LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 18, 2022

CCM YATOA TAARIFA YA MWELEKEO NA MAFANIKIO YA NDANI YA MWAKA MMOJA WA RAIS SAMIA, LEO

Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo kimeleza mwelekeo na mafanikio yaliyopatikana katika Kipindi cha mwaka mmoja wa Utendaji wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Taarifa ya mwelekeo na mafanikio hayo imeelezwa na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba Jijini Dar es Salaam.

 

Ifuatayo ni Taarifa hiyo;👇

TAARIFA YA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MWAKA MMOJA WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. SAMIA SULUHU HASSAN MADARAKANI

Utangulizi

Siku ya kesho, Machi 19, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (atakuwa) anatimiza mwaka mmoja tangu aliposhika rasmi madaraka ya kuongoza nchi hii, baada ya kuapishwa tarehe na mwezi kama huo, mwaka 2021. Kiapo hicho kilimpatia dhamana ya kushika madaraka na mamlaka ya kuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

 

Sote tunajua kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan alichukua dhamana ya kuiongoza nchi yetu, katika mazingira ambayo hayakuwa yametarajiwa, baada ya Taifa kupatwa na msiba mzito wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu John Joseph Pombe Magufuli, ambaye alitwaliwa na muumba wetu mnamo Machi 17, 2021.

 

Nafasi ya CCM katika mwaka 1 wa Rais Samia

Mwaka mmoja wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani ambao Watanzania kwa umoja wetu tutauadhimisha kesho, ni matokeo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupewa ridhaa na Watanzania kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ambapo Chama chetu kilipigiwa kura, kikashinda uchaguzi na kupata dhamana ya kushika dola, kuunda na kusimamia Serikali, na kuongoza Nchi.

 

Sote tunajua kuwa katika kutekeleza wajibu na majukumu yake, Serikali anayoisimamia na kuiongoza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, mbali ya kuongozwa na Katiba ya Nchi, Sheria zinazotungwa na vyombo vya uwakilishi wa wananchi, sera, kanuni na miongozo mbalimbali, pia inatekeleza Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025. Hayo yote kwa pamoja ndiyo yanaunda taratibu ambazo sisi kama Taifa tumekubaliana kuwa ndiyo zana za kuendesha mambo yetu wenyewe, katika kujitawala na kuongozwa.

 

Ni kwa muktadha huo, leo CCM inaposimama hapa kuzungumza kuhusu mafanikio, maendeleo na ustawi wa wananchi na Taifa letu ndani ya mwaka huu mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, tunazumgumzia suala ambalo tuna wajibu nalo kwa asilimia zote.

 

Ndani ya muda huu ambao ukipimwa kwa mizania ya miaka 5, unaonekana ni mfupi, kuna mafanikio mengi. Hapa tutayasema kwa ufupi;

 

Mfariji Mkuu wa Taifa

Kwa nafasi zake zote, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mfariji Mkuu wa Taifa (Comforter-In-Chief). Na huu ndio ulikuwa mojawapo ya wajibu wa kwanza kabisa ambao Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliutekeleza, baada ya hali ambayo Taifa lilipitia kutokana na msiba wa Hayati Ndugu John Magufuli, Mheshimiwa Rais alidhihirisha jukumu hilo kwa kuonesha uongozi imara, madhubuti, kwa ujasiri na umahiri mkubwa, kwenye wakati ambao dunia nzima ilikuwa inatuangalia namna tutakavyosimama na kusonga mbele. Akaitekeleza kwa vitendo kauli mbiu aliyoiasisi ya ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…Kazi Iendelee.’ 

 

Katika muktadha huo huo wa nafasi ya Mfariji Mkuu wa Taifa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuwaonya na kuwatahadharisha Watanzania juu ya jambo lolote linaloweza kuwa na athari hasi kwa maendeleo ya nchi yetu na ustawi wa mtu mmoja mmoja (mfano ukame, njaa, magonjwa) na maneno yenye chokochoko zenye nia ovu.

 

Hali ya kisiasa

Katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2020 – 2025, hasa katika ibara zilizobebwa na Sura ya Sita, CCM iliwaahidi wananchi kuwa itaimarisha hali ya utulivu wa kisiasa na umoja wa kitaifa nchini, hasa kupitia utoaji haki, utawala bora unaozingatia sheria, kuimarisha misingi ya demokrasia na kutoa madaraka kwa wananchi, ikiwemo uhuru wa kutoa maoni juu ya namna wanavyotaka nchi yao ijitawale.

  

Sote ni mashahidi kwa macho na masikio yetu, jinsi ambavyo katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametekeleza eneo hili kwa kauli na vitendo. Tumeshuhudia akikutana na makundi mbalimbali katika jamii, akiwasikiliza, kuzungumza na kushauriana nao kuhusu masuala mbalimbali kwa ajili ya kujenga mstakabali mzuri wa kisiasa wa Nchi yetu, na hatimae kuwa na mwelekeo mzuri wa kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya watu, kama ambavyo CCM  iliahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu. 

 

Lengo la kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii ni kuimarisha misingi ya maelewano na kujenga umoja wa kitaifa. Makundi ambayo Mheshimiwa Rais ameshakutana nayo na amekuwa akishirikiana nayo kwa karibu katika uongozi wake ni viongozi wa dini, viongozi wa kimila, ambao pia wamempatia dhamana ya kuwa mkuu wao, ‘Chifu Hangaya’, walemavu, vijana, wafanyabiashara wadogo wadogo (Wamachinga), Asasi za Kiraia, wanawake, wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), na viongozi wa vyama vya siasa, ama mmoja mmoja au katika makundi.

  

Kwa mfano, tumeona alivyokutana na kuzungumza na wadau wa siasa katika mkutano ulioandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa nchini na kufanyika Disemba 15-17, mwaka jana, ambao ulisababisha kuundwa kwa Kikosi Kazi chini ya uwenyekiti wa Prof. Rwekaza Mkandala, kilichopewa jukumu la kuratibu na kuchambuia maoni ya wadau juu ya namna bora ya kuendesha siasa za ushindani za vyama vingi nchini.  

 

Tayari tumeanza kuona matunda ya kikosi Kazi hicho, ambapo hivi karibuni kiliwasilisha taarifa yake ya awali, na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kwa wizara husika, kuanza kuandaa Kanuni zitakazoongoza na kusimamia namna bora ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.

 

Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini (ndani na nje ya nchi), kwa nia ile ile ya kusikiliza makundi mbalimbali katika jamii, bila kujali tofauti zinazoweza kuwepo, zikiwemo za kisiasa.

 

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, tumeshuhudia jinsi ambavyo uhuru wa kutoa maoni ulivyozidi kuimarika kwa mwananchi mmoja mmoja, makundi ya kijamii, zikiwemo Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari. Hii ni mojawapo ya misingi muhimu katika ukuzaji na ujenzi wa demokrasia na madaraka ya wananchi katika kujitawala, na Chama Cha Mapinduzi kwa kutambua hilo, kililisisitiza jambo hili katika Ilani ya 2020 - 2025, inayotekelezwa sasa na Serikali.

 

Kupitia ilani, CCM ilielekeza Serikali kuhakikisha misingi ya demokrasia na haki za binadamu na umoja wa kitaifa, inalindwa na kuheshimiwa kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria na taratibu mbalimbali pamoja na mikataba na itifaki za kikanda na kimataifa.  Kutokana na kutekeleza vizuri eneo hilo ndani ya mwaka huu mmoja, Rais Samia sio tu ameendelea kuwapatia matumaini wananchi, bali pia kuwahakikishia upatikanaji wa fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo bila kuwepo bugudha yoyote. 

 

Katika muktadha huo huo, tumeshuhudia kuendelea kuimarika kwa uhuru wa utendaji kazi wa mihimili ya dola, ikitekeleza majukumu yake kwa uhuru pasipo kuingiliana huku ikiimarisha utamaduni wa kuheshimiana na kushirikiana kwa ajili ya utendaji mzuri wa Serikali na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

 

Hali ya Kiuchumi na usimamizi wa rasilimali za Watanzania

Kupitia Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025, ndani ya Sura ya Pili, Chama kiliahidi kwa wananchi na kuielekeza Serikali, kuweka mazingira na fursa za kufanikisha mapinduzi ya uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi, kwa maendeleo ya watu, ambapo wananchi wa Tanzania, kupitia shughuli mbalimbali, za umma, sekta binafsi na ushirikiano wa pande hizo mbili, ndiyo watakuwa wanufaika wakubwa wa uchumi huo na rasilimali za Taifa. 

 

Sambamba na hilo, Ilani ya CCM, imeitaka Serikali kuimarisha viashiria vya ukuaji wa uchumi ili kujihakikishia mwenendo tulivu wa uchumi mpana muda wote, jambo ambalo leo hii, CCM inajivunia kwani Serikali zake zimelitekeleza vyema sana. 

 

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, chini ya uongozi wa Rais Samia, tumejionea kuwepo kwa mwenendo mzuri wa ukuaji chanya wa uchumi, ambao kutokana na taarifa za kitaalam, umechangiwa na kuwepo kwa ongezeko la uwekezaji, mathalani katika miradi ya kimkakati kwenye miundombinu  ya nishati ya umeme, maji, afya, elimu, ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege. Aidha, uzalishaji wa madini hususan ya dhahabu, makaa ya mawe na mazao ya kilimo ambao umeongezeka sana.

 

Katika kipindi hicho hicho, kumekuwa na ukuaji wa kiwango kikubwa katika sekta za madini na mawe (asilimia 10.9), habari na mawasiliano (asilimia 10.2), huduma za kijamii (asilimia 9.8), umeme (asilimia 9.7), na maji (asilimia 7.0).

 

Ukuaji chanya wa uchumi umeleta matokeo ya wazi yanayoonekana, mathalani kuongezeka kwa mzunguko wa fedha (ukwasi) kwa wastani wa asilimia 9.3, kutoka asilimia 4.8 iliyokuwepo mwaka wa fedha wakati anakabidhiwa dhamana. Hii imesababishwa na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, msisitizo wa kuhakiki na kulipa malimbikizo ya madeni ya wakandarasi, wazabuni, watumishi na hata wastaafu.

 

Jambo lingine linaloonekana wazi kutokana na ukuaji chanya huo wa uchumi, ni kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi kutoka asilimia 3.1 hadi kufikia asilimia 10. Hili nalo limesababishwa na kuwepo kwa fursa mbalimbali katika shughuli za kiuchumi, ambazo tumeziona katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani. Kanuni za kawaida katika masuala ya ukuaji wa uchumi zinatuambia kuwa ongezeko hilo maana yake ni kwamba kuna shughuli nyingi zinafanyika katika sekta binafsi ambayo ni mojawapo ya injini muhimu katika kukuza ajira na hivyo kugusa maisha ya mtu mmoja mmoja kwenye ngazi ya kaya.

 

Pia kumekuwa na nafuu kubwa upande wa mikopo chechefu kwa mabenki yetu nchini, ambapo imepungua kutoka asilimia 9.3 hadi sasa ni asilimia 8.2. Matokeo haya yamesababishwa na kuboreshwa kwa fursa anuai, ushikirikishwaji wa sekta binafsi katika miradi ya maendeleo na ulipaji wa malimbikizo ya madeni baada ya uhakiki kufanyika, hasa kwa wakandarasi.

 

Lingine ni kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Kimarekani 60 bilioni hadi kufikia Dola za Kimarekani 64 bilioni. Kwa mujibu wa BoT, akiba hii inatosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi kisichopungua nusu mwaka. Wanasema pia, ni zaidi ya lengo la nchi wanachama wa EAC la miezi walau 4.5 na miezi 6 kwa wanachama wa SADC.

 

Aidha, katika kipindi hiki cha mwaka mmoja, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imeweka ‘record’ ya kukusanya kiwango kikubwa cha mapato tangu kuanzishwa kwake, kwa kukusanya jumla ya shilingi trilioni 2.5, mwezi Disemba, mwaka jana. Mbali ya jambo hilo la kipekee, ndani ya kipindi hiki pia kumekuwa na ongezeko la mapato ya ndani kutoka shilingi trilioni 11.6 ya mwaka wa fedha wa 2020 – 2021, hadi kufikia shilingi trilioni 15.9, mwaka wa fedha 2021 – 2022, ikiwa ni sawa na asilimia 93.5 ya makadirio ya kukusanya trilioni 17.0. ongezeko hilo (shilingi trilioni 11.6-15.9) ni sawa na ongezeko la shilingi trilioni 2.1.

 

Kwa ujumla, kutokana na utashi mkubwa wa kisiasa wa Kiongozi Mkuu wa nchi katika kutekeleza Ilani ya Chama tawala, tumeshuhudia kiwango kikubwa cha uboreshwaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara, mashauriano, uwazi, uwajibikaji na elimu kwa umma, kwa mwaka huu mmoja, ambayo yamekuwa yakienda sambamba na utekelezaji wa kasi kubwa wa miradi ya maendeleo inayohusisha ushiriki wa sekta binafsi, mfano hai ukiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii na Mapambano ya UVIKO-19 pamoja na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2021 – 2022. Utashi huo pia umesaidia kuwepo kwa ongezeko la makusanyo ya kodi inayolipwa kwa hiari (imewezesha ujenzi wa madarasa elfu 15, vituo vya afya, maji n.k).  

 

Huduma za kijamii;

Katika eneo hili, Sura ya Tatu ya Ilani ya CCM ya 2020 – 2025, imeahidi kwa wananchi masuala kadhaa ili kuendelea kuimarisha na kupanua huduma za jamii, nchini; ikiwemo elimu, afya, maji na ustawi wa jamii. Hivyo Chama kilielekeza Serikali, kupitia sera, mikakati na mipango mbalimbali, kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na fursa ya kupata huduma hizo kwa ubora, kwa kiwango cha kutosha na bila vikwazo. CCM kama chama kinachotawala, kinaelewa katika eneo hili ndiko taifa litafanikisha mapambano ya maadui wetu wakubwa, Ujinga, Malazi na Umaskini. 

 

1.  Elimu;

Katika eneo la elimu, ndani ya mwaka huu mmoja wa uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na mafanikio na mapinduzi makubwa. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, wanafunzi wa kidato cha kwanza wote wameingia shuleni kuanza masomo yao kwa siku moja bila kuwepo waliosubiria nyumbani kujiunga sekondari kwa chaguo la pili, ambalo miaka yote lilikuwa linasababishwa na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya (UPUNGUFU) miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, hasa vyumba vya madarasa na madawati. Hilo limewezekana baada ya kujengwa kwa madarasa 12,000, bila kusahau madarasa mengine 3,000 ya shule shikizi. Hiyo inafanya jumla ya madarasa 15,000 ambayo yalijengwa ndani ya miezi 3!

 

Ndani ya mwaka huu mmoja kumekuwa na uimarishaji na uboreshaji mkubwa wa utoaji wa elimu katika maeneo yote yaliyoelekezwa katika Ilani ambayo ni elimumsingi, elimu ya sekondari, elimu ya ualimu, elimu ya ufundi na elimu ya juu. Tumeshuhudia namna ambavyo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwa kuboresha utoaji wa elimu maalum na kuongeza nafasi za mafunzo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum. 

 

Aidha, kuna ujenzi wa shule zingine za sekondari mpya zipatazo 245 unaendelea, lengo likiwa ni kuongeza fursa za upatikanaji wa Elimu ya Sekondari hususan kwa watoto wa kike, katika kata ambazo hazina shule za sekondari ili kuwapunguzia watoto umbali wa kutembea sna hivyo kuimarisha ulinzi wao waendapo na watokapo shuleni. 

 

Serikali imetekeleza vyema maelekezo ya Ilani kuhusu uboreshaji na upanuaji wa elimu ya ufundi, ambapo jumla ya vyuo vya ufundi stadi 25 vimejengwa katika wilaya na halmashauri za wilaya maeneo mbalimbali nchini, ujenzi wa vyuo vya VETA katika mikoa 4 ambayo hapo awali haikuwa navyo kabisa pamoja na uboreshwaji wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii (FDC). 

 

Kwenye elimu ya juu, chama kilielekeza Serikali kuimarisha na kuboresha mfumo wa ugharamiaji wa elimu ya juu ili kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji na sifa stahiki wanapata fursa hiyo. Katika eneo hili pia namba za wanufaika na uwekezaji, hazidanganyi, zinasema zenyewe, kuanzia kwenye ongezeko la bajeti ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 464 hadi shilingi bilioni 570, ambazo limeenda sambamba na kuongezeka kwa wanufaika wa mkopo wa mwaka wa kwanza kutoka wanafunzi 55,287 mwaka 2020/21 hadi takribani 76,300 mwaka 2021/22, hivyo kufanya jumla ya wanufaikaji wote pia kuongezeka kutoka wanafunzi 142,170 mwaka 2020/21 hadi wanufunzi 176,617 kwa mwaka 2021/22.

 

Sote tunajua namna wanufaikaji wa mikopo hii walivyoshusha pumzi za ahueni ya kuondolewa mizigo mikubwa miwili iliyokuwa inalalamikiwa kuwaelemea, kwanza ile TOZO ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha katika urejeshaji wa mkopo na pili tozo ya adhabu ya asilimia 10 ya mkopo ambayo ilikuwa ikitozwa kwa wanaochelewa kurejesha mkopo.

 

Ni muhimu kuwakumbusha Watanzania kuwa Serikali ya CCM, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ndani ya mwaka huu mmoja, imeendelea kutekeleza sera ya elimu bila malipo kwa wanafunzi wa elimumsingi nchini kote na kwamba hakuna dhamira ya kurudi nyuma katika hilo.

 

2.  Afya;

Ndani ya mwaka huu mmoja eneo muhimu la sekta ya afya nalo limefikiwa kwa kiwango kikubwa kama ambavyo Ilani ya CCM imeahidi ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi. Hospitali za rufaa za mikoa 19 ziko katika hatua mbalimbali za kukamilisha ujenzi na ukarabati wake. Kuna miradi ipatayo 127 ya ujenzi wa hospitali inaendelea katika halmashauri za wilaya nchini, halikadhalika kuna ujenzi wa vituo vya afya vipatavyo 233 katika tarafa 207, vyote hivi vina uwezo wa kufanya upasuaji, vikiwa na majengo ya OPD, Maabara na vichomea taka. Bila kusahau ujenzi wa zahanati zipatazo 564 katika halmashauri mbalimbali nchini ambao uko katika hatua za kukamilika.

 

Katika eneo la upatikanaji wa dawa ili kuondokana na malalamiko ya wananchi, mbali ya Serikali kutumia takriban Shilingi bilioni 333 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendenashi, inajenga viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba katika eneo la Idofi, Halmashauri ya Makambako, mkoani Njombe kwa lengo la kupunguza ununuzi wa dawa kutoka nje ya nchi. Hatua hii itasaidia kuimarisha upatikanaji wa dawa kwa wakati na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kwa ajili ya kununulia dawa nje ya nchi na hivyo fedha itakayookolewa itaelekezwa katika mipango mingine ya kuboresha huduma kwa wananchi.

 

3.  Maji;

Ilani ya CCM katika ukurasa wa 147 – 150, inatamka kuwa uimarishaji wa huduma ya maji ni mojawapo ya agenda za kudumu za CCM tangu tulipopata uhuru, kwa sababu tunatambua maji ni msingi wa uhai wa binadamu na injini ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwani uhakika wa upatikanaji wake, yakiwa safi na salama, huchangia katika kuzuia magonjwa, na hivyo kuimarisha afya na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.

 

Mwaka 2020 kupitia Ilani ya Uchaguzi, tumewaahidi wananchi kuwa tutaielekeza Serikali kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na usalama wa maji na huduma hiyo iwafikie Zaidi ya asilimia 85 ya wakazi wa vijijini na zaidi ya asilimia 95 kwa mijini ifikapo mwaka 2025. Kazi kubwa inaendelea kufanywa nchi nzima, ikiwemo ile ya ujenzi wa miradi mikubwa ya maji nchi nzima.

 

4.  Miundombinu ya usafirishaji na uchukuzi – barabara, reli, anga na majini

Katika ibara ya 55 hadi ya 96, Chama Cha Mapinduzi kiliweka ahadi kwa wananchi kuhusu namna kitakavyoboresha na kufungua mazingira ya ustawi wa wananchi kuendeleza uzalishaji kwa ajili ya kuongeza kipato na fursa mbalimbali za shughuli za kiuchumi, kupitia sekta za ujenzi wa miundombinu, uchukuzi na mawasiliano.

 

Katika mwaka huu mmoja, eneo hili nalo limefanyiwa kazi kwa kiwango ambacho CCM inaridhika nacho. Serikali imekamilisha ujenzi wa daraja la kisasa la Tanzanite jijini Dar es Salaam sambamba na barabara unganishi zenye urefu wa km 5.2 kwa jumla ya Tsh. 243 bilioni. 

 

Ujenzi wa miradi mikubwa ya Daraja la Magufuli lililoko Kigongo-Busisi, Mwanza, Daraja la Mto Wami, mkoani Pwani, unaendelea katika hatua mbalimbali, ambapo Busisi ujenzi uko asilimia 40 na Wami ujenzi uko asilimia 75 na wakandarasi wako kazini.

 

Tunapozungumza hapa ukanda wa magharibi mwa nchi yetu unazidi kuunganishwa na kufunguliwa fursa mbalimbali baada ya kukamilika kwa Barabara ya Katavi – Tabora huku Barabara ya Kakonko hadi Kasulu ujenzi wake ukiendelea kwa kiwango cha lami. Ni hivi karibuni tu Rais Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje yenye urefu wa kilometa 112.3 katika Jiji la Dodoma.


Kwa upande wa usafiri wa anga, miradi ya ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za usafiri na usafirishaji imefanyika na mingine inaendelea katika hatua za utekelezaji katika mikoa mbalimbali nchini mfano; Kiwanja cha Ndege cha Songea (asilimia 95), Mtwara (asilimia 85), Iringa (asilimia 33.42), Musoma (asilimia 04), pamoja na ujenzi wa jengo la abiria katika kiwanja cha ndege cha Songwe (asilimia 81). Kuhusu Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato Mkoani Dodoma ulipaji fidia umekamilika kwa asilimia 98, mkataba wa awamu ya kwanza wa ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege umesainiwa tayari na mkandarasi amekabidhiwa eneo la mradi mapema mwaka huu.

 

Mwaka huu mmoja pia tumeshuhudia ujenzi na ukarabati wa bandari za TPA na zingine ndogo ndogo, huku tukijionea mafanikio ya ukarabati wa Bandari ya Mtwara katika kurahisisha uchukuzi na usafirishaji na kuifungua mikoa ya Kusini.

 

Halikadhalika ujenzi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR) unaendelea vizuri ambapo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi huo kipande cha kutoka Makutupora (Singida) hadi Tabora chenye urefu wa Kilometa 368 katika kipande cha tatu cha mradi huo (Lot III), alisisitiza kuwa lazima utatekelezwa hadi kumalizika kwa namna yoyote ile. Chini ya usimamizi na uongozi wake, Mheshimiwa Rais amesaidia kuwepo kwa mazungumzo kati ya nchi nne, Tanzania, Congo DRC, Burundi na Rwanda, ili kushirikiana kufikisha SGR katika nchi hizo na kuunganisha sekta ya uchukuzi na usafirishaji, ambapo kwa upande wa Congo DRC itaunganishwa kwa kipande cha Kaliua, Mpanda kupitia Bandari za Karema na Kalemie. Burundi itaunganishwa kupitia Uvinza (Kigoma) hadi Musongati (Burundi) huku Rwanda ikiunganishwa kupitia Isaka (Shinyanga) hadi Kigali. Hakika kazi inaendelea.

 

Aidha, kumekuwa na ukarabati na ujenzi wa meli na vivuko katika maeneo mbalimbali nchini ili kufanikisha usafiri na uchukuzi kupitia njia za majini.

 

Nishati

Kutokana na umuhimu wa kimkakati wa sekta ya nishati, kwenye Ilani ya 2020 – 2025, CCM ilikusudia kuimarisha zaidi eneo hili, ili kuhakikisha nchi inazalisha umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya uchumi wa viwanda na hata soko la nje ya nchi yetu. Ni kutokana na maelekezo hayo Watanzania wameshuhudia katika mwaka huu mmoja, Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais imechukua hatua madhubuti katika eneo hili pia, kuondoa changamoto ya umeme nchini kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuzalisha umeme pamoja na kuongeza vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo ili kuhakikisha maeneo yote ya nchini yanapata umeme wa uhakika hususan maeneo ya vijijini.

 

Kazi ya kuunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa, hasa katika mikoa minne iliyobakia ya Kagera, Kigoma, Katavi na Rukwa inaendelea. Maeneo hayo yatakuwa na umeme wa uhakika kutokana na mradi wa Rusumo unaotekelezwa kwa makubaliano ya kiserikali kati ya Tanzania, Rwanda na Burundi, kuzalisha megawati 80.

 

Serikali pia imeendelea kuweka mkazo katika kusimamia ukamilishaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), ambao utakapokamilika utazalisha megawati 2,115.

 

Kupitia ziara za kimkakati za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan nje ya nchi, Tanzania tumefanikiwa kusaini mikataba na hati za makubaliano ya ushirikiano katika kuendeleza miundombinu ya nishati, ikiwemo ya kupokelea na kuhifadhia mafuta na gesi itakayojengwa hapa hapa nchini, huku ikilenga kuhudumia ukanda mzima wa Afrika Mashariki.

 

Aidha, tumeona pia dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha mradi wa kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG), unaanza ili kupanua wigo wa uzalishaji wa nishati ya kutosha na uhakika. Hadi sasa mradi huo umefikia katika hatua ya majadiliano ya kimkataba na wawekezaji.

 

Diplomasia ya Uchumi, mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Katika eneo hili, CCM tulisema katika Ilani kuwa ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine ni fursa muhimu katika kuleta maendeleo na kudumisha amani. Hivyo Chama kilielekeza Serikali kuhakikisha uhusiano wa nchi kikanda na kimataifa unaendelezwa katika maeneo mbalimbali hususan kunufaika na diplomasia ya kiuchumi, huku Tanzania ikiendelea kuwa mstari wa mbele kuimarisha amani, uhuru na maslahi ya Taifa, kutekeleza mikakati na maazimio ya kikanda na kimataifa yanayohusiana na utawala bora na haki za binadamu.

 

Kipindi cha mwaka huu mmoja, kupitia ziara za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan nje ya nchi, kuhudhuria mikutano ya kimataifa, kufanya mazungumzo na wakuu wenzake wa nchi (au wawakilishi wao) na wakuu wa mashirika ya kimataifa, halikadhalika viongozi wa nchi zingine (au wawakilishi wao) na mashirika ya kimataifa kuja hapa nchini, sio tu kumeifungua zaidi nchi na uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa na kikanda kuzidi kuimarika na nchi yetu kunufaika kupitia kusainiwa kwa makubaliano na mikataba ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa, bali pia taswira ya Tanzania katika anga za kimataifa imeendelea kuchomoza na kung’aa, huku tukiendeleza umahiri wetu tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

 

Ulinzi na Usalama

Chama kinatambua kuwa uhakika wa amani, ulinzi na usalama ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha wananchi kuishi na kufanya shughuli za maendeleo, hivyo siku zote, hata kupitia Ilani ya 2020 – 2025, kimeihimiza Serikali kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu, raia wake na mali zao, ili kudumisha umoja, mshikamano, amani, utulivu ambazo ni tunu kuu za taifa letu.

 

Katika mwaka huu mmoja, sio tu vyombo vya dola vimeendelea kuitumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uaminifu, uzalendo na uadilifu mkubwa, lakini pia ulinzi na usalama wa mipaka uko sawasawa kudumisha Muungano wetu, kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, umoja, mshikamano, amani na usalama wa raia na mali zao, huku nchi yetu ikiendeleza ushiriki katika jitihada za utatuzi wa changamoto za amani katika nchi jirani na zingine, hususan kupitia juhudi za kikanda, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa. 

 

Mawasiliano na Habari

Katika kipindi hiki cha mwaka mmoja wa Serikali ya CCM, chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na mabadiliko makubwa kwenye sekta za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ambayo yamegusa moja kwa moja uhuru wa wananchi kujieleza na hivyo kusaidia uhuru wa habari kuongezeka nchini, hilo limeenda sambamba na uwekezaji kwenye sekta hizo, hivyo kuchangia maendeleo ya uchumi wan chi na kuongeza ajira na kipato. Kumefanyika mabadiliko katika Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010, Sheria ya Shirika la Posta ya 1993 pamoja na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

 

Pia baadhi ya kanuni zimebadilishwa, ikiwa ni pamoja na Kanuni za Utangazaji kwa Njia ya Kidigitali za Mwaka 2018, Kanuni za Leseni za mwaka 2018 na Kanuni za Maudhui ya Mtandao za mwaka 2020.

 

Tumeona namna Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan alivyoweka msisitizo kwenye suala la utekelezaji wa Mfumo wa Anawani za Makazi na Postikodi, ambapo tayari ameziangiza mamlaka zinazohusika, ikiwemo wizara na wakuu wa mikoa wote nchini kuhakikisha kuwa kila mwananchi, ofisi au biashara inatambuliwa na kufikiwa na bidhaa au huduma za kijamii na kiuchumi katika maeneo yao, ambapo pia utawezesha biashara au kazi mtandao kushamiri katika nyakati hizi za uchumi wa kidijitali.

 

Michezo na utamaduni (Kiswahili, utalii wa utamaduni)

Kwenye kipindi hiki cha mwaka mmoja cha Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, lugha yetu adhimu hatimae imekubaliwa na kuidhinishwa kuwa mojawapo ya lugha rasmi katika Umoja wa Afrika.

 

Aidha, tumeona kwa mara ya kwanza, ikiwa ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, wasanii 1,123 wamelipwa malipo ya mirabaha ya kazi zao za sanaa, baada ya shilingi milioni 312 kukusanywa kupitia utaratibu wa kisheria uliowekwa kwenye bajeti ya 2021 – 2022. Hili halijawahi kutokea.

 

Aidha, tumeona pia namna ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amehamasisha utalii wa utamaduni wa jamii zetu, huku pia akiweka mifumo ya kuwashirikisha machifu kama walinzi wa mila na desturi za Watanzania ili kunufaika na mchango wao.

 

Serikali pia imekamilisha hatua muhimu za ujenzi wa miundombinu ya michezo, ikiwa ni pamoja na usanifu wa uwanja wa soka wa Dodoma, viwanja vya mazoezi na kupumzikia wananchi maeneo ya Dar es Salaam, Dodoma na Geita.

 

Utalii – (The Tanzania Royal Tour)  

Katika Ilani ya 2020 – 2025 CCM ilisema kuwa sekta hii ina umuhimu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla, hasa upatikanaji wa fedha za kigeni, hivyo iliahidi na kuielekeza Serikali kuweka mkazo katika kupanua wigo wa bidhaa/mazao ya utalii ili sekta hiyo iendelee kuchangia zaidi katika pato la taifa. 

 

Katika eneo hili pia tumeona hamasa kubwa iliyowekwa na kusimamiwa na hata kuongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan mwenyewe moja kwa moja, hasa aliposhiriki kwenye kipindi cha The Tanzania Royal Tour ambacho, pamoja na kwamba maudhui yake yanatarajiwa kurushwa mwezi ujao duniani kote, tayari matanagazo yake ya awali tu, yamekuwa na matokeo chanya kuvuta watalii kutoka nje na ndani ya nchi yetu kutembelea na kujionea vivutio na utajiri mkubwa wa hifadhi za wanyama, maporomoko, ya maji, milima, misitu ya mazingira asilia, utamaduni, fukwe na malikale. 

 

Mkakati wa namna ya kukabiliana na Janga la Ugonjwa wa Uviko – 19, uliosimamiwa na kuongozwa na Mheshimiwa Rais mwenyewe, hasa alipounda Kamati ya Wataalam ili kuishauri serikali, uliifungua zaidi nchi yetu na hivyo kuwapatia imani wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani kuingia nchini kwa ajili ya utalii.

 

Tamati

Mwaka mmoja; zege haijalala, kazi inaendelea;

Kidumu Chama Cha Mapinduzi

Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo akizungumza na Wandishi wa Habari, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages