LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 3, 2023

DC MPOGOLO AWAFUNDA VIONGOZI JIMBO LA SEGEREA JUU YA UHUSIANO WA SIASA, SERIKALI NA WANANCHI KATIKA KUTATUA KERO ZA WANANCHI

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam,  Edward Mpogolo, amewataka Viongozi wa ngazi zote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wa Serikali kufanyakazi kwa mshikamano mkubwa, na kuonya kuwa bila kufanya hivyo shida walizonazo wananchi hazitaweza kutatuliwa.

Amesema, ulazima wa viongozi hao kushirikiana upo kwa sababu, wa CCM na wa Serikali wote wajibu wao wa kwanza ni kushughulikia shida au changamoto za wananchi, na kimsingi zile shida zinazokuwa zinashughulikiwa na kiongozi wa CCM na zinazoshughulikiwa na yule wa Serikali zote ni za aina moja.

DC Mpogolo ameyasema hayo,leo, wakati akizungumza na viongozi wa CCM na wa Serikali kutoka Kata saba zilizomo katika Jimbo la Segerea, kujitambulisha kwao na kuwapa semina maalum, kwa lengo la kuwapanua uelewa juu ya Uhusiano ulipo kati ya Chama, Serikali Kuu, Kata, Mitaa na Wananchi.

Alisema, katika ushirikiano huo, kiongozi wa Serikali hapaswi kudhani kuwa shughuli zinazofanywa na kiongozi wa Chama kuhudumia wananchi hazimhusu au yule wa Chama kudhani shughuli zinazofanywa na kiongozi wa serikali kuhudumia wananchi hazimhusu.

"Nataka niwaambieni, uhusiano ulipo katika ya Serikali Kuu na hizi za chini na wananchi ni kwamba msingi wa uhusiano huu ni Wananchi, maana hakuna kiongozi ambaye anapatikana bila maamuzi ya mwananchi.

Tazama, ili Chama kishike dola, kinaingia katika Uchaguzi, katika uchaguzi huo watu ndiyo wanakipa ridhaa ya kukifanya kiunde Serikali, sasa Chama kikishaunda Serikali maana yake ni kwamba wewe kiongozi wa Serikali usingepatikana kama Wananchi wasingechangua Chama.

Kwa hiyo hapo maana yake ni kwamba hakuna kiongozi wa Serikali ambaye ataacha kujali shida za watu wakati ametokana na  Chama ambacho kimepewa nafasi na watu, na hata kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Wananchi ndiyo msingi wa Mamlaka", akasema DC Mpogolo.

"Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana ukiwepo mkutano wa Chama wa kikatiba, wanashirikishwa viongozi wa kiserikali katika ngazi husika ambao wanatambuliwa na vikao husika kikatiba ya Chama, na vilevile katika Vikao vya Kiuongozi wa Serikali wapo viongozi wa Chama ambao hushiriki kwa mujibu wa utaratibu.

Na utaratibu huu unafanyika kwa sababu ya kutaka Viongozi wa Serikali na wa Chama wapate fursa ya kujadili kwa pamoja changamoto zinazowakabili wananchi, kwa kuwa wanapozijadili kwa pamoja ndiyo ufumbuzi unapatikana", akasema DC Mpogolo.

Akasema, kwa hiyo ili viongozi washiriki vema katika vikao hivyo mtambuka ni lazima kila kiongozi kwa pande zote, kuhakikisha anashiriki kwanza kikamilifu katika vikao vinavyohusu upande wake kujadili changamoto za wananchi, asipofanya hivyo maana yake akienda kwenye vikao mtambuka atakuwa hana ajenda zinazohusu wananchi bali ataenda na ajenda zake binafsi.

Unakuta kiongozi wa Chama, mkewe amenyang'awa eneo la biashara na kiongozi wa Serikali pengine kwa mujibu wa sheria, sasa kwa kuwa kiongozi huyo wa Chama hashiriki vikao vya Chama vinavyomhusu, akienda kwenye vikao mtambuka anaingia na ajenda ya mkewe kunyang'anywa eneo la biashara, wakati hiyo siyo ajenda ya wananchi.

"Sasa hali hii ya kukiuka mfumo ikiendelea inaleta matokeo mabaya hadi kwenye ngazi za juu za maamuzi, maana ngazi hiyo ya juu, inakuwa imefikishiwa ajenda ambazo si za wananchi, kwa hiyo matokeo yake miradi inakwama, wananchi hawapati maendeleo, na kubaki wanamlaumu mtendaji wa mwisho, yaani Rais wa Nchi kwa hafai.

Kwa hiyo tafadhalini sana, fanyeni kazi kwa kushirikiana viongozi wote, tufanye kazi kwa mshikamano na alama ya mshikamano ni maendeleo ya wananchi, msipofuata mfumo huu mnaumiza wananchi", akasema DC Mpogolo.

Baadaye DC Mpogolo alitoa nafasi kwa Wawakilishi kutoka Benki ya CRDB na Takukuru kuzungumza na kisha wakapewa nafasi madiwanin na baadhi ya wajumbe wa mkutano huo kueleza kero kwa niaba ya wananchi, ambapo akijibu alisema, atazifanyia kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo akizungumza na viongozi wa CCM na wa Serikali kutoka Kata saba zilizomo katika Jimbo la Segerea, kujitambulisha kwao na kuwapa semina maalum, kwa lengo la kuwapanua uelewa juu ya Uhusiano ulipo kati ya Chama, Serikali Kuu, Kata, Mitaa na Wananchi, Kikao hicho kimefanyika leo katika Ukumbi wa GBF kata ya Liwiti. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Charangwa Makwiro na kulia ni Diwani wa Kata ya Liwiti Alice Mwangomo.
Wajumbe wakiwa kwenye Kikaosemina hicho.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages