Katika kuendeleza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya Viwanda, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Albert Chalamila amewataka baadhi ya viongozi na wananchi kutokuwakwamisha wawekezaji na kuwakemea kuacha tabia hiyo kwani inakwamisha uchumi na maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza mara baada ya kukagua shughuli za uzalishaji kiwanda cha kahawa cha Source of The Nile Commodities kilichopo Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera wakati wa ziara yake ya kukagua miradi na shughuli za maendeleo Wilayani humo, Mhe. Chalamila ameeleza kuwa zipo tabia za baadhi ya watu si nzuri kwa ustawi wa uchumi wa Taifa letu za kuwawekea vikwazo wawekezaji hali ambayo inawakatisha tamaa na kufanya wasiendelee na nia ya uwekezaji ndani ya Mkoa na hata Taifa letu.
“Ukiona una wawekezaji wa hivi katika Wilaya zetu maana yake ni kiashiria cha kukua kwa uchumi wa Mkoa wetu.Mna kiwanda chenye uchumi endelevu, uchumi endelevu ni jambo la muhimu katika suala la maendeleo.
"Huwezi kusema unabadili uchumi kama hujaubadili kuwa uchumi endelevu, ishara ya kuwa na uendelevu ni kuwa na kitu leo,kesho na keshokutwa,” ameeleza Mhe. Chalamila.
Sambamba na hayo ameshauri juu ya kutokimbilia kutafuta kodi kwa wawekezaji bali kufanya tathmini ya faida ya uwekezaji hususani kwa jamii.Huku akieleza baadhi ya faida za uwekezaji zikiwemo ajira kwa jamii, mapato kwa Serikali na maendeleo kwa ujumla hivyo ni vema kuwalinda wawekezaji na si kuwakatisha tamaa.
Aidha,amewashukuru wawekezaji wenye moyo walioamua na wanaoendelea kuja kuwekeza Mkoani Kagera na kuwasihi wazawa ambao wako nje ya Mkoa na nje ya Nchi wenye uwezo wa kuwekeza kuja kuwekeza ikiwa ni kurudisha fadhila kwa jamii yao.
Kwa upande wake mmiliki wa kiwanda hicho Ndg. Leonard Kachebonaho ameeleza kuwa mpango wa kiwanda ni kuwezesha wakulima wa kahawa na vanilla kupitia AMCOS zao kwa kuwajengea stadi za kuboresha kilimo na kuendesha shughuli za kilimo.
Kuhamasisha na kuongeza kasi ya upandaji na utunzaji wa zao la kahawa na miti ya matunda ikiwemo parachichi na kuwezesha AMCOS kuwa na mipango mikakati itakayosaidia vyama kupata huduma za kifedha moja kwa moja kutoka taasisi za kifedha.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇