LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 4, 2022

KAMPUNI YA JHIL KUISAIDIA KLABU YA SOKA YA KMKM KUPATA SOKO LA WACHEZAJI WAKE ULAYA

Na Makame Mshenga, Zanzibar
Kampuni ya Kimataifa ya JHIL inayojenga Uwanja wa Kimataifa wa Cricket na michezo mingine katika kijiji cha Fumba Zanzibar, inakusudia kuisaidia Klabu ya KMKM, kubadilishana uzoefu na kuwatafutia soko la Ulaya wachezaji wake.

Mratibu wa Kampuni hiyo Ismail Shah alisema kwa kuwa mradi wa viwanja vya michezo Fumba utajumuisha pia uwanja wa soka hivyo ni vyema kuanza taratibu mapema ili kabla ya viwanja kujengwa programu mbali mbali za kuimarisha soka ziwe zimeanza

Alisema wameichagua KMKM kwa vile klabu hiyo imejipanga vyema katika michezo mingi ikiwemo mchezo wa soka.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya JPM Sports na Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Viking FC ya Norway, Eirik Henningsen alisema kupitia makubaliano na KMKM watakuwa na utaratibu wa kubadilishana uzoefu ambapo wachezaji, makocha na wataalamu wa KMKM watakwenda Norway kujifunza na wale wa Norway watakuja Zanzibar.

Mwenyekiti wa Klabu ya KMKM Capt. Khatibu Khamis Mwadini, aliushukuru ugeni huo na kusema kuwa umekuja muda muafaka wakati klabu ya KMKM ambayo ni bingwa wa ligi kuu ya Zanzibar ikijiandaa kwa michezo ya kimataifa.

Alimshukuru  Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kwa kusaidia kupatikana wataalamu hao ambao watasaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo nchini.

Katibu wa klabu ya KMKM, Sheha Mohamed Ali, alisema ana matumaini makubwa kuwa wataalamu hao watakuwa chachu ya mabadiliko ya michezo mingi nchini jambo ambalo litaing’arisha Zanzibar katika medani ya michezo.

Aidha alisema watatoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika kuhakikisha malengo yaliyopangwa yanaweza kutimia kwa wakati.

Mratibu wa Kampuni ya Kimataifa ya JHIL Enterprises, Ismail Shah, akizungumza na uongozi wa Klabu ya KMKM  juu ya makubaliyano ya kuisaidia klabu ya KMKM, katika mazungumzo iliyofanyika Makao Makuu, Kibweni, Zanzibar, leo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages