WAUMINI SAFARI ZA IBADA YA HIJA ZAANZA
Na HEMEDI MUNGA
BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limezindua safari
za ibada za Hija kwa mwaka 1444 hijiria sawa na mwaka 2023 miladia huku taasisi
15 zakidhi vigezo kati ya taasisi 18 ziliotuma maombi ya kutoa huduma hiyo.
Aidha, limesema watu wenye umri wa miaka 65
waliokuwa wameziwiliwa kuingia Makka kwa lengo la kutekeleza ibada hiyo sasa
wanaruhusiwa hata kwa muumini aliyekuwa na miaka 100.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika uzinduzi
huo leo, jijini Dar es Salaam, Mratibu wa ofisi ya Hija Tanzania Bara (BIITHA),
Shekhe Mussa Hemed alisema wanazindua msimu kwa lengo la kuwataka waumini
kufanya maandalizi ya kutekeleza ibada hiyo mapema.
‘’Kuwahi kufuata taratibu ni vyema na kuchelewa
kukamilisha taratibu za kutekeleza ibada ya hija inaweza kuwa kikwazo cha
kuwafanya waumini kuziwiliwa kwenda hija.
Ninaomba kuupa umma wa kiislamu taarifa kuwa leo
tumezindua rasmi shughuli za maandalizi ya hija kwa mwaka 2023, ‘’ alisema.
Aidha, taasisi hiyo ilipokea maombi ya taasisi 18
ambazo zimekusudia kusafirisha mahujaji kwa mwaka huu, hivyo taasisi zilizokidhi
vigezo ni 15.
Shekhe Hemed alifafanua vigezo vinavohitajika kwa
taasisi kukidhi sifa ya kutoa huduma hiyo kuwa ni kusajiliwa serikalini katika
wizara ya mambo ya ndani na RITA, iwe na ofisi, iweimelipa dhamana ya benki, iweimelipa
ada ya mwaka katika ofisi ya uratibu na iweimelipa ada ya Haji.
‘’Haya ni masharti muhimu kwa mmiliki wa taasisi
kwa lengo la taasisi yake kuthibitishwa na kuruhusiwa kutoa huduma ya
kusafirisha mahujaji,’’alisema.
Hatahivyo, Shekhe Hemed alitoa wito kwa wamiliki wa
taasisi hizo kuwahamasisha waumini kutekeleza ibada hiyo ya hija kwa sababu
idadi ya mahujaji inayoruhusiwa Tananzia na serikali ya Saudiarabia ni mahujaji
25,000 huku wanaodaiwa kuomba katika kota hiyo kuwa ni mahujaji 3500 ambayo ni
idadi ndogo sana.
‘’Nimatumaini ya taasisi hii kuwa taasisi
zilizokidhi vigezo zitahamasisha waislamu kwenda kutekeleza ibada
hii,’’alisema.
Aidha, aliwataka waumini wanaokusudia kutekeleza
ibada hiyo kuanza kujiandikisha mapema kwa sababu taratibu za hija kwa
kuzingatia mikataba iliyokubaliana kati ya Tanzania na Saudiarabia kuwa mwisho
wa kukamilisha shughuli za maandilizi ya hija kwa mwaka huu ni tarehe 15 mfungo
mosi.
‘’Kuchelewa kujiandikisha na kulipia kunaweza kusababisha
kushindwa kusafiri,’’ alisisitiza.
Hata hivyo, Shekhe Hemed aliwatahadharisha waumini
wanaokusudia kutekeleza ibada hiyo kuchanja kwa kuwa ni takwa la kisheria na
hata dini nayo inahimiza waumini kutosababisha madhara kwa watu wengine.
Alisema katika ibada ya hija huwa kunachanzo za
ziada kwa sababu ya mkusanyiko mkubwa wa watu, hivyo kuna chanjo ya homa ya uti
wa mgongo, kuna chanjo ya ini, chanjo ya homa ya manjano, chanjo ya
kipindupindu na chanjo COVID 19.
‘’Kwa kweli tunawasisitiza mahujaji wetu watarajiwa
wahakikishe wanachanja kwa sababu ya kulinda afya zao na kuzuwia madhara kwa
jamii,’’ alisema.
Ibada ya hija ni moja kati ya nguzo tano za uislamu
ambapo Qur’ ani Tukufu inasema kuwa waislamu wenye uwezo wa kimwili na kifedha
wanapaswa kuhiji mara moja katika maisha yao.
Mahujaji husafiri kwenda makka kutoka ulimwenguni
kote kwa siku tano za kutekeleza ibada hiyo.
Waislamu hutekeleza ibada hiyo kwa namna ambavyo
alivyotekeleza Mtume Muhammad (SAW) karibu miaka 1,400 iliyopita na inaaminika
ibada ya Hija ya sasa inafuata nyayo za Manabii Ibrahim na Ismaili amani ya Mungu
iwe juu yao.
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kupitia Mratibu
wa Ofisi ya Hija Tanzania Bara (BIITHA), Shekhe Mussa Hemed kushoto akizindua
rasmi safari za ibada ya hija leo. (Picha na Hemedi Munga)
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kupitia
Mratibu wa Ofisi ya Hija Tanzania Bara (BIITHA), Shekhe Mussa Hemed akikabidhi
cheti kwa Shekhe Omar Mohammed wa Taasisi ya Baraza Kuu la Waislamu kulia kwa kukidhi
sifa za kusafiririsha Mahujaji rasmi katika safari za ibada ya hija leo.(Picha
na Hemedi Munga)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇