LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 25, 2022

TUKO TAYARI KWA MJADALA WA KITAIFA KUHUSU MAPENDEKEZO YA SERA YA ELIMU NA MITAALA - PROF.MKENDA






Na WyEST
Mwanza 

Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu Msingi yamekamilika na yanasubiri mchakato wa ndani ya Serikali ili kupata ridhaa ya rasimu zilizoandaliwa  kupelekwa kwa wadau kwa mjadala wa kitaifa.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Adolf  Mkenda wakati akizungumza katika Mahafali ya 41 ya Chuo Kikuu Huria Jijini Mwanza, ambapo amesema kuna mambo makubwa ambayo yamependekezwa na wadau mbalimbali.

Prof. Mkenda  amefafanua kuwa  utekelezaji wa kazi hiyo umeendelea kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Maaskofu, Mashekhe, walimu, wenye shule binafsi pamoja na wataalamu kutoka nje ya nchi ili kupata uzoefu kutoka katika nchi zilizoleta mageuzi ya elimu na kufanikiwa na zile ambazo hazikufanikiwa. 

"Tumekamilisha rasimu ya mapitio ya Sera, ina mapendekezo mengi makubwa, tunachosubiri sasa ni mchakato wa ndani wa kupitia mapendekezo hayo kabla hatuyatangaza rasmi kwa ajili ya mdahalo wa kitaifa na hatimae mchakato wa maamuzi uweze kufikiwa ndani ya Serikali," amesema Prof. Mkenda.

Akitolea mfano jambo moja ambalo limeguswa katika mapitio ya Sera ni suala la walimu  kupewa kipaumbele katika ubora na suala la mafunzo endelevu kazini ambalo hata sasa suala hilo la mafunzo kazini limeshaanza na linaendelea.    

"Katika mapitio ya Sera walimu waliopo wataendelea kupewa mafunzo kazini, ambayo tayari wameshaanza kuyapata na walimu wapya tutaona vigezo katika mapitio ya Sera kuhakikisha tunakuwa na walimu bora wa kuendeleza elimu yetu," amefafanua Prof. Mkenda.

Aliongeza kuwa kazi ya kupitia mitaala nayo inakwenda vizuri  pamoja na kuwa kwa kawaida hapa nchini kazi hiyo ilikuwa hailepelekwi katika ngazi ya maamuzi kutokana na kuwa ni kazi ya kitaalamu zaidi, lakini kwa mageuzi haya ya elimu italetwa kwenye ngazi za juu na kisha kujadiliwa na umma wa Watanzania.

Ameongeza kuwa mageuzi hayo ya mitaala yatafanyika pia katika ngazi ya  Elimu ya Juu ambapo huko utaangaliwa zaidi ubora wa elimu.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages