
Mbunge Jimbo la Igunga Nicholaus Ngassa akizungumza na wananchi kwenye moja ya mikutano ya Hadhara anayoendelea kufanya jimboni hapo.
Na Odace Rwimo, Igunga.
MBUNGE wa Jimbo la Igunga Mkoani Tabora Mheshimiwa Nicholaus Ngassa amesema kuwa Kata 11 za maeneo ya mbugani katika jimbo hilo zitapatiwa huduma ya Mawasiliano ya a Simu kwa kujengwa Minara ya mawasiliano hivi karibuni na kutatua changamoto ya mawasiliano kwa wakazi wa maeneo hayo ambao ni wafugaji na wakulima wa mazao mbalimbali ya biashara na chakula.
Hayo ameyasema leo katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, mfuko wa jimbo na kwa nguvu za wadau, wananchi na yeye mwenye.
Mheshimiwa Ngassa alisema kuwa, Tarehe 13 Mei, 2023 Serikali imesaini Mikataba na Makampuni kwa ajili ya ujenzi wa Minara ya Mawasiliano ya Simu, ambapo halfa ya utiaji saini ilishuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
" Jimbo la Igunga Tumepatiwa Minara ya Mawasiliano ya simu itakayojengwa kwenye vijiji vyetu vilivyopo katika Kata ya Igurubi kijiji cha Kalangale, Kata ya Isakamaliwa maeneo ya katikati ya Hindishi na Isakamaliwa, Kata ya Itumba kijiji cha Itumba, Kata ya Itunduru eneo la Itunduru, Kata ya Bukoba kijiji cha Mangungu,"
" Kata ya Kining'inila maeneo ya katikati ya Iyogelo na Mwanyagula, Kata ya Kinungu eneo la Katikati Mwamagobo, Mwandinhimiji na Kinungu, Kata ya Mbutu katikati ya Mbutu na Mwabakima, Kata ya Mwamashimbabenei ni katikati ya Mwamashimba, Ijogoyha na Mwanyalali, Kata ya Nguvumoja katikati ya Nguvumoja na Mwanshoma na Kata ya Mtungulu maeneo ya Mtungulu," alisema Ngassa.
Katika hatua nyingine Mbunge Ngassa ameahidi kuweka umeme wa jua katika Zahanati ya Mwamashimba ili iweze kutoa huduma nyakati za usiku umeme unapokuwa umekatika, huku akiahidi kuendelea kutatua changamoto ya maji katika vijiji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.
"Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa Wananchi wa Jimbo la Igunga kwenye kuboresha Miundombinu ya kuichumi na huduma za kijamii, hivyo ninawaomba wananchi wa maeneo ya mbugani kutuamini kwani mpaka sasa tumeisha tekeleza miradi mingi ikiwemo shule hii ya Sekondiri iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 400.7, ujezi wa Zahanati ambazo sasa zinatoa huduma na zina vifaa tiba vya kutosha," alisema Ngassa.
Kwa upande wao Wananchi wa Kata hizo waliojitambulisha kwa majina ya Emmanuel Mandi, Esta Kasema na Mashala Zengo wamempongeza Mheshimiwa Ngassa kwa kutekeleza ahadi na ufuatiliaji wa miradi hiyo.
" Sisi tunampongeza Mbunge Ngassa na Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia kwa kuitekeleza vyema ilani ya chama na kutupatia miradi na kuisimamia kwa wakati, tumeona leo ametuhakikishia kupata minara ya simu, kumaliza tatizo la maji katika vijiji vilivyobakia ifikapo mpaka mwezi Desemba, ametuahidi kufuatilia barabara yetu kuu itokayo Shinyanga kuja Igunga kujengwa kwa lami" alisema Mandi.
" Mbunge Ngassa ni aina ya Mbunge tuliyekuwa tunaitaji katika jimbo la Igunga, anajitoa sana kufuatilia miradi ya maendeleo, ona leo anajenga ofisi za chama chake na leo ametoa mifuko 20 kwa kila kata alizopita, kwa kweli ni mtendakazi mzuri sana, " alisema Diwani wa Mwamashimba kutoka chama cha Chadema Andrew Lutuja.
Mbunge Ngassa anafanya ziara katika Kata nne katika jimbo la Igungu ambapo ameanza Jana 19.05.2023 na anatarajia kumaliza ziara yake kesho Jumapili tarehe 21.05.2023 ikiwa na lengo ka kukagua miradi ya maendeleo inayojengwa na serikali ya awamu ya sita chini ya usimamizi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇