Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda ameishauri Serikali na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia uwezekano wa kutoa elimu ya mlipa kodi kuanzia elimu ya msingi, kati, sekondari na vyuo ili kuwajengea mazoea ya kulipa kodi bila shurti.
Pinda ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kutumia viongozi wa dini kuelimisha waumini na watanzania kuhusu umuhimu wa kulipa kodi.
Ushauri na pongezi hizo alizitoa jijini hapa wakati wa mkutano wa Amani uliojumuisha viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini na serikali ambapo alitumia nafasi hiyo kuipongeza TRA kwa kuwaamini viongozi hao na kuwahamasisha watanzania kulipa kodi kwa kutumia majukwaa ya ibada.
“Mtu wa TRA ameona ana watu wanaoweza kumsaidia sababu ya uwezo tuliojaliwa na Mungu hivyo tuangalie suala hilo kupitia elimu ya msingi, kati na sekondari, vyuo maana wasipojazwa mawazo haya tangu wadogo ni tabu na ulimwengu wa leo huu nao ni shida tupu utandawazi improvement,”alisema.
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo amewaomba viongozi wa dini nchini kutumia majukwaa ya ibada kuhamasisha wanachi kulipa kodi kwa hiari na kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa yoyote.
Kayombo alisema serikali imeleta jambo zuri la wananchi kudai risiti kila wanapofanya manunuzi lakini kuna changamoto ya wengi kutodai.
“Niwaombe viongozi wa dini kwa sauti zenu za upole, zinazoheshimika tutumie sauti hizo kuhamasisha watanzania watekeleze wajibu wao wa kulipa kodi wakati wa mahubiri kwenye nyumba za ibada (Misikiti, makanisa).
…Nichukue fursa hii kuwaomba viongozi wangu wa dini mliopo hapa na mahali popote nchini usitoke bila kudai risiti, zungumzeni na waumini kupitia mahubiri kuhusu umuhimu wake ili kuwepo ukadiriaji kwa haki…
Asiyetoa risiti ana nia ya kijidhulumu yeye na serikali yake na wananchi wenzake na atatucheklewesha kwenye masuala ya upatikanaji wa dawa, barabara za lami, maji, umeme,”alisema Kayombo.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa nchini kuna ukanda mrefu wa bahari, maziwa na kumepakana nan chi nane hivyo kuna vichochoro vingi vya magendo ambavyo vinanufaisha baadhi ya watu na kusababisha ukusanyaji mapato kutoongezeka wakati lengo la kufikia zaidi ya sh. Trilioni 3 lipo.
Kayombo alifafanua kuwa suala hilo likiendelea kuna athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo bidhaa zinazoingia kupita sehemu isiyo sahihi kwa kutofanyiwa ukaguzi na Shirika la Viwango Tanzania(TBS) zinazoweza kuathiri afya za watanzania.
“Lakini kuna hatari nyingi kama silaha haramu, madawa ya kulevya ndio maana sisi kama TRA kazi yetu si kukusanya tuu bali kudhibiti bidhaa haramu zinazoweza kuingia nchini na kuvuruga amani,” alisema.
Alisisitiza kuwa wapo wafanyabiashara wanaojishughulisha na shuguli mbalimbali wasiosajiliwa licha ya kuwekwa utaratibu rahisi wa kujisajili kwa njia ya mtandao hivyo kuwataka kufanya hivyo ili nchi izidi kupata maendeleo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇