LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 16, 2023

WCF YASHIRIKI MAONESHO YA SABASABA KWA MAFANIKIO MAKUBWA

Na Mwandishi Maalum
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeshiriki kwenye Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara na Viwanda (Sabasaba) huku wadau wengi wakitembelea banda la WCF kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.

Akizungumza kuhusu Maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema wadau wengi walijitokeza kupata uelewa kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko.

"Wadau wengi wamejitokeza kutembelea banda letu kuanzia waajiri, waajiriwa na wananchi kwa ujumla jambo linaloonesha hamasa ya wadau kutaka kufahamu kuhusu haki yao ya fidia kisheria endapo wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi", alisema Dkt. Mduma na kuongeza:

"Kauli mbiu ya maonesho haya ni Tanzania - Mahali Sahihi kwa Uwekezaji na Biashara ambayo inaakisi malengo ya Mfuko ya kulinda nguvukazi ya Taifa na kuchochea tija kwa sekta za umma na binafsi kupitia uwekezaji na biashara. Tunajivunia kuwa moja ya Taasisi ambazo zinalenga kutimiza kwa vitendo kaulimbiu ya mwaka huu".

Dkt. Mduma anatanabaisha kuwa hadi sasa asilimia 86 ya huduma zote za WCF zinapatikana kwa njia ya mtandao hivyo kuwaondolea waajiri adha ya upotevu wa muda na kuwapa fursa ya kujikita katika uzalishaji mali.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la WCF mmoja wa wadau, Bi. Zakia Kimaro alisema amefurahishwa na uwepo wa WCF katika maonesho haya kwa sababu wananchi wengi wamepata fursa ya kujifunza huduma zitolewazo.

"Uwepo wa taasisi ya WCF unatupa nafasi ya kujifunza huduma ambazo ni haki yetu kisheria. Pia nitoe kongole kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma zake kwa njia ya mtandao. Taasisi nyingine za umma zinapaswa kujifunza kupitia WCF".

Maonesho ya Kimataifa ya Biashara na Viwanda yamefanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Juni 2023 hadi kufikia kilele tarehe 13 Julai 2023 ambapo Mgeni Rasmi katika Sherehe za ufungaji alikua ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Jamal Katundu (kushoto) akizungumza jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (katikati) na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Bi. Laura Kunenge alipofika kwenye banda la Mfuko huo wakati wa Maonesho ya Sabasaba yaliyokamilika Julai 13, 2023.

 

Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter (aliyesimama kushoto) akizungumza jambo mbele ya mteja (aliyekaa).

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria WCF, Bw. Abraham Siyovelwa (kushoto) akimpatia Elimu ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Mwananchi aliyetembelea kwenye banda la WCF.








 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages