LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 5, 2022

DK. MPANGO AFANYA MAZUNGUMZO NA MSAIDIZI WA KATIBU MKUU WA UN, IKULU DAR ES SALAAM, LEO

Ikulu, Dar es Salaam
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ted Chaiban, ambaye ni Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko19.

Katika mazungumzo na mgeni huyo yaliyofanyika leo, Ikulu Dar es Salaam, Makamu wa Ramesema Serikali imelenga kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na Uviko 19 ikiwemo kutoa chanjo hususani kwa watu wote walio katika hatari ya kupata madhara zaidi ya ugonjwa huo.

Amesema katika kudhibiti ugonjwa huo, Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya afya, kuwajengea uwezo watumishi wa Afya katika kukabiliana na ugonjwa huo,kuimarisha huduma za dharura pamoja na ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya ili kusaidia huduma muhimu ya afya ambayo iliathiriwa na janga la Uviko19 hususani kwa huduma ya afya ya msingi.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba pamoja na mafaniko yaliopatikana katika kudhibiti Uviko19 bado serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na  kujenga miundombinu itakayoweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pindi yatakapotokea.

Kwa upande wake Chaiban, ameipongeza Tanzania kwa juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya utoaji wa chanjo. Amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwafikia watu wengi zaidi wanaohitajika kupata chanjo ikiwemo makundi maalum kama vile watumishi wa afya pamoja na wazee.

Amesema juhudi za ufanikishaji wa utoaji chanjo zinapaswa kuhusisha moja kwa moja ngazi ya mikoa na wilaya ili kufikia kirahisi malengo ya taifa katika zoezi hilo na kwamba ipo haja ya kuwaelimisha watumishi wa sekta muhimu kama vile Elimu na Utalii ili kuendelea kuhamasisha zoezi la upokeaji chanjo katika sekta zao.

Chaiban amesema changamoto za Uviko 19 zinatoa funzo kwa mataifa hususani yanayoendelea kuwekeza katika afya ya msingi pamoja na kuongeza uzalishaji wa ndani ili kuendelea kupata bidhaa hususani wakati wa mlipuko wa magonjwa duniani.

Makamu Dk. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ted Chaiban, ambaye ni Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko19, Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Julai 5, 2022.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages