LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 29, 2022

BODI YA MICHEZO YA KUBAHATISHA YATEKETEZA MASHINE HARAMU 300 ZA MICHEZO HIYO (SLOT MACHINES), WANANE MATATANI.

Na Mwandishi Maalum, Kisarawe
Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (Gaming Board of Tanzania-GBT) imeteketeza mashine haramu za kuendeshea michezo ya kubahatisha (Slot Machines) zipatazo 300, huku watu Wanane wakiwa mikoni mwa vyombo vya kisheria kuhusiana na mashine hizo.

Zoezi hilo lililoongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa GBT Bw. James Mbalwe limefanyika jana Oktoba 28, 2022 kwenye eneo la kuteketeza vifaa vya kielektroniki lililoko Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani.

“Katika jitihada za kudhibiti waendeshaji haramu wa michezo ya kubahatisha GBT iliendesha operesheni maalum kwenye mikoa ya Pwani, Lindi, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Morogoro, Manyara na Songwe na kufanikiwa kukamata mashine hizo zenye thamani ya shilingi Milioni 300.” Alifafanua Bw. Mbalwe.

Alisema mashine hizo zilikamatwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kufanya biashara bila ya Leseni ya GBT, mashine kuingizwa nchini bila ya kufuata taratibu za kisheria, kufanya biashara kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi au hayajakaguliwa na kuthibitishwa na Bodi (GBT) pamoja na  kukwepa kulipa kodi na tozo mbalimbali.

“Mashine hizi pekee zimepelekea serikali kukosa mapato yake kiasi cha shilingi Milioni 33 kwa mwezi sawa na shilingi Milioni 400 kwa mwaka, jambo hili halikubaliki.” Alisisitiza.

Pia Bw. Mbalwe alisema waendeshaji hao haramu ndio ambao wamekuwa wakiruhusu watu wenye umri usioruhusiwa kucheza michezo hiyo,

“Operesheni hii ni endelevu na itakuwa ikifanyika mara kwa mara ili kudhibiti vitendo hivyo na kuhakikisha michezo ya kubahatisha inaendeshwa kwa kuzingatia misingi ya kisheria na kuleta tija katika maendeleo ya Taifa letu bila ya kusababisha athari hasi au madhara yoyote kwa jamii yetu.” Alisema Bw. Mbalwe.

Aidha Mkurugenzi Mkuu huyo aligusia pia hatua ya hivi karibuni ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Yasinta Mboneko ya kuzuia biashara ya michezo ya kubahatisha katika wilaya yake baada ya kubaini kwamba kulikuwa na uvunjfu wa sheria ambapo alielekeza jeshi la jadi Sungusungu kusimamia agizo hilo.

“Sisi kama chombo cha serikali tunaona hatua aliyochukua ni nzuri na itasaidia katika kuimarisha utekelezaji wa sheria lakini nashauri wakati mwingine ili zoezi hilo lifanyike vizuri ni vema viongozi na mamlaka nyingine wakashirikisha GBT ambayo ina watu wenye weledi katika eneo hilo na kwahakika itarahisisha utekelezaji wake bila ya kuleta taharuki.” Alisema.

“Sisi tumeamua kupambana na uhalifu wa mashine za michezo ya kubahatisha zilizozagaa kwenye maeneo yasiyoruhusiwa na kutozingatia sheria, hata kama watakuwa ni waendeshaji tuliowapa leseni tutachukua hatua kali pindi tutakapobaini wamevunja sheria.” Alionya Bw. Mbalwe.

Pia alisema GBT inaendelea na msako wa kuwabaini wale wote wanaoingiza mashine hizo nchini kinyume cha sharia.

Nae Mkurugenzi Msaidizi wa Kampuni ya Chilambo ambayo ndiyo inahusika na kuharibu “taka hatarishi” hususan za umeme, Bi. Venither Gideon alisema mashine hizo zitavunjwa vunjwa na kisha kuzitenga kwenye makundi kulingana na asili yake.

“Jukumu letu ni kuhakikisha tunaziharibu mashine hizi katika njia ambayo ni salama kwa uhifadhi wa mazingira.” Alisema.

 

Mkurugenzi Mkuu wa GBT James Mbalwe, akionyesha shehena ya mashine haramu za kuendeshea michezo ya kubahatisha (Slot Machines) zipatazo 300, ambazo baadaye  GBT iliziteketeza Kisarawe mkoa wa Pwani, jana Oktoba 28, 2022.

Baadhi ya mashine haramu za kuendeshea michezo ya kubahatisha (Slot Machines) zipatazo 300, zilizoteketezewa Kisarawe mkoa wa Pwani, jana Oktoba 28, 2022.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages