LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 11, 2022

WAZIRI MKUU AAHIRISHA BUNGE LEO, ASEMA RAIS SAMIA AMERIDHIA 28,000 WAENDELEE NA USAJILI VYUONI, AZUNGUMZIA HALI YA CHAKULA NCHINI

Bungeni, Dodoma
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.

“Lengo la Mheshimiwa Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” amesema.

Ametoa kauli hiyo Bungeni leo (Ijumaa, Novemba 11, 2022) wakati akiahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 12, jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Januari 31, mwakani.

Waziri Mkuu amewashukuru Wabunge kwa kuibua hoja zenye lengo la kuboresha utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na mfumo mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Amesema miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa hisia na kupewa uzito mkubwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mkutano huo ni hoja ya ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. “Nyote mtakubaliana nami kwamba lengo la mjadala huo, lilikuwa ni kutafuta suluhu ya suala la wanafunzi takribani 28,000 wenye uhitaji wa kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 ambao walikuwa hawajapangiwa mikopo, kutokana na ukomo wa kibajeti,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hadi sasa taasisi za umma 455 zimeunganishwa na zinatumia mfumo mpya wa taarifa za kiutumishi na mishahara ili kupunguza muda wa kuchakata malipo ya mishahara kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na kuwa na taarifa sahihi za watumishi wanaotarajia kustaafu.

Akizungumzia utendaji kazi na uwajibikaji wa watumishi wa umma, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuboresha, kuimarisha na kuweka mifumo imara ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utendaji kazi wa watumishi wa umma na taasisi za umma ili kuhakikisha kuwa mifumo iliyopo na inayojengwa inasaidia kuharakisha utendaji kazi na usimamizi wa watumishi na inakuwa na taarifa sahihi kwa lengo la kuongeza tija na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amesema mfumo huo mpya ambao ulianza kutumika rasmi Mei 2021, umeunganishwa na mfumo wa PSSSF kwa ajili ya kubadilishana taarifa za michango ya watumishi na nyaraka za hitimisho la ajira; mfumo wa mikopo ya elimu ya juu (HESLB) kwa ajili ya kubadilishana taarifa za mikopo ya elimu ya juu kwa watumishi; mfumo wa ajira portal kwa ajili ya kubadilishana taarifa za waajiriwa wapya na mfumo wa NIDA kwa ajili ya kubadilishana taarifa za utambulisho wa Taifa wa watumishi.

Ameitaja mifumo mingine iliyojengwa kwa lengo la kukabiliana na changamoto za upimaji wa utendaji kazi wa watumishi na mikataba ya utendaji kazi ya taasisi kuwa ni Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Watumishi wa Umma (PEPMIS) na Mfumo wa Kusimamia Utendaji Kazi wa Taasisi za Umma (PIPMIS).

“Ujenzi wa mifumo hiyo mipya umekamilika. Hivi sasa inafanyiwa majaribio na inatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa majaribio na kutoa mafunzo kwa watumishi katika taasisi zote za umma,” amesema.

Amesema hatua ya mifumo hiyo kuwa ya kielektroniki itaondoa muhali, hisia za kupendeleana au kuoneana katika usimamizi wa utendaji kazi na itahamasisha uwajibikaji wa hiari wa watumishi wa umma itakayosaidia utoaji huduma bora na kwa wakati kwa umma wa Watanzania.

Pia Waziri Mkuu amezungumzia hali ya Chakula Nchini na kusema,  katika kukabiliana na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza kwa baadhi ya maeneo nchini, Serikali inawataka wananchi waendelee kutumia chakula kilichopo sasa kwa uangalifu na waepuke matumizi mabaya ya chakula au yasiyokuwa ya lazima kama vile utengenezaji wa pombe na matumizi ya chakula katika sherehe zisizo za lazima.

Amesema katika kukabiliana na hali ya ukame na kuchelewa kuanza kwa mvua za msimu 2022/2023, wakulima waendelee kutumia mbinu bora na walime mazao yenye kuhimili ukame.

Pia, Waziri Mkuu amesema wakulima waendeleze kilimo kinachohimili ukame na chenye ufanisi mkubwa ikiwemo matumizi ya mbolea za mboji, samadi, kilimo cha matandazo ambacho huimarisha uhifadhi wa maji na unyevunyevu kwenye udongo; kupanda mbegu za mazao ya chakula yanayokomaa kwa muda mfupi na kutumia maji vizuri kwenye skimu za umwagiliaji.

“Maafisa ugani endeleeni kushirikiana na vituo vya utafiti vilivyopo kwenye maeneo yenu kwa lengo la kupata na kusambaza teknolojia za uzalishaji wa mazao, kufuatilia kwa karibu taarifa za mara kwa mara kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ili kuwa na wigo mpana wa kuwashauri wakulima kuhusiana na hali ya hewa na kilimo kwa wakati.”

Akizungumzia kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula, Waziri Mkuu amesema mwezi Juni hadi Julai 2022, Serikali ilifanya tathmini ya awali ambayo ilionesha kuwa, uzalishaji wa mazao ya chakula unatarajiwa kufikia kiasi cha tani 17,403,880. Mahitaji yote ya chakula kwa mwaka 2022/2023 ni kiasi cha tani 15,073,855. Kwa kulinganisha uzalishaji na mahitaji, nchi inatarajiwa kuwa na kiwango cha utoshelevu wa kiasi cha asilimia 115.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema mwezi Oktoba, 2022 Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilifanya Tathmini ya Kina ya Hali ya Upatikanaji wa chakula kwa ngazi ya kaya katika maeneo ambayo yalibainika kuwa na upungufu wa uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu 2021/2022.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana na matokeo ya tathmni hiyo, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imetenga jumla ya tani 4,572,300 za chakula kwa ajili ya kupelekwa kwenye maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa chakula.

Amesema hadi kufikia mwezi Oktoba, 2022 jumla ya Halmashauri 20 zimepelekewa chakula kama ifuatavyo: Liwale (tani 200), Nachingwea (tani 100), Bunda (tani 400), Geita TC (tani 100), Nzega (tani 300), Sengerema (tani 300), Monduli (tani 100).

Halmashauri nyingine ni Ngorongoro (tani 100), Butiama (tani 100), Meatu (tani 100) Kishapu (tani100), Longido (tani 1,872), Urambo (tani100), Handeni (tani 100), Mkinga (tani 100), Chemba (tani (100), Chamwino (tani 100), Mbulu (tani 100), Mwanga (tani 100) na Hai (tani 100).

Mheshimiwa Majaliwa amesema pamoja na hatua hizo, Serikali inaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu wa hali ya upatikanaji wa chakula hususan mazao ya nafaka na kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kupeleka chakula kutoka Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kitakachouzwa kwa bei ya chini ya bei ya soko.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Novemba, 2022 unyeshaji wa mvua katika maeneo mengi yanayopata mvua hizo hasa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro na Manyara ni wa kusuasua. Kwa upande wa mikoa ya Kagera, Geita, Mara na Mwanza, mvua za vuli zinaendelea kunyesha na mazao ya chakula shambani yapo katika hatua mbalimbali za ukuaji.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma, November 11, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages