Seoul, Korea Kusini
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasihi Watanzania wanaoishi ughaibuni kuwa mabalozi wazuri kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi wanazoishi ili kujenga taswira nzuri ya Taifa lao huko waliko.
Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Oktoba 28, 2022) wakati akizungumza na Watanzania waishio katika Jamhuri ya Korea kwenye ukumbi wa hoteli ya Mondrian iliyopo Seoul nchini humo.
Mheshimiwa Majaliwa pia amewataka Watanzania hao watumie fursa walizonazo kushawishi na kuvutia uwekezaji nchini Tanzania.
“Tumieni ushawishi na fursa mlizonazo kuwavutia wawekezaji na siku zote semeni mazuri na fursa za kiuchumi zilizopo Tanzania bila kusahau kuwasemea vizuri viongozi wakuu hasa dhamira nzuri ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuliletea maendeleo Taifa”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wajenge utamaduni wa wa kutumia lugha ya Kiswahili kama fursa ya kiuchumi kwani nchi nyingi zinahitaji walimu, waandishi, watangazaji na wakalimani wa lugha ya kiswahili.
Pia Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia kuwa Tanzania ipo salama na Mheshimiwa Rais Samia anafanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba maisha ya Watanzania yanaimarika kwa kuendelea kusogeza karibu huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo maji, umeme na elimu.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Korea John Bakunda ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuendelea kuimarisha diplomasia ya kiuchumi na mataifa mbalimbali duniani.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watanzania waishio nchini Korea kwenye hoteli ya Mondrian iliyopo Seoul, Oktoba 28, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇