Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Umoja
wa Ulaya (EU) umeipatia Tanzania msaada wa euro milioni 166 sawa na
takribani shilingi za Tanzania bilioni 380 ajili ya utekelezaji wa
miradi mitatu ikiwemo kuibua fursa zitokanazo na bahari (Uchumi wa Buluu), sekta Jumuishi ya fedha na kuimarisha ushirikiano.
Msaada
huo umetangazwa leo tarehe 26 Oktoba, 2022 Jijini Dar es Salaam mbele
ya wanahabari na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya
Ulaya Mhe. Jutta Urpilainen na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Mwigulu Lameck Nchemba.
Dkt.
Nchemba alisema kuwa msaada huo umeidhinishwa na Umoja wa Ulaya katika
mwaka wa pili wa utekelezaji wa ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa
Ulaya kwa kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka 2021 hadi 2027, ambapo
katika awamu ya kwanza, tarehe 22 Machi, 2022, Serikali ilipokea msaada
wa euro milioni 180, sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 400.
Alifafanua
kuwa katika awamu hiyo ya pili ya msaada wa euro milioni 166, mradi wa
uchumi wa buluu umetengewa euro milioni 110, mradiwa kuimarisha sekta ya
fedha (euro milioni 50) na mradi wa kuimarisha ushirikiano umetengewa
euro milioni 6.
“Fedha
hizi ni sehemu ya matokeo ya ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan,
iliyofanyika mwezi Februari, 2022 jijini Brussels, nchini Ubelgiji
ambapo Umoja huo ulitangaza kuipatia Tanzania msaada wa kiasi cha euro
milioni 426 kwa kipindi cha miaka minne ijayo kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini” alisema Dkt. Nchemba
Dkt.
Nchemba aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada huo mkubwa ambao ameahidi
kuwa miradi itakayonufaika na fedha hizo itatekelezwa kwa viwango na
kama ilivyokusudiwa kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa
haraka.
Alisema
Tanzania inathamini kwa kiwango kikubwa ushirikiano uliopo kati yake na
Umoja wa Ulaya tangu uanzishwe mwaka 1975 ambapo hadi sasa Umoja huo
umetoa misaada na mikopo yenye thamani ya euro bilioni 2.4 sawa na
takribani shilingi trilioni 5.9 na mikopo yenye masharti nafuu yenye
thamani ya euro milioni 270.9 sawa na shilingi bilioni 706.5.
Kwa
upande wake, Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya
Ulaya, Mhe. Jutta Urpilainen, alisema Tanzania ni mshirika muhimu wa
Umoja wa Ulaya ikiwa ni nguzo imara inayounganisha Mashariki na Kusini
mwa Afrika na na kuipongeza kwa kujiimarisha katika nafasi ya uchumi wa
kati.
kuwa
Umoja huo unafurahishwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliyofikiwa
nchini na kwamba wako tayari kuendelea kutoa misaada ili kufanikisha
agenda hiyo.
Alisema
kuwa msaada huo wa euro milioni 166 umelenga kuimarisha shughuli za
uchumi wa buluu uliolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na
kuvumbua fursa za kiuchumi zinazopatikana kupitia bahari ili taifa na
jamii inayozunguka fukwe za bahari iweze kunufaika kupitia uvuvi, utalii
wa kiikolojia, huku ikihifadhi mazingira na kukuza ajira.
Alisema
manufaa mengine ya mpango huo ni kuiwezesha jamii kuzifikia fursa za
kiuchumi kupitia taasisi za fedha, uwekezaji wenye lengo la kuchochea
mapinduzi ya kilimo, uchumi jumuishi na maendeleo endelevu nchini
Tanzania, kuboresha ujuzi wa wananchi na kuboresha mazingira ya sheria
mbalimbali.
“Msaada
huo umelenga kutekeleza mkakati wa Umoja wa Ulaya ujulikanao kama The
Global getway, wenye lengo la kuboresha mifumo ya kidijitali, mabadiliko
ya tabianchi, afya, elimu, miundombinu ya usafiri na masuala ya utafiti
kwa kuzishirikisha sekta ya umma na sekta binafsi nchini Tanzania”
alisema Mhe. Urpilainen
“Watekelezaji
wa miradi hii watafanyakazi bega kwa bega na Serikali kutekeleza
malengo hayo kwa kutumia misaada ya fedha kutoka Umoja wa Ulaya ili
kuongeza uwekezaji zaidi hapa nchini” aliongeza Mhe. Urpilainen.
Kamishna
wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya, Mhe. Jutta
Urpilainen, yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na baadae
ataelekea nchini Malawi kwa ziara kama hiyo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiteta
jambo na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya Bi.
Jutta Urpilainen, baadaa ya kuzindua mpango wa pili wa msaada wa Umoja
wa Ulaya kwa Tanzania wenye thamani ya euro milioni 166 sawa na shilingi
bilioni 380 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,
Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇