Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ameendeleza mwito wake wa kuzitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ( OAG), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OSG) na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwito huo ameutoa hivi karibuni mkoani Tanga wakati akizungumza na Mawakili wa Serikali wanaosimamia Ofisi hizo akiwa katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga mkoani humo.
"Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Feleshi amesisitiza ushirikiano kati ya Ofisi hizi tatu na kututaka tufanye kazi kwa kushirikiana", amesema Wakili wa Serikal Mwadamizi Rebecca Msalanhi, wakati akizungumza na Mwandishi wa habari hii.
Wakili Mwandamizi Rebecca, akaongeza kwamba, AG pia amezitaka Ofisi hizo kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na Taasisi nyingine zilizomo ndani ya mkoa huo kwa kutoa msaada wa kisheria pamoja na mambo mengine.
Aidha kwa mujibu wa Wakili Mwandamizi Rebecca, AG amemuagiza Mwakilishi huyo wa Mwanasheria Mkuu katika Mkoa wa Tanga kuanza mchakato wa kutafuta kiwanja katika Wilaya ya Mkinga.
Katika ziara hiyo ambayo ilijumuisha Uongozi wa Mahakama akiwamo Jaji Kiongozi Mhe. Mustapher Siyani, Makamishna Adv Julius Bundala Kalolo na Adv Genoveva Kato, pamoja na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga, walitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mahakama Mahakama ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Akiwa Mkoani Morogoro, Mwanasheria Mkuu huyo wa serikali alipewa heshima ya kupanda mti wa kumbukumbu katika Mahakama Kuu ya Mkoa huo. Ziara ya viongozi hao ilifanyika kuanzia tarahe 8 hadi 11, mwezi huu wa Machi, 2022.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi na Jaji Kiongozi Mustepher Siyani wakionyeshwa michoro ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga, AG alipokagua ujenzi wa Mahakama hiyo akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Tanga, akiambatana na Viongozi wa Mahakama, hivi karibuni.Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima na Mawakili wa Serikali Rebecca Msalanhi Ofisi ya Mwanasheria Mku wa Serikali Tanga Luciana Kikala Wakilli wa Serikali Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Tanga na Juma Maige Mwendesha Mashtaka wa Mkoa wa Tanga, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, wakati wa ziara yake Mkoani Tanga akiambatana na Viongozi wa Mahakama kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mkinga mkoani humo.Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Dk. Eliezer Feleshi akipanda mti wa kumbukumbu kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu ya Mkoa wa Morogoro, wakati wa ziara yake Mkoani humo akiambatana na Viongozi wa Mahakama. (Picha zote na Ofisi ya AG).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇