LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 3, 2023

DKT MPANGO AWATAKA WATANZANIA WAISHIO UGHAIBUNI KUITANGA VYEMA TANZANIA

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango tarehe 02 Machi 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na watanzania waishio nchini Azerbaijan, Mazungumzo yaliofanyika katika Jiji la Baku nchini humo.


Akizungumza na Watanzania hao, Makamu wa Rais amewaasa watanzania hao kuendelea kuitangaza vema Tanzania na vivutio vyake vilivyopo,kutangaza lugha ya
Kiswahili na kuendelea kueneza utamaduni wa Tanzania pamoja na kuwa wazalendo kwa nchi yao.

 Pia amewaagiza kutoa elimu kwa watanzania wengine juu ya fursa za elimu zilizopo katika jumuiya yan chi wanachama zisizofungamana na upande
wowote.

Makamu wa Rais amewataka watanzania waishio nje ya Tanzania kufuata sheria na taratibu za nchi walizopo pamoja na kujifunza mazuri katika nchi hizo na kuhamishia
maarifa hayo nchini Tanzania. 

Pia amewaasa kutambua jukumu la kwanza la ujenzi wa Tanzania litafanywa na watanzania wenyewe hivyo wanapaswa kutoa mchango
wa kila hali katika kuliletea taifa maendeleo.

Amesema serikali itaendelea kuleta mabadiliko yenye tija kwa watanzania wote
ikiwemo kuendelea na jitihada za kuboresha sekta mbalimbali kama vile Afya, Elimu
na Miundombinu pamoja na hivi sasa kuanzisha programu maalum ya kilimo ya
Building Better Tomorrow itakayowasaidia vijana katika sekta hiyo.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Urusi Mheshimiwa
Fredrick Kibuta.

Makamu wa Rais yupo nchini Azerbaijan kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Nchi
Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Aligned Movement) unaojadili kuhusu
namna ya kukabiliana na athari za Uviko-19.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akifanya
mazungumzo na mazungumzo na watanzania waishio nchini Azerbaijan,
Mazungumzo yaliofanyika katika Jiji la Baku nchini humo leo tarehe 02 Machi 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Urusi Mheshimiwa Fredrick Kibuta katika picha ya pamoja na baadhi watanzania waishio nchini Azerbaijan mara baada ya
mazungumzo yaliofanyika katika Jiji la Baku nchini humo  tarehe 02 Machi 2023.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages