Na Bashir Nkoromo, Official CCM Blog
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilipokuwa kinajipanga kutafuta kura kwa Watanzania ili kipate ridhaa ya kuliongoza taifa kwa awamu ya tano, baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, kiliandaa kwanza ahadi zake kwa ajili ya kuzinadi kwenye kampeni za Uchaguzi huo.
Ikitambua itawaomba ridhaa Watanzania siyo kwa ajili ya kushika dola tu, bali kuunda serikali itakayowajali na kuwatumikia kwa dhati, ilihakikisha ahadi hizo ni zenye mashiko na zinazolenga kulivusha taifa kutoka hatua moja hadi nyingine kubwa zaidi.
Ahadi hizo iliziweka katika Kitabu cha kurasa 297, kikiwa ndiyo ilani ambayo Chama kitaisimamia kuhakikisha serikali inaitekeleza bila kutetereka, ndani ya kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka huo wa 2020 ulipofanyika Uchaguzi Mkuu hadi taifa litakapaoingia tena katika uchaguzi mkuu mwingine mwaka 2025.
Ilani hiyo imeanisha mambo kadhaa ikiwemo kusimamia Mapinduzi ya Uchumi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa kwa jumla, kuanzisha na kuboresha zaidi huduma za jamii, na maeneo mengine ya kipaumbele.
Hayo yaliyomo katika Ilani hiyo hadi kufikia Serikali ya Awamu hii ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, yametekelezwa kwa kiwango kikubwa kwa kusimamiwa vema na CCM na Serikali ikiyatekeleza kwa vitendo kupitia taasisi zake mbalimbali.
Miongozi mwa taasisi ambazo zimeonekana kuchomoza kwa kasi katika kutekeleza kwa dhati ilani ya CCM ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kuitekeleza Ilani hiyo, katika mpango mkakati wake, pamoja na kuzingatia mipango mingine ya Serikali na miongozo iliyopo, imeuandaa pia kwa kuoanisha Ilani hiyo ya CCM.
Hayo yamewekwa bayana na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Masha Mshomba, alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa majukumu na mafanikio yaliyopatikana kuanzia Machi 2021 hadi Juni 2023, katika
Mkutano wa Mfuko huo na Wahariri wa Vyombo vya Habari, uliofanyika
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar
es Salaam, leo, Septemba 25, 2023.
Mkutano huo ulifanyika ukiwa ni mwendelezo wa Mikutano baina ya taasisi za serikali na wahariri, ambayo imekuwa ukiratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), kwa lengo la wahariri hao kuwa kiunganishi cha mawasiliano baina ya Taasisi za Umma na Wananchi katika kupata taarifa sahihi za taasisi hizo.
"Mpango Mkakati huu, pamoja na kuzingatia mipango mingine ya Serikali na miongozo iliyopo, umeandaliwa pia kwa kuoanisha Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 na mikakati ya Mfuko hususani katika maeneo yafuatayo: i. Kuongeza wigo wa hifadhi ya jamii kwa sekta rasmi na isiyo rasmi nchini Tanzania kama ilivyoelezwa katika Sura ya Sita, Ibara ya 130, Aya (c) ya Ilani ya Uchaguzi. Hili ni eneo la kipaumbele kwa Mfuko na limeainishwa katika malengo ya Mpango Mkakati wa Mfuko.
ii. Kukuza uwekezaji katika sekta ya kilimo na viwanda ambazo zinaajiri idadi kubwa ya watu kama ilivyoelezwa katika Sura ya Pili, Ibara ya 46, Aya (c) ya Ilani ya Uchaguzi. Mfuko umewekeza kwenye sekta hizi kupitia kiwanda cha sukari Mkulazi kinachotarajiwa kuanza uzalishaji mwishoni mwa mwezi Oktoba 2023 ambapo jumla ya Watanzania wapatao 11,315 wanatarajiwa kupata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja katika mradi huu.
iii. Kuongeza matumizi ya TEHAMA na hivyo kutoa fursa kwa njia mpya za ubunifu za kuboresha utoaji huduma kama ilivyoelezwa katika Sura ya Pili, Ibara ya 61, Aya (l) ya Ilani ya Uchaguzi. Matumizi ya TEHAMA ili kuboresha utoaji huduma ni eneo la kipaumbele kwa Mfuko na limeainishwa katika moja ya malengo ya Mpango Mkakati wa Mfuko;
iv. Kuimarisha usimamizi wa uwekezaji na kuufanya uwekezaji unaofanywa na Mifuko ya Hifadhi ya jamii iwe na manufaa kwa wanachama wake kama ilivyoelezwa katika Sura ya Tatu, Ibara ya 130, Aya (p) ya Ilani ya Uchaguzi. Mkakati wa Uwekezaji wa Mfuko umetoa kipaumbele kwa uwekezaji ulio salama, faida na manufaa kwa jamii. Mfuko umewekeza katika miundombinu ya Daraja la Nyerere lililopo Kigamboni Dar es Salaam. Aidha, takribani ya nusu ya uwekezaji wa Mfuko upo kwenye dhamana za Serikali eneo ambalo ni salama, lenye faida kwa Mfuko na taifa kwa ujumla", alisema Mshomba, baada ya kueleza kwa kina Mpango Mkakati wa Mfuko huo wa NSSF.
Taarifa ya Msomba hiyo👇
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇