LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 28, 2022

CCM YAPULIZA KIPYENGA KWA WANACHAMA WAKE WANAOHITAJI KUTEULIWA NA CHAMA KUGOMBEA UBUNGE WA BUNGE LA AFRIKA MASHIRIKI

CCM Makao Makuu, Dodoma
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeliza kipyenga kwa wanachama wake wote walio na nia na sifa za kuweza kugombea na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa tiketi ya CCM, kukaa mguu sawa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, leo Julai 28, 2022 imesema, mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za maombi ya kuteuliwa kugombea nafasi hizo kupitia CCM,  utaanza Agosti Mosi, 2022 hadi Agosti 10, 2022.

Shaka ameeleza katika taarifa hiyo kwamba Fomu za maombi ya kuteuliwa kugombea nafasi hizo zitachukuliwa na kurejeshwa  kuanzia saa 2.00 hadi saa 10:00 jioni katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM Dodoma,  Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar na Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam.

Amezitaja sifa za mwanachama anayestahiki kugombea nafasi hizo kupitia CCM kuwa ni;
(a) Awe ni Mwanachama hai wa CCM, (b) Awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na (c) Awe na sifa zinazostahiki kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977.

(d) Awe sio Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, (e) Awe sio mtumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na (f) Awe na uzoefu uliothibitishwa au moyo wa kupenda kuimarisha na kuendeleza malengo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Siku ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu za maombi ya kuteuliwa kugombea nafasi hizo, ni tarehe 10 Agosti, 2022, Saa 10:00 Jioni", mesisitiza Shaka katika taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages