka ukumbini baada ya kufungua mafunzo hayo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akisikiliza jambo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba wakati akiagana kabla hajaondoka eneo la tukio.
"Bila shaka TET tunaenda vizuri katika jambo hili", ni kama ndivyo walivyokuwa wakisema viongozi hawa wa TET baada ya Naibu Katibu kufungua mafunzo hayo. Kushoto ni DG Dk. Aneth na kulia ni Mkurugenzi Dk. Fika.
Washiriki wakipata chai wakati wa mapumziko mafupi, baada ya mafunzo kufunguliwa.

©2024 Official CCM Blog/Bashir Nkoromo

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages