LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 23, 2022

DK. MPANGO AUNGURUMA USWIS, ASEMA NCHI ZA AFRIKA ZINAWEZA KUFANYA UWEKEZAJI MKUBWA KATIKA KILIMO NA KUTOSHELEZA MAHITAJI YA CHAKULA DUNIANI

Davos, Uswis
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango amesema, nchi za Bara la Afrika zinaweza kufanya uwekezaji mkubwa katika kilimo cha kisasa na kuweza kutosheleza mahitaji ya chakula Duniani.

Akizungumza katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani unalofanyika Davos nchini Uswisi kuchangia mada ya kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa chakula duniani, Makamu wa Rais amesema hatua hiyo itakuwa ni moja ya njia muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa chakula Duniani.

 

Amesema nchi za Afrika kutokana na kujaliwa ardhi pamoja na maeneo ya uzalishalishaji katika sekta ya kilimo zinapaswa kuboresha sera ili ziwe rafiki katika kilimo ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa chakula.

 

Makamu wa Rais ameongeza kwamba nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na himilifu, kuwekeza katika miundombinu ikiwemo barabara pamoja na kutenga ardhi kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa pamoja na wawekezaji. 

 

Ameongeza kwamba kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi kuna ulazima wa kuwekeza katika viwanda vitakavyozalisha pembejeo ikiwemo mboleo na mbegu.

 

Makamu wa Rais ameziasa taasisi za Kimataifa za utafiti kuungana mkono jitihada za nchi za Afrika katika kuboresha afya ya udongo ili kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo. Aidha amesisitiza umuhimu wa suala la amani duniani ili kutoa fursa ya uzalishaji na usambazaji wa chakula duniani.

 

Amesema Tanzania inapanga kutumia rasilimaliwatu hasa vijana katika mnyororo wa thamani wa kilimo kwa kutenga maeneo ya kilimo yatakayokwenda sambamba na huduma za pamoja kama vile huduma za ugani, pembejeo na masoko.

 

Mada hiyo imejadiliwa kutokana na dunia kukabiliwa na changamoto mbalimbali zinazopelekea upungufu wa chakula duniani kama vile Uviko19, vita pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi.

 

Makamu wa Rais yupo Davos nchini Uswisi kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani unaoshirikisha wakuu wa nchi, wakuu wa taasisi na mashirika ya kimataifa pamoja pamoja na wafanyabiashara.

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango akizungumza kwenye Mkutano huo, leo.
Wajumbe wa Mkutano huo wakimsikiliza Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages