LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 18, 2023

RAIS DK. MWINYI AWAKARIBISHA WAROMANIA KUWEKEZA KATIKA SEKTA ZA UCHUMI WA BULUU, RAIS KLAUS AVUTIWA NA DIRA YA MAENDELEO ZANZIBAR

Ikulu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amezikaribisha Kampuni za Romania kufika kuwekeza Zanzibar katika sekta za Uchumi wa Buluu na Utalii ambazo ni sekta za kipaumbele kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Dk. Mwinyi ametoa makaribisho hayo, leo Novemba18, 2023, Ikulu Zanzibar, wakati wa hafla ya chakula cha mchana iliyoandaliwa kwa heshima ya Rais wa Romania Klaus Iohannis ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku nne.

Dt. Mwinyi amesema, ziara ya Rais Iohannis ni heshima kubwa kwa Zanzibar na imedhihirisha kuwa licha ya nchi hizo mbili kuwa mbali kijiografia lakini zinaweza kufanya kazi pamoja kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Ametoa mwito kwa Romania kufika Zanzibar, kisiwa kilichojaliwa vivutio vingi vya utalii na vinavyovutia na kumhakikishia Rais Iohannis, kuwa hatajutia uamuzi wake wa kupanga kutembelea Mji Mkongwe kwa kuwa atafurahia historia na mandhari nzuri ya Mji huo.

Kwa upande wake, Rais wa Romania alieleza furahishwa na dira ya Maendeleo ya Zanzibar na kuahidi kuwa Serikali yake itashirikiana na Zanzibar ili kufanikisha utekelezaji wa Dira hiyo.

Amesema ziara yake ni moja ya jitihada za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Romania na Tanzania ambao mwezi Mei 2024 utafikisha miaka 60 tangu ulipoanzishwa mwaka 1964.

Rais Iohannis atamaliza ziara yake nchini kesho Novemba 19, 2023, huku katika ziara hiyo akiwa amefanya mambo mbalimbali ikiwemo uwekaji saini Hati za Makubaliano kuhusu kushirikiana na Tanzania katika masuala ya utafiti wa kisayansi katika kilimo na usalama wa chakula pamoja na kukabiliana na majanga.


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages