Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Baba mzazi wa aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, aliyefariki usiku wa kuamkia jana katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Mzee John Nchimbi atazikwa kesho katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mzee Nchimbi ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ikiwemo Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Katibu wa CCM wa mikoa ya Kigoma, Singida na Dar es Salaam, kwa nyakati tofauti na pia kuwa mkufunzi wa vyuo vya chama vya Ilonga na Kivukoni amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77.
Mbali na kuwahi kuhudumu nafasi mbalimbali katika CCM, Mzee Nchimbi amewahi pia kuwa mtumishi wa Serikali kwa kuhudumu katika nafasi kadhaa ikiwemo Ukamanda wa Polisi mikoa ya Morogoro na Mtwara ambako alistaafu mwaka 1996.
Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema, Baba yake amefariki Dunia wakati akiwa katika matibabu ya Ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.
“Mzee wetu alikuwa na matatizo ya moyo lakini siku tatu zilizopita hali yake ilibadilika na alichukuliwa kwenda kwenye vipimo Hospitali ya TMJ, Mikocheani, baada ya kupata vipimo kesho yake hali yake iliendelea kuwa mbaya kwa hiyo tukaamua kumuhamishia JKCI kwa ajili ya vipimo zaidi.
Na katika vipimo walibaini mishipa yake ya upande wa kulia na kushoto inayotoka kwenye moyo imeziba ambayo huwezi kuzibua kwa kutumia waya na ilitakiwa afanyiwe upasuaji mkubwa wa moyo ili kutengeneza njia nyingine na mingine kuibadilisha, Wakiwa kwenye mchakato wa kufanya hivyo ilipofika saa nane usiku wa kuamkia jana, Baba akafariki,” amesema Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kuhusu mazishi, John Nchimbi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto amesema taratibu za mazishi zinaendelea nyumbani kwa marehemu, Tabata jijini Dar es Salaam, lakini kwa sehemu kubwa ya mazishi hayo itazingatia itifaki mbalimbali kwa kuwa alikuwa mtumishi wa Chama na Serikali.
“Mzee wetu alikuwa Kamshina wa Jeshi la Polisi, alikuwa kwenye siasa kwa hiyo kutakuwa na miongozo ya kiserikali kwa sababu alilitumikia taifa kwa mara ya mwisho akiwa Kama Kamanda wa Polisi wa Mtwara kabla ya kustaafu mwaka 1996", amesema John Nchimbi na kuongeza kuwa ameacha mjane na watoto saba (7).
Kufuatia msiba huo, jana viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa CCM Komredi Daniel Chongolo akifuatana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, walifika nyumbani kwa marehemu Tabata Jijini Dar es Salaam na kutoa pole kwa Wanafamilia wakiongozwa na Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
Marehemu Mzee John Alfonso Nchimbi
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇