LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 15, 2023

NMB, SIMBA WAZINDUA UKARIBU WA NGUVU

 

 NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB na Klabu ya Simba, zimezindua ushirikiano wa kibiashara uliopewa jina la 'Ukaribu wa Nguvu,' lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika kufanya usajili wa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, ambayo Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wake, Imani Kajula, amesisitiza Ukaribu wa Nguvu unalenga pia kuwafanya wadau wa Simba washabikie timu yao kwa faida.

Ukaribu wa Nguvu ni mwamvuli unaojumuisha akaunti tatu za NMB Simba Account, NMB Simba Queens Account (Malkia - kwa wanawake) na NMB Simba Mtoto Account (kwa watoto), ambapo mashabiki na Wanachama wa Simba watajisajili kupitia mtandao mpana wa matawi 229 ya Benki hiyo, ambako watapewa kadi zenye Bima ya Maisha ya hadi Sh. Mil. 6.

Uzinduzi hu umefanyika Jumamosi hii kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam, ambalo licha ya Kajula, Simba iliwakilishwa pia na Mwenyekiti wake Murtaza Mangungu, huku NMB ikiwakilishwa na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi, Afisa Mkuu wa Biashara ya Kadi, Philbert Casmir na Mkuu wa Idara ya Mtandao wa Matawi, Donatus Richard.

Akizungumza katika uzinduzi huo mbele ya mamia ya mashabiki, wanachama na wapenzi wa Simba, Mponzi alisema ushirikiano huo baina ya taasisi hizo kubwa nchini, unaenda kunufaisha pande zote, hususani Wana Simba, ambao watahudumiwa na benki yake hiyo kupitia bidhaa zao, ikiwemo ya Mshiko Fasta - mikopo nafuu isiyo na masharti inayoanzia Sh. 1,000 hadi 500,000 kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo.

"Tuna mtandao mpana wa matawi, ambao tunaenda kuutumia kuwafikia Watanzania wote wanaoipenda Simba, ambao watapata kadi za NMB zenye logo ya Simba, ambazo watazitumia Kufanya miamala, sambamba na ofa za mapunguzo ya asilimia 10 na kuendelea watapolipia huduma kupitia kadi zao hizo.

"Mashabiki wajitokeze matawini kote nchini kuanzia leo kifungua akaunti zao na wale waliokuwa na akaunti za NMB hapo kabla, watabadilishiwa kadi zao na kupewa mpya zenye logo ya klabu yao pendwa.

"Tumejipanga kuhakikisha tunafanikisha mchakato huu, pamoja sajili za Wana Simba wote katika Wiki ya Simba (Simba Week) inayoanzia Agosti 1," alibainisha Mponzi na kuongeza ya kwamba makubaliano baina ya NMB na Simba yaneanda kuwapa faida kubwa mashabiki wa klabu hiyo aliyoipongeza kwa kushika nafasi ya Saba ya ubora Afrika.

Kwa upande kwake, Kajula alisema: "Mashabiki Simba wanapaswa kuwa ushabiko wa faida, ndiyo maana tumekuja na akaunti na kadi hizi, ambazo Mwanasimba atafungua akaunti kwa Sh. 5,000 na Akaunti zote zitaambatana na bima za maisha.

"Tumeingia nao mkataba, NMB kwa kuwa wana mawakala na matawi mengi nchini, wana zaidi ya mawakala elfu 20 nchini," alisema Kajula.

Naye Mangungu alisema: "Tumeingia mkataba wa ushirikiano na NMB ambapo ushirikiano huu kwa kiasi kikubwa ndiyo unatusaidia kuendesha timu, kusajili wachezaji wazuri na mengineyo. Kwa mashabiki wetu ambao walikuwa na kadi na taasisi nyingine ambazo tulikuwa tunashirikiana nazo huko nyuma tunawaomba wahamie NMB sasa."

Ikumbukwe kuwa Simba inakuwa klabu ya pili NMB kuingia nayo mkataba wa kutoa kadi za mashabiki baada ya hivi karibuni kuingia mkataba kama huo na mabingwa wa kihistoria wa soka la Tanzania, Yanga.

Katika hafla hiyo, Simba walimtambulisha winga wao mpya Mcameroon, Willy Essomba Onana aliyetua Msimbazi akitokea Rayon Sports ya Rwanda, ambapo pia walitanga tarehe za uzinduzi wa jezi mpya kuwa Julai 21 kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, pamoja na siku ya Tamasha la Simba Day, Agosti 6.




No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages