Mkutano wa Tano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (The 5th Joint-Permanent Commission For Cooperation - JPCC) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi umeanza leo Oktoba 26, 2022 jijini Dar es Salam.
Mkutano huu wa siku tatu, kuanzia tarehe 26 – 28 Oktoba 2022, utafanyika katika ngazi ya Wataalamu Waandamizi tarehe 26 Oktoba 2022, Makatibu Wakuu tarehe 27 Oktoba 2022, na kuhitimishwa na Mawaziri tarehe 28 Oktoba 2022.
Agenda za mkutano huu zinaangazia masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili ikiwemo biashara, uwekezaji, utalii, kilimo, afya, ulinzi na usalama, usafirishaji, sekta ya mafuta, maliasili, masuala ya utafiti na Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Vilevile Mkutano huu utajadili namna ya kuondoa vikwazo vya kibiashara visivyo vya forodha ili kurahisisha ufanyaji wa biashara baina ya mataifa haya mawili.
Akifungua Mkutano huo katika ngazi ya Wataalamu Waandamizi, Balozi Joseph Sokoine Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ameeleza mkutano huo ni kielelezo tosha kuwa Serikali za pande zote mbili zinaendelea kutambua na kuthamini umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na karibu zaidi ili kuchochea maendeleo ya shughuli mbalimbali za kijamii na uchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.
Aidha Balozi Sokoine ametoa rai kwa wataalamu waandamizi wa pande zote mbili kuhakikisha kuwa wanatumia mkutano huo kujadili na kuweka mikakati madhubuti ili kutengeneza mazingira wezeshi kwa mataifa hayo mawili yenye utajiri wa fursa na rasilimali, kuweza kuchochea kasi ya maendeleo siyo tu kwa faida ya mataifa hayo mawili bali kwa faida ya kikanda na kimataifa kwa ujumla
“Sote tunatambua kuwa mataifa yetu yameendelea kufarahia ushirikiano mzuri uliopo baina yetu ambao kwa kiasi kikubwa umechangiwa na mifumo mizuri ya kisheria inayotuwezesha kukutana na kujadili masuala yanayotuhusu mara kwa mara. Natoa rai kwenu kutumia mkutano huu vyema katika kujadili kwa kina kuhusu masuala muhimu kwa maslahi na maendeleo ya pande zote mbili” alisema Balozi Sokoine.
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiendelea kuendesha programu na kuchukua hatua mbalimbali katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi sambamba na kudumisha Uhusiano wa Kidiplomasia na Mataifa mbalimba duniani.
Kwa upande wa Malawi, Ubalozi wa Tanzania nchini humo chini ya Mhe. Balozi Humphrey Polepole sambamba na kuendelea dumisha Uhusiano wa Kidiplomasia umekuwa ukiendelea na utekelezaji wa mikakati inayoliwezesha Taifa kunufaika na fursa za kiuchumi zinazopatikana nchini humo.
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), biashara kati ya Tanzania na Malawi imeendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 138.12 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 186.1 mwaka 2019. Kutokana na janga la UVIKO-19 mwaka 2020, biashara ilipungua na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 159.4. Hata hivyo mwaka 2021 biashara iliongezeka tena hadi kufikia shilingi milioni 198.3.
Ujumbe wa Malawi katika Mkutano huo umeongozwa na Bw. William Kantayeni ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Afrika na Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchini humo.
Your Ad Spot
Oct 26, 2022
Home
featured
Habari
MKUTANO WA TANZANA NA MALAWI KUJADILI MASUALA YA USHIRIKIANO WAANZA LEO JIJINI DAR ES SALAAM
MKUTANO WA TANZANA NA MALAWI KUJADILI MASUALA YA USHIRIKIANO WAANZA LEO JIJINI DAR ES SALAAM
Tags
featured#
Habari#
Share This
About Bashir Nkoromo
Habari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇