LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 14, 2022

AG FELESHI AKAGUA UJENZI WA JENGO LA OFISI YA AG KATIKA MJI WA MTUMBA, AWASHUKURU RAIS SAMIA, JPM KWA MAONO

Na Mwandishi Maalum, Dodoma.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi, ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuijumuisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara nyingine ambazo zimepewa fedha za kujenga Majengo ya kudumu katika Mji wa Serikali wa Mtumba, Jijini  Dodoma.

Ametoa shukrani hizo leo, Alhamisi, Julai 14, 2022, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo jipya la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mji huo wa Serikali.

“Ninawashukuru sana Rais wa Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan na Mtangulizi wake Hayati Dk. John Magufuli kwa maono yao na utambuzi wao wa kuiunganisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara mbalimbali katika awamu ya kwanza na ya pili ya ujenzi wa majengo ya kudumu hapa Mtumba.Hii ni heshima kubwa kwetu na  hasa kwa kuzingatia unyeti wa majukumu yetu”, akaeleza Mhe. AG

Katika ziara yake hiyo ambayo alikuwa ameambatana na Menejimenti yake, AG Feleshi amesema uamuzi wa Serikali wa kuwa na majengo ya kudumu ya serikali katika Mji wa Serikali wa Mtumba ni uamuzi wa kihistoria kwa vizazi na vizazi na umeufanya mji huo wa Serikali kuwa kivutio cha kitalii.

“ Majengo haya ni ya kudumu, ni historia kwa vizazi na vizani na kwa miaka mingi ijayo.  Kwa  hiyo nanyi Wakandarasi ambao mmepata fursa ya kujenga majengo haya lazima mjivunie historia hii kwa kufanya kazi wa uadilifu na kwa  wakati, kwa sababu mnaandika historia”, akasisitiza  AG Feleshi.

Jengo la Ofisi  ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lenye ghorofa tano  na  umbo la herufi 'Y'  linajengwa na   Mkandarasi SUMA JKT  Kanda ya Kati na licha  ya kuwa na umbo la herufi Y, litakapokamilika  litakuwa ni kati ya majengo ya kipekee na makubwa matatu katika majengo yote ya serikali yanayojengwa katika mji huo wa serikali.

AG Feleshi pamoja na kuridhishwa na namna kazi ya jenzi wa  mradi huo , memtaka Mkandarasi kutosita kumpatia taarifa endapo kutakuwa na uchelewesashi wowote au urasimu kutoka pande zote mbili ( mteja na   mkandarasi) ili aweze kuchukua hatua zozote.

“Mmenieleza hapa kwamba kwa sasa hamna changamoto kubwa, ila niwaombe kama kutakuwa na changamoto yoyote iwe kutoka Ofisini kwangu au kutoka Jeshini msisite kunijulisha ili hatua za mapema zichukuliwe. Lakini sisi ni wasimamizi wa Sheria, pia nisingependa kuona kunajitokeza matatizo yoyote ya kisheria kwenye mradi huu”, akasema AG Feleshi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia alijiridhisha kwamba fedha za utekelezaji wa mradi huo zimekuwa zikitolewa kwa wakati kila Mkandarasi anapowasilisha hati zake ( Certificate) na kwamba hakuna malimbilizo yoyote.

Awali akitoka maelezo ya maendeleo ya  mradi huo  Mshauri  Mwelekezi Mhandisi  William Sele  kutoka  Wakala wa  Majengo ( TBA) alimweleza Mhe. AG na Ujumbe wake kwamba kazi ya ujenzi wa jengo hilo  unakwenda vizuri kwa asilimia 26 ya ujenzi na kwamba hawategemei kupata changamoto kubwa labda uhaba wa mali ghafi  hapo baadaye.

Mhandisi Sele pia amesema  sasa hivi TBA  inajitahidi sana katika  usimamizi wa kazi zake ili kwenda na wakati na kuondoa malalamiko  ya kwamba TBA wamekuwa  wakishelewesha utekelezaji  na ukamilishaji wa miradi mbalimbali.

“Sasa hivi kwa kweli  tumejipanga  vizuri, kazi zinakwenda kwa wakati, vibali vinatolewa kwa wakati, huko nyuma TBA tulikuwa tunalalamikiwa  kwa ucheleweshaji wa vibali na mengineyo kama hayo, sasa tupo vizuri”, akasema  Mhandisi Sele

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi akizungumza na Makandarasi (hawapo pichani) baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Mwanasheria Mkuu wa Serikali linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba JijiniDodoma, leo.( Picha na Mpigapicha Maalum, Ofisi ya AG).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages