Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Timu za Yanga na Mbeya City zimeambulia suluhu ya bila kufungana na katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka uliopigwa leo Februari 5, 2022 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Temeke jijini Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo Yanga inafikisha alama 36 na kuendelea kuongoza ligi kwa alama nane zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC baada ya wote kucheza mechi 14.
Mbeya City yenyewe inafikisha pointi 23 katika mchezo wa 14, ingawa inabaki nafasi ya nne ikizidiwa alama moja na Azam FC.
Mechi nyingine ya Ligi Kuu NBC leo, Kagera Sugar imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Mabao ya Kagera Sugar yamefungwa na Erick Mwijage dakika ya 20 na 73, wakati la Coastal Union limefungwa na Vincent Abubakar dakika ya 54.
Kagera Sugar inafikisha alama 19 na kusogea nafasi ya tano, wakati Coastal Union inabaki na alama zake 17 katika nafasi ya nane baada ya wote kucheza mechi 14.
Nayo KMC imelazimishwa sare ya 1-1 na Biashara United katika dimba la Azam Complex, Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
KMC inafikisha alama 16 katika nafasi ya 10 na Biashara United inafikisha alama 12 katika nafasi ya 13 kwenye ligi ya timu 16 baada ya timu zote kucheza mechi 14.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇